Brandon Toropov, Mkristo wa zamani, Marekani (sehemu ya 2 kati ya 2)
Maelezo: Jitihada za mtu binafsi za kujifunza mistari halisi zaidi ya Biblia, mistari ya Q, zinamwongoza kwa Uislamu. Sehemu ya pili: Ulinganisho na Qur'ani.
- Na Brandon Toropov
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,849 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Kuzingatia Maneno ya Injili kwa Makini
Hususan, nilikuwa nikifuatilia kwa makini utafiti uliofanywa ambao ulionyesha kuwa matabaka ya zamani zaidi ya Injili yalionyesha chanzo cha mdomo cha mapema sana kinachojulikana kama Q, na kwamba kila kundi la maneno ya Yesu, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake, linahitajika kutathminiwa kwa sifa zake lenyewe, na sio kama sehemu ya nyenzo simulizi zilizolizunguka.
Hii ni kwa sababu nyenzo hizo simulizi ziliongezwa miaka mingi baadaye.
Simulizi ya Shahidi?
Kwa kweli, nilivyotafiti somo hili kwa zaidi, ndivyo nilivyojikuta nikifikiria mazungumzo hayo kuhusu Injili ya Yohana kati yangu mimi na kuhani wangu. Nilitambua kwamba kile ambacho hakutaka au hakuweza kuniambia ni kwamba mwandishi/waandishi wa Injili ya Yohana walidanganya. Ilikuwa wazi kuwa hayo siyo masimulizi ya shahidi, ingawa wailidai hivyo.
Nilikuwa katika hali ya ajabu. Kwa hakika nilifurahia ushirika wa Wakristo katika kanisa langu, ambao wote walikuwa watu wenye nia nzuri na wenye kusali. Kuwa mwanachama wa jumuiya ya kidini ilikuwa muhimu kwangu. Hata hivyo nilikuwa na shaka kubwa kimantiki kuhusu historia inayodaiwa ya simulizi za Injili. Zaidi ya hayo, nilikuwa nikizidi kupata ujumbe tofauti kutoka kwa maneno ya Yesu katika Injili kuliko ule ambao Wakristo wenzangu walikuwa wakiupata.
Kukabiliana na Mafundisho ya Utatu
Nilivyozidi kutazama maneno haya, ndivyo nilivyopata ugumu kupatanisha dhana ya Utatu na ile ambayo ilionekana kwangu kuwa ya kweli katika Injili. Nilijikuta nikikabiliana uso kwa uso na maswali magumu sana.
Ni wapi katika Injili Yesu alitumia neno “Utatu”?
Ikiwa Yesu alikuwa Mungu, kama vile mafundisho ya Utatu yanadai, kwa nini alimwabudu Mungu?
NA - kama Yesu alikuwa Mungu, kwa nini aseme kitu kama kifuatacho?
“Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake.” (Marko 10:18)
Je, kuna uwezekano, kwa namna fulani, alisahau kwamba yeye mwenyewe alikuwa Mungu wakati aliposema haya?
(Maelezo ya kando -- Nilikuwa na mazungumzo na mwanamke fulani aliyenihakikishia kwamba kifungu hiki hakikuwa katika Injili, na alikataa kuamini kwamba kilikuwa pale mpaka nilipompa sura na namba ya mstari na akaiangalia mwenyewe!)
Qur'ani Takatifu
Mnamo mwezi wa Novemba mwaka wa 2002, nilianza kusoma tafsiri ya Qurani.
Sijawahi kusoma tafsiri ya Kiingereza ya maandishi yote ya Qurani kabla ya hapo. Nilisoma tu muhtasari wa Qurani ulioandikwa na wasio Waislamu. (Na ulikuwa muhtasari wa kupotosha sana.)
Maneno hayaelezei kwa kutosha athari ya ajabu ambayo kitabu hiki kilikuwa nayo kwangu mimi. Inatosha kusema kwamba mvuto ule ambao ulinivuta kwa Injili katika umri wa miaka kumi na moja ulikuwepo kwa namna mpya na yenye maana kubwa sana. Kitabu hiki kilikuwa kinaniambia, kama vile nilivyoweza kujua kuwa Yesu alikuwa akiniambia, kuhusu mambo yaliyo muhimu kabisa.
Mwongozo Imara
Qurani ilikuwa ikitoa mwongozo imara na majibu halisi kwa maswali niliyokuwa nikiyauliza kwa miaka mingi kuhusu Injili.
“Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma. Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa ni miungu. Je, atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?” (Kurani 3:79-80)
Qurani ilinivuta kwa ujumbe wake kwa sababu ilithibitisha vizuri maneno ya Yesu ambayo nilihisi moyoni mwangu yalikuwa ya kweli. Kuna kitu kilibadilishwa katika Injili, na kitu hicho, nilijua katika moyo wangu, kilikuwa kimesalia kama kilivyokuwa awali katika maandishi ya Qurani.
Usambamba wa Kushangaza
Chini utapata mifano michache tu ya ulinganifu uliofanya moyo wangu uelekee kwa ibada ya Mungu. Kila mstari wa Injili unakuja na maandishi yaliyojengwa upya yanayojulikana kama matini ya-- Q ambayo wasomi wa leo wanaamini yanawakilisha tabaka la mwanzo kabisa la mafundisho ya Masihi. Angalia jinsi nyenzo hii ilivyo karibu na ujumbe wa Qurani.
Q Inakubaliana na Qur'ani juu ya Tawheed (Umoja wa Mungu)
Katika Q, Yesu anathibitisha, kwa maneno yasiyo na utata, umoja wa mungu.
“Nenda nyuma yangu, Ewe Shetani; maana imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako, na umwabudu yeye peke yake.” (Luka 4:8)
Linganisha:
“Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka"(Kurani 36:60-61)
Q Inakubaliana na Qur'ani Kuhusu Aqaba (Njia ya Kupanda Mlima)
Q inabainisha njia iliyo nyooka ambayo mara nyingi ni ngumu, njia ambayo makafiri watachagua kutofuata.
““Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba; kwa maana mlango mpana na njia rahisi huelekea kwenye maangamizo, na watu wanaopitia huko ni wengi. Lakini mlango mwembamba na njia ngumu huelekea kwenye uzima, na ni wachache tu wanaoiona.” (Mathayo 7:13 -14)
Linganisha:
“Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na wanawafanyia maskhara walio amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao Siku ya Kiyama...” (Kurani 2:212)
“Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani? Kumkomboa mtumwa. Au kumlisha siku ya njaa,Yatima aliye jamaa, Au masikini aliye vumbini. Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana.” (Kurani 90:12-17)
Q Inakubaliana na Qur'ani Kuhusu Taqwa (Kumcha Mwenyezi Mungu)
Q anatuonya tuogope tu hukumu ya Mungu.
“Nawambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, na halafu basi. Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kumwua mtu ana mamlaka ya kumtupa motoni. Naam: huyo, mwogopeni!” (Luka 12:4 -5)
Linganisha:
“Na ni vyake Yeye viliomo katika mbingu na ardhi. Na Dini ni yake Yeye daima. Je! Mtamcha mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu?” (Kurani 16:52)
Q Inakubaliana na Qur'ani Kuhusu Mitego ya Dunya (Maisha ya Dunia)
Katika Q, Yesu anawaonya wanadamu waziwazi kwamba faida za kidunia na raha hazipaswi kuwa lengo la maisha yetu:
“Lakini ole wenu ninyi matajiri, kwa sababu mmekwisha pata furaha yenu! Ole wenu ninyi mlioshiba, maana mtaona njaa! 25 Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, maana mtalia na kuomboleza.” (Luka 6:24)
Linganisha:
“Kumekushughulisheni kutafuta wingi, Mpaka mje makaburini! . Sivyo hivyo! Mtakuja jua! Tena sivyo hivyo! Mtakuja jua! Sivyo hivyo! Lau mngeli jua kwa ujuzi wa yakini, Basi bila ya shaka mtaiona Jahannamu! Tena, bila ya shaka, mtaiona kwa jicho la yakini. Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.” (Kurani 102:1-8)
Q Inawaonya Watu Wasidhani Wana Uhakika Wataingia Mbinguni!
Fikiria pia maneno yafuatayo kutoka kwa Masihi, ambayo yanapaswa (!) yaufanye kila moyo uwe mnyenyekevu, yaondoe kila aina ya kiburi katika masuala ya kiroho, na yanyamazishe kila shambulio lolote juu ya muumini mwingine:
“Ninawahakikishia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi nao wataketi mezani pamoja na Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa mbinguni. Lakini wanaoamini ufalme wa mbinguni ni wao, watatupwa nje gizani, huko watu watalia na kusaga meno.” (Matayo 8:11 -12)
Ni wazi kwamba, haya ni mafundisho muhimu kwa watu wote wenye nia nzuri wazingatie... na kuyakumbuka daima.
Q Haisemi Chochote Kuhusu Kusulubiwa au Dhabihu!
Umeona jinsi aya za awali kabisa katika historia --aya za Q --yanaenda sambamba na mafundisho makuu ya Qur'ani. Pia ni muhimu kutaja ukweli kwamba Q haifundishi chochote kuhusu kusulubiwa kwa Yesu, au asili ya kidhabihu ya utume wa Yesu... na kuondolewa kwa hayo ni jambo la kusisimua kweli!
Tunabaki basi na Injili ya awali kabisa -- Injili ambayo wasomi (wasio Waislamu) wanaamini ni karibu sana na Yesu kihistoria -- Injili ambayo ina sifa zifuatazo:
Ukubaliano na ujumbe wa Qur'ani usio na kigeugeu kuhusu umoja wa Mungu.
Ukubaliano na ujumbe wa Qurani kuhusu maisha ya baadaye ya wokovu au maangamizi kwenye moto... kulingana na matendo yetu duniani.
Ukubaliano na onyo la Qur'ani dhidi ya kupotoshwa na duniya -- vishawishi na raha za maisha ya kidunia.
Na...
UKOSEFU kamili wa kumbukumbu yoyote kuhusu kifo cha Yesu msalabani, ufufuo, au dhabihu kwa ajili ya wanadamu!
Hii ndiyo Injili ambayo wasomi wakubwa wa leo wasio Waislamu wametubainishia... na Injili hii inatuelekeza, iwapo tu tutasikiliza, kwa mwelekeo sawa na Qurani!
Ndugu na dada zangu wapendwa wa Kikristo, nawasihi kuomba kwa sala, kutafuta mwongozo wa Mungu juu ya swali hili: Je, hii inaweza kuwa tukio la kibahati tu?
Tangaza Neno!
Niliingia Uislamu tarehe 20 Machi, 2003. Ilikuwa dhahiri kwangu kwamba nilipaswa kushiriki ujumbe huu na Wakristo wengi iwezekanavyo wenye kufikiria.
Ongeza maoni