Kisa cha Isa na Maryamu katika Kurani Tukufu (sehemu ya 1 kati ya 3): Maryamu
Maelezo: Mfululizo huu wa sehemu tatu una aya nyingi kutoka kwa Kurani Tukufu kuhusu Maryamu (Mama wa Isa) pamoja na kuzaliwa kwake, utoto wake, sifa zake za kibinafsi, na kuzaliwa kimiujiza kwa Isa.
- Na IslamReligion.com
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 01 Jan 2024
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,292
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Kuzaliwa kwa Maryamu
“Hakika Mwenyezi Mungu alimteua Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote. Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua. Aliposema mke wa Imran: ‘Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.’ Basi alipomzaa alisema: ‘Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shetani aliyelaaniwa.'" (Kurani 3: 33-36)
Wakati wa Utotoni wa Maryamu
“Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipoingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: ‘Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi?’ Naye akasema: ‘Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hesabu.’” (Kurani 3:37)
Maryamu, Mnyenyekevu
“Na kumbuka pale malaika waliposema: ‘Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteua, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote.’ ‘Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao.’ Hizi ni khabari za ghaibu tunazokufunulia; nawe hukuwa nao walipokuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipokuwa wakishindana.” (Kurani 3:42-44)
Habari njema ya kuzaliwa mtoto mchanga
“Na pale malaika waliposema: ‘Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana kwa) neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye heshima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa waliokaribishwa (kwa Mwenyezi Mungu).’ ‘Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.’ Maryamu akasema: ‘Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanadamu?’ Mwenyezi Mungu akasema: ‘Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapohukumu jambo, huliambia: Kuwa!’ Likawa. Na atamfunza kuandika na Hekima na Taurati na Injili. Na ni mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: ‘Mimi nimekujieni na ishara kutoka kwa Mola wenu Mlezi, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnachokila na mnachoweka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo ishara kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini. Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlioharimishiwa, na nimekujieni na ishara kutokana na Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.’” (Kurani 3:45-51)
“Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipojitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki. Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu. (Maryamu) akasema: ‘Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mcha Mungu.’[1] (Malaika) akasema: ‘Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliyetakasika.’ (Maryamu) akasema: ‘Nitampataje mwana hali mwanadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba?’ (Malaika) akasema: Ndio hivyo hivyo! Mola wako Mlezi amesema: ‘Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu, na rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo liliokwisha hukumiwa.’”[2] (Kurani 19:16-21)
Utungaji mimba wa Bikira
“Na mwanamke aliyelinda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni ishara kwa walimwengu.”[3] (Kurani 21:91)
Kuzaliwa kwa Isa
“Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka mahali pa mbali. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: ‘Laiti ningelikufa kabla ya haya, na nikawa niliyesahaulika kabisa!’ Pakatangazwa kutoka chini yake: ‘Usihuzunike! Hakika Mola wako Mlezi amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji! Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.’ Akaenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: ‘Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu!’ ‘Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.’ Akawaashiria (mtoto). Wakasema: ‘Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi.’ Akasema (Isa): ‘Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya Nabii.[4] Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu ni hai. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.’” (Kurani 19:22-33)
“Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: ‘Kuwa!’ Basi akawa.”[5] (Kurani 3:59)
“Na tukamfanya mwana wa Maryamu na mama yake kuwa ni ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipoinuka penye utulivu na chemchemu za maji.”[6] (Kurani 23:50)
Ubora wa Maryamu
“Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano wa walioamini - mkewe Firauni, aliposema: ‘Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhalimu. Na Maryamu binti wa Imran, aliyelinda ubikira wake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa watiifu.” (KuranI 66:11-12)
Rejeleo la maelezo:
[1] Mwingi wa Rehema ni moja ya majina ya Mungu katika Kurani.
[2] Yesu ni ishara ya nguvu ya Mungu, ambapo Mungu aliwaonyesha watu kuwa angeweza kumuumba Isa bila baba, kama alivyomuumba Adam bila wazazi wowote. Yesu pia ni ishara kwamba Mungu ana uwezo wa kufufua watu wote baada ya wao kufa, kwani yule ambaye anaumba kutoka kutokuwepo kitu anaweza bila shida yoyote kurudisha uhai. Yeye pia ni ishara ya Siku ya Hukumu, wakati atakaporudi duniani na kumuua Masihi Dajali katika Nyakati za Mwisho wa dunia.
[3] Vivyo hivyo, kama vile Mungu alivyomuumba Adam bila baba wala mama, kuzaliwa kwa Isa kulitokana na mama bila baba. Ili jambo litokee, ilitosha Mungu kusema "Kuwa" na likawa; kwa sababu Mungu ana uwezo juu ya vitu vyote.
[4] Utume ni nafasi ya juu zaidi na yenye kuheshimika ambayo mwanadamu anaweza kuifikia. Mtume ni mtu anayepokea wahyi au ufunuo kutoka kwa Mungu kupitia Malaika Jibril.
[5] Adam aliumbwa wakati Mungu alisema, "Kuwa," na yeye kuwa bila baba wala mama. Vivyo hivyo Yesu aliumbwa kutokana na Neno la Mungu. Ikiwa mazazi ya ajabu ya Yesu yanamfanya kuwa Mungu, basi Adam anastahiki zaidi uungu huo kwa sababu Isa angalau alikuwa na mzazi mmoja, wakati Adam hakuwa na yeyote. Kwa kuwa Adam sio Mungu, vivyo hivyo Yesu sio Mungu, walakini wote ni watumishi wanyenyekevu wa Mungu.
[6] Hapa ndipo Maryamu alipojifungua Yesu.
Kisa cha Isa na Maryamu katika Kurani Tukufu (sehemu ya 2 kati ya 3): Isa I
Maelezo: Sehemu hii inachunguza maisha ya Mtume Isa, ujumbe wake, miujiza yake, wanafunzi wake na kile kinachotajwa juu yao katika Kurani Tukufu.
- Na IslamReligion.com
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,316
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Isa Mtume
“Semeni nyinyi: ‘Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na waliyopewa Musa na Isa, na pia waliyopewa manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutofautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.’” (Kurani 2:136)
“Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyowapelekea wahyi Nuhu na manabii waliokuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.” (Kurani 4:163)
“Masihi mwana wa Maryamu si chochote ila ni mtume. Wamekwishapita mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli.[1] Wote wawili walikuwa wakila chakula.[2] Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.” (Kurani 5:75)
“Hakuwa yeye (Isa) ila ni mtumishi tuliyemneemesha, na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.” (Kurani 43:59)
Ujumbe wa Isa
“Na tukawafuatishia hao Isa mwana wa Maryamu, kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili, iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu.” (Kurani 5:46)
“Enyi watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa, mwana wa Maryamu, ni mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake.[3] Basi muaminini Mwenyezi Mungu na mitume wake. Wala msiseme: ‘Utatu.’ Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliyomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha. Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala malaika waliokaribishwa.[4] Na watakaoona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.” (Kurani 4:171-172)
“Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.[5] Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao waliokufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu!” (Kurani 19:34-37)
“Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: ‘Nimekujieni na hekima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii mimi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.’ Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya Siku chungu.” (Kurani 43:63-65)
“Na Isa mwana wa Maryamu aliposema: ‘Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad.’[6] Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: ‘Huu ni uchawi ulio dhahiri!’”[7] (Kurani 61:6)
Miujiza ya Isa
“(Maryamu) akawaashiria (mtoto). Wakasema: ‘Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi.’ Akasema (Isa): ‘Hakika mimi ni mtumishi wa Mwenyezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya mtume.[8] Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu ni hai. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.’” (Kurani 19:29-33)
(Miujiza zaidi imetajwa chini ya kichwa: Habari njema ya mtoto mchanga aliyezaliwa)
Meza Iliyoandaliwa (vyakula) kutoka Mbinguni kwa idhini ya Mungu
“Wanafunzi waliposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?’ Akasema: ‘Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini wa kweli.’ Wakasema: ‘Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.’ Akasema Isa mwana wa Maryamu: ‘Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku.’ Mwenyezi Mungu akasema: ‘Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekana baadaye, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.’” (KuranI 5:112-115)
Isa na Wanafunzi Wake
“Enyi mlioamini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Isa mwana wa Maryamu kuwaambia wanafunzi wake: ‘Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?’ Wakasema wanafunzi: ‘Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!’ Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walioamini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.”[9] (Kurani 61:14)
“Na nilipowafunulia wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: ‘Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.’” (Kurani 5:111)
“Tena tukafuatisha nyuma yao mitume wetu wengine, na tukamfuatisha Isa mwana wa Maryamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wapotovu. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.”[10] (Kurani 57:27-29)
Rejeleo la maelezoi:
[1] Hili neno la Kiarabu linaashiria kiwango cha juu kabisa cha imani kinachowezekana, ambapo juu yake zaidi ni utume.
[2] Masihi na mama yake mcha Mungu walikuwa wakila, na hiyo si tabia ya Mungu, ambaye hali wala hanywi. Pia, anayekula anajisaidia kwa kwenda haja, na hii haiwezi kuwa sifa ya Mungu. Isa hapa anafananishwa na wajumbe wote watukufu waliomtangulia: ujumbe wao ulikuwa uleule, na hadhi yao, ya kuwa viumbe walioumbwa na wala wao sio Mungu, inafanana. Heshima kuu zaidi inayoweza kupewa mwanadamu ni utume, na Isa ni mmoja wa mitume watano wanaoheshimika sana. Tazama aya 33:7 na 42:13
[3] Isa anaitwa neno au roho kutoka kwa Mungu kwa sababu aliumbwa Mungu aliposema, “Kuwa,” naye akawa. Katika hilo yeye ni kiumbe wa pekee, kwa sababu wanadamu wote, isipokuwa Adam na Hawa, wameumbwa kutokana na wazazi wawili. Lakini licha ya upekee wake, Isa anafanana na kila mtu mwingine kwa kuwa yeye si Mungu, bali ni kiumbe chenye kufa.
[4] Kila kitu na kila mtu mwingine isipokuwa Mungu ni mwabudu au mtumwa wa Mungu. Aya hiyo inasisitiza kwamba Masihi kamwe hawezi kudai hadhi iliyo juu ya ile ya mwabudu wa Mungu, kinyume chake ni kuwa alitupilia mbali madai yoyote ya uungu wake. Na kwa hakika hawezi kamwe kudharau nafasi hiyo ya kuwa mwabudu au mtumwa wa Mungu, kwa sababu ndiyo heshima ya juu kabisa ambayo mwanadamu yeyote angeweza kuitamani.
[5] Ikiwa uumbaji wa Isa bila baba unamfanya kuwa mwana wa Mungu, basi kila kitu kilichoumbwa kama Isa bila mtangulizi kinapaswa kuwa cha kiungu pia, na hiyo inajumuisha Adam, Hawa, wanyama wa kwanza, na dunia hii yote pamoja na milima na maji yake. Lakini Isa aliumbwa kama vitu vyote duniani, Mungu aliposema, “Kuwa,” naye akaumbwa.
[6] Hili ni jina jingine la Mtume Muhammad.
[7] Hii inaweza kurejelea mitume wote wawili, Isa na Muhammad, amani iwe juu yao. Walipokuja na ujumbe kutoka kwa Mungu kwa watu wao, walituhumiwa kuleta uchawi.
[8] Utume ni cheo cha juu kabisa na cha heshima ambacho mwanadamu anaweza kufikia. Nabii ni yule anayepokea wahyi au ufunuo kutoka kwa Mungu kupitia Malaika Jibril. Mjumbe ni nabii anayepokea kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sheria za kuwafikishia watu wake. Isa alipata heshima kuu ya kuwa nabii na mjumbe.
[9] Ushindi wa waumini ulikuja kupitia ujumbe wa Uislamu, na ulikuwa ni ushindi wa kimwili na wa kiroho. Uislamu uliondoa shaka yote juu ya Isa na ukatoa uthibitisho wa utume wake, na huo ndio ulikuwa ushindi wa kiroho. Uislamu pia ulienea kimwili, jambo ambalo liliwapa waumini katika ujumbe wa Isa kimbilio na nguvu dhidi ya adui yao, na huo ndio ulikuwa ushindi wa kimwili.
[10] Mungu humpa muongozo amtakaye, bila kujali asili na rangi. Na watu wanapoamini, Mungu huwaheshimu na kuwainua juu kuliko mtu mwingine yeyote. Lakini wanapokufuru, Mwenyezi Mungu huwashusha ingawa walikuwa waheshimiwa hapo mwanzoni.
Kisa cha Isa na Maryamu katika Kurani Tukufu (sehemu ya 3 kati ya 3): Isa II
Maelezo: Sehemu hii inaangazia aya za Kurani Tukufu zinazozungumzia ulinzi wa Mwenyezi Mungu kwa Isa, wafuasi wake, ujio wake wa pili katika ulimwengu huu na yale atakayokumbana nayo Siku ya Kiyama.
- Na IslamReligion.com
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 3
- Imetazamwa: 4,338
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Shauku ya Kristo
“Isa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: ‘Ni nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?’ Wanafunzi wake wakasema: ‘Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu.’[1] Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata huyu mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia.’ Na makafiri walipanga mipango, na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.[2] Pale Mwenyezi Mungu aliposema: ‘Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkikhitalifiana.’” (Kurani 3:52-55)
“Na kwa kusema kwao: ‘Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu.[3] Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi wowote nayo, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimtukuza kwake.[4] na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.” (Kurani 4:157-158)
Wafuasi wa Yesu
“Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikilia elimu hii waambie: ‘Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.’ Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hekima. Na kama wakigeuka, basi Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu. Sema: ‘Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi[5] Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu[6].’ Na, wakigeuka basi semeni: ‘Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.’” (Kurani 3:61-64)
“Hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu.’ Sema: ‘Ni nani mwenye kumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi?’ Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu. Na Mayahudi na Wakristo wanasema: ‘Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.’ Sema: ‘Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya madhambi yenu?’ Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine aliowaumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.” (Kurani 5:17-18)
“Hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu!’ Na hali Masihi mwenyewe alisema: ‘Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru.’ Kwa hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu.’[7] Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayoyasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanaokufuru. Je, hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.” (Kurani 5:72-74)
“Na Mayahudi wanasema: ‘Uzeir ni mwana wa Mungu,’[8] Na Wakristo wanasema: ‘Masihi ni mwana wa Mungu.’ Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya waliokufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa! Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi mwana wa Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayomshirikisha nayo.”[9] (Kurani 9:30-31)
“Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.” (Kurani 9:34)
Ujio wa Pili
“Na hawi katika watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake.[10] Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.”[11] (Kurani 4:159)
“Na kwa hakika yeye (Isa) ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka,[12] na nifuateni. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.” (Kurani 43:61)
Yesu Siku ya Kiyama
“Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipotengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipowaponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipokukinga na Wana wa Israili ulipowajia na hoja zilizo wazi,’ na wakasema waliokufuru miongoni mwao: ‘Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!’” (Kurani 5:110)
“Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu?’[13]’ (Na Isa) atasema: ‘Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyofichikana.’[14] ‘Sikuwaambia lolote ila uliyoniamrisha, nayo ni: ‘Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi.’ Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao. Na uliponifisha ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu. Ukiwaadhibu basi hao ni waja wako. Na ukiwasamehe basi Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.’[15] Mwenyezi Mungu atasema: ‘Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.’ Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu.” (Kurani 5:116-120)
Rejeleo la maelezo:
[1] Jina lililotolewa la wanafunzi katika Kurani ni al-Hawariyyun, ambalo linamaanisha waliotakaswa, kama rangi nyeupe. Pia inaripotiwa kuwa walikuwa wakivaa nguo nyeupe.
[2] Isa alipaishwa katika hali ya usingizi. Neno linalotumika hapa ni wafah, ambalo linaweza kumaanisha usingizi au kifo. Kwa Kiarabu, usingizi huitwa kifo kidogo. Tazama pia aya 6:60 na 39:42, ambapo neno wafah hurejelea usingizi na sio kifo. Kwa kuwa aya ya 4:157 inakanusha kuuawa na kusulubishwa kwa Isa, na kwa kuwa kila mwanadamu hufa mara moja lakini Isa anatakiwa kurudi duniani, tafsiri pekee iliyobaki ya aya hiyo ni kulala.
[3] Wajihi wa mfanano wa Isa uliwekwa kwa mwingine, na ni mtu huyo ndiye, sio Isa, aliyesulubiwa. Kwa mujibu wa maelezo kadhaa ya Kurani, aliyesulubiwa alikuwa mmoja wa wanafunzi, aliyekubali afananishwe na Isa, na kujifia shahidi ili kumwokoa Isa kwa malipo ya peponi.
[4] Isa alipaishwa akiwa mzima wa mwili na roho, na hakufa. Bado anaishi huko juu, na atarudi kuelekea wakati wa mwisho wa dunia. Baada ya kutimiza daraka lake duniani, hatimaye atakufa.
[5] Hivi ndivyo mitume wote wa Mungu walilingania na kukubaliana. Na kwa hivyo, kauli hii sio ya kundi moja pekee, bali ni misingi ya kawaida kwa wale wanaotaka kumwabudu Mungu.
[6] Mtu anapomtii mwanadamu mwingine kwa kumuasi Mungu, anakuwa amemfanya kuwa bwana badala ya Mungu.
[7] Kwa kurejelea Utatu.
[8] Ingawa sio Mayahudi wote waliiamini, walishindwa kuishutumu (tazama aya 5:78-79). Dhambi linaporuhusiwa kuendelea na kuenea bila kupingwa, jamii nzima inapatilizwa kwa kutowajibika.
[9] Wanachuoni wa dini ndio wenye elimu, na watawa ndio waliozama katika ada na ibada. Wote wawili wanachukuliwa kuwa viongozi wa kidini na viigizo, na kupitia ushawishi wao wanaweza kuwapotosha watu.
[10] Kiwakilishi katika "kifo chake" kinaweza kurejelea Isa au mtu kutoka kwa watu wa Maandiko. Ikiwa inamrejelea Isa, inamaanisha kwamba watu wote wa Maandiko Matakatifu watakuja kumwamini Isa atakaporudi mara ya pili duniani na kabla ya kifo chake. Kisha Isa atathibitisha kwamba yeye ni mtume kutoka kwa Mungu, sio Mungu wala mwana wa Mungu, na atawataka watu wote kumwabudu Mungu peke yake na kujisalimisha Kwake katika Uislamu. Ikiwa kiwakilishi kinamrejelea mtu mmoja mmoja kutoka kwa watu wa Kitabu, basi aya hiyo ina maana kwamba kila mmoja wao ataona kabla tu ya kufa kwake ni nini kitakachomshawishi kwamba Isa alikuwa mtume wa kweli kutoka kwa Mungu, na sio Mungu. Lakini imani hiyo wakati huo haitamnufaisha, kwa kuwa haitokani na uchaguzi huru, bali anapowaona malaika wa adhabu.
[11] Tazama aya 5:116-118.
[12] Ujio wa pili wa Yesu kutakuwa ishara kwamba Siku ya Hukumu imekaribia.
[13] Kuabudu wengine pamoja na Mungu ni sawa na kuwaabudu wao badala ya Mungu. Yote mawili yanamaanisha kuwa ibada inaelekezwa na kufanyiwa mtu mwingine asiyekuwa Mungu, lakini Mungu ndiye Pekee anayefaa kuabudiwa.
[14] Mungu, kama Isa alivyosema, anajua kwamba Isa hakulingania ibada ifanywe kwa ajili yake mwenyewe au ya mama yake. Lengo la swali ni kuwaelekeza wale wanaomwabudu Isa au Mariamu kwamba kama wangekuwa wafuasi wa kweli wa Isa, wangeacha mazoea hayo, kwa sababu Isa hakuwaita kwayo kamwe. Lakini ikiwa wataendelea, basi wajue kwamba Isa atawakana Siku ya Mwisho, na kwamba wamekuwa hawamfuati, bali wanafuata tu matakwa yao binafsi.
[15]Kwa maneno mengine, Wewe unamjua ni nani anayestahiki adhabu, basi utamuadhibu. Na unamjua ni nani anayestahiki kusamehewa, basi utamsamehe. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu, na Wewe ni Mwenye hekima katika kuendesha kila jambo, basi unawasamehe wanaostahiki msamaha.
Ongeza maoni