Kisa cha Isa na Maryamu katika Kurani Tukufu (sehemu ya 2 kati ya 3): Isa I
Maelezo: Sehemu hii inachunguza maisha ya Mtume Isa, ujumbe wake, miujiza yake, wanafunzi wake na kile kinachotajwa juu yao katika Kurani Tukufu.
- Na IslamReligion.com
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,366 (wastani wa kila siku: 3)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Isa Mtume
“Semeni nyinyi: ‘Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na waliyopewa Musa na Isa, na pia waliyopewa manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutofautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.’” (Kurani 2:136)
“Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyowapelekea wahyi Nuhu na manabii waliokuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.” (Kurani 4:163)
“Masihi mwana wa Maryamu si chochote ila ni mtume. Wamekwishapita mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli.[1] Wote wawili walikuwa wakila chakula.[2] Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.” (Kurani 5:75)
“Hakuwa yeye (Isa) ila ni mtumishi tuliyemneemesha, na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.” (Kurani 43:59)
Ujumbe wa Isa
“Na tukawafuatishia hao Isa mwana wa Maryamu, kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili, iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu.” (Kurani 5:46)
“Enyi watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa, mwana wa Maryamu, ni mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake.[3] Basi muaminini Mwenyezi Mungu na mitume wake. Wala msiseme: ‘Utatu.’ Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliyomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha. Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala malaika waliokaribishwa.[4] Na watakaoona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.” (Kurani 4:171-172)
“Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.[5] Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao waliokufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu!” (Kurani 19:34-37)
“Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: ‘Nimekujieni na hekima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii mimi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.’ Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya Siku chungu.” (Kurani 43:63-65)
“Na Isa mwana wa Maryamu aliposema: ‘Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad.’[6] Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: ‘Huu ni uchawi ulio dhahiri!’”[7] (Kurani 61:6)
Miujiza ya Isa
“(Maryamu) akawaashiria (mtoto). Wakasema: ‘Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi.’ Akasema (Isa): ‘Hakika mimi ni mtumishi wa Mwenyezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya mtume.[8] Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu ni hai. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.’” (Kurani 19:29-33)
(Miujiza zaidi imetajwa chini ya kichwa: Habari njema ya mtoto mchanga aliyezaliwa)
Meza Iliyoandaliwa (vyakula) kutoka Mbinguni kwa idhini ya Mungu
“Wanafunzi waliposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?’ Akasema: ‘Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini wa kweli.’ Wakasema: ‘Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.’ Akasema Isa mwana wa Maryamu: ‘Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku.’ Mwenyezi Mungu akasema: ‘Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekana baadaye, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.’” (KuranI 5:112-115)
Isa na Wanafunzi Wake
“Enyi mlioamini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Isa mwana wa Maryamu kuwaambia wanafunzi wake: ‘Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?’ Wakasema wanafunzi: ‘Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!’ Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walioamini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.”[9] (Kurani 61:14)
“Na nilipowafunulia wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: ‘Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.’” (Kurani 5:111)
“Tena tukafuatisha nyuma yao mitume wetu wengine, na tukamfuatisha Isa mwana wa Maryamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wapotovu. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.”[10] (Kurani 57:27-29)
Rejeleo la maelezoi:
[1] Hili neno la Kiarabu linaashiria kiwango cha juu kabisa cha imani kinachowezekana, ambapo juu yake zaidi ni utume.
[2] Masihi na mama yake mcha Mungu walikuwa wakila, na hiyo si tabia ya Mungu, ambaye hali wala hanywi. Pia, anayekula anajisaidia kwa kwenda haja, na hii haiwezi kuwa sifa ya Mungu. Isa hapa anafananishwa na wajumbe wote watukufu waliomtangulia: ujumbe wao ulikuwa uleule, na hadhi yao, ya kuwa viumbe walioumbwa na wala wao sio Mungu, inafanana. Heshima kuu zaidi inayoweza kupewa mwanadamu ni utume, na Isa ni mmoja wa mitume watano wanaoheshimika sana. Tazama aya 33:7 na 42:13
[3] Isa anaitwa neno au roho kutoka kwa Mungu kwa sababu aliumbwa Mungu aliposema, “Kuwa,” naye akawa. Katika hilo yeye ni kiumbe wa pekee, kwa sababu wanadamu wote, isipokuwa Adam na Hawa, wameumbwa kutokana na wazazi wawili. Lakini licha ya upekee wake, Isa anafanana na kila mtu mwingine kwa kuwa yeye si Mungu, bali ni kiumbe chenye kufa.
[4] Kila kitu na kila mtu mwingine isipokuwa Mungu ni mwabudu au mtumwa wa Mungu. Aya hiyo inasisitiza kwamba Masihi kamwe hawezi kudai hadhi iliyo juu ya ile ya mwabudu wa Mungu, kinyume chake ni kuwa alitupilia mbali madai yoyote ya uungu wake. Na kwa hakika hawezi kamwe kudharau nafasi hiyo ya kuwa mwabudu au mtumwa wa Mungu, kwa sababu ndiyo heshima ya juu kabisa ambayo mwanadamu yeyote angeweza kuitamani.
[5] Ikiwa uumbaji wa Isa bila baba unamfanya kuwa mwana wa Mungu, basi kila kitu kilichoumbwa kama Isa bila mtangulizi kinapaswa kuwa cha kiungu pia, na hiyo inajumuisha Adam, Hawa, wanyama wa kwanza, na dunia hii yote pamoja na milima na maji yake. Lakini Isa aliumbwa kama vitu vyote duniani, Mungu aliposema, “Kuwa,” naye akaumbwa.
[6] Hili ni jina jingine la Mtume Muhammad.
[7] Hii inaweza kurejelea mitume wote wawili, Isa na Muhammad, amani iwe juu yao. Walipokuja na ujumbe kutoka kwa Mungu kwa watu wao, walituhumiwa kuleta uchawi.
[8] Utume ni cheo cha juu kabisa na cha heshima ambacho mwanadamu anaweza kufikia. Nabii ni yule anayepokea wahyi au ufunuo kutoka kwa Mungu kupitia Malaika Jibril. Mjumbe ni nabii anayepokea kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sheria za kuwafikishia watu wake. Isa alipata heshima kuu ya kuwa nabii na mjumbe.
[9] Ushindi wa waumini ulikuja kupitia ujumbe wa Uislamu, na ulikuwa ni ushindi wa kimwili na wa kiroho. Uislamu uliondoa shaka yote juu ya Isa na ukatoa uthibitisho wa utume wake, na huo ndio ulikuwa ushindi wa kiroho. Uislamu pia ulienea kimwili, jambo ambalo liliwapa waumini katika ujumbe wa Isa kimbilio na nguvu dhidi ya adui yao, na huo ndio ulikuwa ushindi wa kimwili.
[10] Mungu humpa muongozo amtakaye, bila kujali asili na rangi. Na watu wanapoamini, Mungu huwaheshimu na kuwainua juu kuliko mtu mwingine yeyote. Lakini wanapokufuru, Mwenyezi Mungu huwashusha ingawa walikuwa waheshimiwa hapo mwanzoni.
Ongeza maoni