Sunnah ni nini? (sehemu ya 1 kati ya 2): Uteremsho kama Kurani
Maelezo: Makala fupi inayoelezea nini kinajumuisha Sunnah, na nafasi yake katika Sheria ya Kiislamu. Sehemu ya Kwanza: Ufafanuzi wa Sunnah, maana yake, na aina za ufunuo.
- Na The Editorial Team of Dr. Abdurrahman al-Muala (translated by islamtoday.com)
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 28 Aug 2022
- Ilichapishwa: 57
- Imetazamwa: 9,284
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Sunnah, kwa mujibu wa wasomi wa hadithi, ni kila kilichopokewa kutoka kwa Mtume kwa kauli zake, matendo yake, idhini zake za kimyakimya, utu wake, maelezo ya kimwili au wasifu wake. Haijalishi ikiwa habari inayohusiana inarejelea kitu kabla ya kuanza kwa utume wake wa kinabii, au baada yake.
Ufafanuzi wa maana hii:
Kauli za Mtume ni pamoja na kila alichosema Mtume kwa sababu mbalimbali katika nyakati tofauti. Kwa mfano, alisema:
“Hakika vitendo ni nia, na kila mtu atapata kulingana na alilokusudia.”
Matendo ya Mtume yanajumuisha kila alichofanya Mtume ambacho kilihusishwa na sisi kwa Maswahaba zake. Hii ni pamoja na jinsi alivyotawadha, jinsi alivyoswali, na jinsi alivyohiji.
Ridhaa za kimyakimya za Mtume ni pamoja na kila kitu ambacho Maswahaba wake walisema au walichofanya ambacho aidha alionyesha upendeleo kwake au angalau hakukipinga. Chochote ambacho kilikuwa na idhini ya kimyakimya ya Mtume ni sawa na kitu chochote alichosema au alichofanya mwenyewe.
Mfano wa hayo ni idhini waliyopewa Maswahaba walipotumia busara zao katika kuamua wakati wa kuswali kipindi cha Vita vya Bani Quraydhah. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaambia:
“Mmoja wenu asiswali swalah yake ya alasiri mpaka afike Bani Quraizhah.”
Masahaba hawakufika Bani Quraydhah mpaka baada ya machweo. Baadhi yao waliyachukulia maneno ya Mtume kihalisi na wakaahirisha swala ya Alasiri, wakisema: “Hatutaswali mpaka tufike huko.” Wengine walielewa kwamba Mtume alikuwa akiwaambia kuwa wafanye haraka katika safari yao, hivyo wakasimama na kuswali Swalah ya Alasiri kwa wakati wake.
Mtume alielewa kuhusu yale makundi mawili yalichokuwa yameamua, lakini hakukosoa kundi hata moja kati yao.
Ama kwa wasifu wa Mtume, hii itajumuisha kauli ifuatayo ya Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa mchafu wala muovu, wala hakuwa na sauti kubwa sokoni. Hangeweza katu kulipa unyanyasaji wa wengine kwa unyanyasaji wake mwenyewe. Badala yake, alikuwa mvumilivu na mwenye kusamehe.”
Maelezo ya kimwili ya Mtume yanapatikana katika kauli kama ile iliyosimuliwa na Anas (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa mrefu kupita kiasi wala hakuwa mfupi. Hakuwa mweupe sana wala mweusi. Nywele zake hazikuwa za kujikunja kupita kiasi wala zilizonyooka.”
Uhusiano baina ya Sunnah na Ufunuo
Sunnah ni ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume wake. Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“…na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima…” (Kurani 2:231)
Hekima inahusu Sunnah. Mwanafaqihi mkubwa al-Shafi’i anasema: “Mwenyezi Mungu anakitaja Kitabu ambacho ni Quran. Nimesikia kutoka kwa watu ambao ninawaona kuwa wana mamlaka juu ya Kurani kwamba Hekima ni Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mungu anasema:
Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia hisani kubwa Waumini pale alipotuma Mtume miongoni mwao kutoka miongoni mwao, anaye wasomea Aya zake na awatakase na kuwafundisha Kitabu na hikima.
Imebainika kutokana na aya zilizotangulia kwamba Mwenyezi Mungu alimfunulia Mtume wake Kurani na Sunnah, na kwamba alimuamuru kuzifikisha zote mbili kwa watu. Hadithi ya Mtume pia inathibitisha kuwa Sunnah ni ufunuo. Imesimuliwa kutoka kwa Mak’hul kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:
“Mwenyezi Mungu alinipa Kurani na yaliyo kama hayo kutokana na hekima.”
Al-Miqdam b. Ma’di Karab anasimulia kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:
“Nimepewa Kitabu pamoja na kitu mfano wake.”
Hisani b. Atiyyah anasimulia kwamba Jibrili alikuwa akimjia Mtume na Sunnah kama vile alivyokuwa akimjia na Kurani.
Maoni yanayotoka kwa Mtume hayakuwa tu mawazo yake mwenyewe au mijadala juu ya jambo; ni kile ambacho Mungu alimfunulia. Kwa njia hii, Mtume alikuwa tofauti na watu wengine. Aliungwa mkono na ufunuo. Alipotumia fikra zake mwenyewe na kuwa sahihi, Mungu huthibitisha, na ikiwa atafanya kosa katika kufikiria kwake, Mungu alikuwa akimsahihisha na kumwongoza kwenye kweli.
Kwa sababu hii, inasimuliwa kwamba Khalifa Umar alisema akiwa kwenye mimbari: “Enyi watu! Maoni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yalikuwa sahihi kwa sababu tu Mwenyezi Mungu alimfunulia. Ila kwa maoni yetu, si chochote ila ni fikra na dhana tu.”
Ufunuo alioupata Mtume ulikuwa wa aina mbili:
A. Ufunuo wa taarifa: Mwenyezi Mungu humjulisha jambo kwa njia ya ufunuo kwa namna moja au nyingine kama ilivyotajwa katika aya ifuatayo ya Kurani:
“Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.” (Kurani 42:51)
Aishah alisimulia kwamba al-Harith b. Hisham alimuuliza Mtume jinsi ufunuo unavyomjia , na Mtume akajibu:
“Wakati mwingine, malaika huja kwangu kama mlio wa kengele, na hii ndiyo huwa ngumu zaidi kwangu. Inanielemea na ninaiweka kwenye kumbukumbu anayosema. Na wakati mwingine malaika anakuja kwangu katika umbo la mwanadamu na kusema nami na ninaweka kwenye kumbukumbu anayosema.”
Aishah anasema:
“Niliwahi kumwona wakati ufunuo ukimjia siku ya baridi sana. Ulipoisha, uso wake ulikuwa umejaa jasho.”
Wakati mwingine, alikuwa akiulizwa juu ya jambo fulani, lakini alikuwa akikaa kimya hadi ufunuo ulipomjia. Kwa mfano, wapagani wa Makkah walimuuliza kuhusu roho, lakini Mtume alinyamaza mpaka Mwenyezi Mungu alipoteremsha:
Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: 'Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu'. (Kurani 17:85)
Pia aliulizwa jinsi ya urithi unavyogawanywa, lakini hakujibu mpaka Mungu alipomfunulia:
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu…” (Kurani 4:11)
B. Ufunuo wa Uthibitisho: Hapa ndipo Mtume alipotumia hukumu yake katika jambo. Iwapo mawazo yake yalikuwa sahihi, ufunuo ulimjia kuthibitisha, na kama hakuwa sahihi, ufunuo ungekuja kumsahihisha, na kuwa kama ufunuo mwingine wowote wenye kuelimisha. Tofauti pekee hapa ni kwamba ufunuo ulikuja kama matokeo ya kitendo ambacho Mtume alikifanya kwanza peke yake.
Katika matukio kama hayo, Mtume aliachwa atumie busara yake katika jambo. Ikiwa angechagua kilicho sawa, basi Mungu angethibitisha chaguo lake kupitia ufunuo. Ikiwa angechagua kwa makosa, Mungu angemsahihisha ili kulinda uaminifu-maadili ya imani. Mwenyezi Mungu asingemruhusu Mtume Wake kufikisha ujumbe usio sahihi kwa watu wengine, kwa kuwa hatua hii itawafanya wafuasi wake walifuate kosa hilo. Hili litakuwa kinyume na hekima ya kutuma Mitume, ambayo ni kuwa watu hawatakuwa na hoja juu ya Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, Mtume alilindwa kutokana na kutumbukia kwenye upotofu, kwani kama akikosea, ufunuo ulikuja kumsahihisha.
Maswahaba wa Mtume walijua kuwa uidhinishaji wa kimyakimya wa Mtume kwa hakika ulikuwa ni ridhaa ya Mwenyezi Mungu kwa sababu kama wangefanya jambo ambalo lipo kinyume na Uislamu wakati wa uhai wa Mtume, ufunuo ungeshuka na kulaani waliyoyafanya.
Jabir alisema: “Tulikuwa tukifanya jambo la kukatiza[1] zamani tangu Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa hai.” Sufyan, mmoja wa wapokezi wa Hadiyth hii, alisema: “Kama kitu kama hiki kingeharamishwa, Kurani ingekiharamisha.
Vielezi-chini:
[1] kukatiza: Kutolewa kwa uume kabla ya kutolewa kwa manii wakati wa tendo la ndoa. – IslamReligion.com
Ongeza maoni