Manufaa ya Kusilimu (sehemu ya 1 kati ya 3)
Maelezo: Maswali yako yote yamejibiwa.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 27 Apr 2022
- Ilichapishwa: 2
- Imetazamwa: 9,170
- Imekadiriwa na: 77
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Makala nyingi katika wavuti huu zinafafanua jinsi ilivyo rahisi kwa mtu kusilimu. Kadhalika, kuna makala na video zinazojadili vizuizi vinavyoweza kusababisha mtu kutoukubali Uislamu. Waliosilimu kihakika husimulia hadithi zao, na tunaweza kuelezea na kusambaza furaha zao na misisimko yao. Hata kuna makala inayoelezea jinsi ya kuwa Muislamu. Kujiunga na Uislamu kumeshughulikiwa katika sehemu mbalimbali na msururu wa makala hii unajadili manufaa yanayotokana na kusilimu.
Kuna manufaa mengi yanayopatikana mtu anaposilimu, iliyowazi zaidi ni hali ya utulivu na uzima anayoipata mtu yeyote baada ya kugundua ukweli wa kimsingi wa maisha. Kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu katika njia halisi na rahisi hukuacha huru na kukusisimua, na matokeo yake huwa ni utulivu wa moyo. Hata hivyo, haya siyo manufaa ya pekee ya kusilimu, kuna manufaa mengine ambayo mtu huweza kuyapata na tutayajadili hapa, moja moja.
1.Kusilimu humkomboa mtu kutoka utumwa, mifumo ya kiubinadamu pamoja na mitindo ya kimaisha.
Uislamu huikomboa akili kutoka kwa ushirikina na mambo yasiyo na uhakika; huikomboa nafsi kutoka kwa dhambi na ufisadi na huiweka huru dhamira kutoka kwa uonevu na woga. Kujisalimisha kwa Mungu, hakuzuii uhuru, bali, huleta uhuru mwingi sana kwa kuikomboa akili kutoka ushirikina na kuijaza ukweli pamoja na elimu.
Pindi tu mtu anapoukubali Uislamu, hujinasua kutoka utumwa wa fasheni, ama ulaji, na hujikomboa kutoka utumwa wa mfumo wa kifedha unaolenga kuwadhalilisha watu. Katika kiwango kidogo lakini kilicho na umuhimu mkubwa, Uislamu humuweka mtu huru kutokana na ushirikina unaoyatawala maisha ya wale ambao hawajajisalimisha kwa Mwenyezi Mungu. Muumini hujua kwamba hakuna bahati nzuri na mbaya. Vipengele vyote vya uzuri na ubaya wa maisha yetu hutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofafanua Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie yeye, kuwa mambo yote ya muumini ni mazuri, "Anapofanyiwa wepesi, hushukuru, na hali hii ni nzuri kwake. Na anapozongwa na ugumu wa maisha, huvumilia, na hali hii ni nzuri kwake".[1]
Baada ya mtu kukombolewa kutoka mifumo ya kiubinadamu na mitindo ya kimaisha, huwa huru kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa njia inayofaa. Muumini huweza kumwamini Mungu na kuwa na matarajio mazuri kwa Mungu na hutafuta kwa dhati Rehema zake.
2.Kusilimu humpa mtu nafasi kuyapata mapenzi ya dhati ya Mwenyezi Mungu.
Mtu huyapata mapenzi ya Mungu anapojiunga na Uislamu kwa kufuata mwongozo wa Allah katika maisha yake - ambao ni Kurani, na mafundisho sahihi na mwenendo wa Mtume Muhammad. Wakati Mungu alipoumba ulimwengu, hakuuacha ulimwengu uyumbe na kukosa ulinzi kamili. Alituma kamba (hablu au dini), thabiti na imara, na kwa kushikilia kamba hiyo vyema, binadamu asiyethaminiwa anaweza kufikia daraja la ukuu na kupata amani ya kudumu. Katika maneno ya Kurani, Mwenyezi Mungu anayaweka waziwazi matakwa yake, hata hivyo, wanadamu wana hiari ya kumfurahisha au kumkasirisha Mwenyezi Mungu.
Sema (Ewe Muhammad): "Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu." (Kurani 3:31)
Na anayetafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri (kupata hasara). (Kurani 3:85)
Hapana kulazimisha katika dini. Kwani Uongofu umekwishapambanuka na upotofu. Basi anayemkataa Taghut[2] na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. (Kurani 2:256)
3.Manufaa ya kujiunga na Uislamu ni kwamba Mwenyezi Mungu anamuahidi Pepo aliyeamini.
Pepo, kama ilivyoelezewa kwenye aya nyingi za Kurani, ni sehemu ya furaha ya kudumu na imeahidiwa kwa waumini. Mwenyezi Mungu anaonyesha rehema yake kwa waumini kwa kuwazawidi Pepo. Yeyote yule anayemkana Mwenyezi Mungu ama kuabudu kitu kingine, au badala ya Allah, ama kudai kwamba Mwenyezi Mungu ana mtoto wa kiume ama wa kike au mshirika, ataangamia Akhera ndani ya Jehanamu. Kusilimu kutamwokoa mtu na adhabu ya kaburi, mateso ya Siku ya Hukumu na Jehanamu ya milele.
"Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni neema ya malipo ya watendao." (Kurani 29:58)
4.Furaha, utulivu na amani ya dhati huweza kupatikana kwa kujiunga na Uislamu.
Uislamu pekee unahusishwa moja kwa moja na amani ya dhati na utulivu. Maneno Uislamu, Muislamu na salaam (amani) yote hutokana na shina la neno "Sa - la – ma" yakimaanisha amani, ulinzi na usalama. Mtu anaponyenyekea kwa Mungu atapata usalama na amani.
Furaha halisi hupatikana Peponi pekee. Huko, tutapata amani kamili, utulivu na ulinzi na kuwa huru na woga, wasiwasi na maumivu, hali ambazo ni sehemu ya maisha ya binadamu. Hata hivyo, mwongozo uliotolewa na Uislamu unaturuhusu, sisi wanadamu wenye mapungufu, kutafuta furaha katika ulimwengu huu. Njia bora ya kuwa na furaha katika ulimwengu huu na kesho Akhera ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, na kumuabudu, bila ya kumshirikisha na chochote.
Katika makala ifuatayo tutaendelea na majadiliano yetu kuhusu manufaa ya kusilimu kwa kutaja msamaha na huruma, pamoja na majaribio na masaibu.
Rejeleo la maelezo:
[1] Saheeh Muslim
[2] Taghut – Ni neno la Kiarabu lenye maana nyingi. Kimsingi, ni kitu chochote kinachoabudiwa bila ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu mmoja wa Kweli, wakiwemo shetani, mapepo, masanamu, mawe, nyota, jua, mwezi, malaika, wanadamu, makaburi ya mawalii au watakatifu, watawala na viongozi.
Manufaa ya Kusilimu (sehemu ya 2 kati ya 3)
Maelezo: Sababu muhimu za kusilimu bila ya kuchelewa.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,485
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Watu wengi ulimwenguni huchukua muda mwingi sana kusoma na kujifunza kuhusu kanuni za Uislamu; hutafiti na kuzipitia tafsiri nyingi za Kurani na kuvutiwa na maisha na nyakati za Mtume Muhammad. Wengine huhitaji tu kujua kwa uchache kuhusu Uislamu na kusilimu mara moja. Ilhali wengine hutambua ukweli lakini hungoja, na kungoja na kuendelea kungoja, wakati mwingine kuhatarisha akhera yao. Tunaendelea na majadiliano yetu kuhusu manufaa, yasiyo wazi wakati mwingine, ya kujiunga na Uislamu.
"Na anakayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri [kupata hasara]." (Kurani 3:85)
5. Kusilimu ni hatua ya kwanza ya kuimarisha uhusiano wa kudumu na Muumba.
Kila mtu katika jamii ya wanadamu huzaliwa akijua kimaumbile kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Mtume Muhammad alisema kwamba kila mtoto huzaliwa katika hali ya fitra[1], huku akiwa na uelewa sahihi wa Mwenyezi Mungu.[2] Kulingana na Uislamu hii ndio hali ya asili ya mwanadamu, akiwa na silika ya kujua kwamba kuna Muumba, na kimaumbile akitaka kumuabudu na kumridhisha Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, wale wasiomjua Mungu ama wasioimarisha uhusiano na Mungu wanaweza kutatanishwa na uwepo wa mwanadamu na wakati mwingine kufadhaishwa. Kwa wale wengi, ambao humruhusu Mwenyezi Mungu kwenye maisha yao na kumuabudu Yeye kwa njia inayomridhisha, huleta maana mpya kabisa kwa maisha.
"...Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua." (Kurani 13:28)
Kupitia matendo ya ibada kama vile sala na dua, mtu huanza kuhisi ukaribu wa Mwenyezi Mungu, kupitia kwa elimu na hekima yake isiyo na kikomo. Muumini huwa salama kwa kuelewa kwamba Mwenyezi Mungu, aliye Mkuu wa Vyote, yuko juu ya mbingu, na kufarijika na uhakika kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja nao katika mambo yao yote. Muislamu kamwe hayuko peke yake.
"...Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote mnayoyatenda." (Kurani 57:4)
6. Kusilimu hudhihirisha rehema za Mungu na msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake.
Kama wanadamu wanyonge aghlabu tunajihisi tumepotea na tukiwa peke yetu. Kisha tunarudi kwa Mwenyezi Mungu na kuomba Huruma na Msamaha Wake. Tunaporudi kwa Mwenyezi Mungu tukijisalimisha kwake kwa dhati ya mioyo yetu, utulivu wa Mungu hutushukia. Kisha tunaweza kuhisi ubora wa huruma Yake na kuiona huruma hiyo ikidhihirika ulimwenguni. Hata hivyo, ili kumuabudu Mwenyezi Mungu, tunapaswa kumfahamu. Kwa kusilimu, milango ya kumfahamu Mungu hufunguka, ikiwemo ukweli kwamba Msamaha wa Mwenyezi Mungu hauna mipaka.
Watu wengi huchanganyikiwa ama kuaibishwa na madhambi mengi waliyotenda katika kipindi cha maisha yao. Kujiunga na Uislamu hufuta kabisa madhambi yote hayo; yakawa kana kwamba hayakuwahi kufanyika kabisa. Muislamu mgeni huwa safi kama mtoto mchanga aliyezaliwa.
"Waambie wale waliokufuru [kwamba] wakikoma, watasamehewa yaliyokwishapita. Lakini wakiyarudia, basi imekwishapita mifano ya [waasi] wa zamani." (Kurani 8:38)
Ikiwa baada ya kujiunga na Uislamu mtu atatenda madhambi zaidi, mlango wa msamaha bado huwa wazi kabisa.
"Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni madhambi [maovu] yenu, na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati [chini] yake..." (Kurani 66:8)
7. Kujiunga na Uislamu hutufunza kwamba majaribio na mitihani ni sehemu ya hali ya maisha ya mwanadamu.
Pindi mtu anapojiunga na Uislamu huanza kuelewa kwamba majaribio, masaibu, na ushindi katika maisha haya sio matukio nasibu ya ulimwengu katili usio na mpangilio. Muumini wa kweli huelewa kwamba uwepo wetu ni sehemu tu ya ulimwengu uliopangika vyema, na maisha huendelea kwa namna aliyoipanga Mwenyezi Mungu, kwa hekima Yake isiyo na kikomo.
Mwenyezi Mungu anatuambia kwamba tutafanyiwa majaribio, na Allah anatushauri kuyavumilia majaribio na masaibu hayo. Hili sio rahisi kulielewa mpaka mtu anapokubali kuwa kuna Mungu mmoja, dini ya Uislamu, ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia miongozo dhahiri kuhusu jinsi tunavyopaswa kufanya tutakapokabiliwa na majaribio na masaibu. Tukiifuata miongozo hii, iliyomo kwenye Kurani na mwenendo sahihi wa Mtume Muhammad, basi itawezekana kuyavumilia madhila kwa urahisi na hata kuwa mwenye shukurani.
"Hapana shaka Tutakujaribuni kwa chembe ya hofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri." (Kurani 2:155)
Mtume Muhammad alisema, “Mtu atapimwa kulingana na kiwango cha kujitolea kwake katika dini, na majaribio yataendelea kumuathiri muumini mpaka atakapoachwa akitembea duniani bila dhambi yoyote kabisa".[3]Muislamu anafahamu kwa hakika kwamba dunia hii, maisha haya, ni mapito ya muda mfupi tu, ni kituo katika safari ya maisha yetu ya milele ima kwenye Jehanamu ama Peponi. Kwa kukutana na Muumba bila ya mzigo wowote wa dhambi, hilo ni jambo zuri sana, bila shaka linaloambatana na ushindi wa majaribio yanayotufika.
Katika makala ifuatayo, tutakamilisha majadiliano haya kwa kutaja kwamba Uislamu ni njia ya maisha. Uislamu hufafanua wazi haki, wajibu na majukumu tuliyonayo kwa wanadamu wengine, na matunzo yetu kwa wanyama na mazingira. Uislamu una majibu ya maswali yote makubwa na madogo ya maisha yetu.
Manufaa ya Kusilimu (sehemu ya 3 kati ya 3)
Maelezo: Tunaendelea na majadiliano yetu kuhusu manufaa ya kusilimu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,555
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Manufaa ya kusilimu hayahesabiki, hata hivyo tumechagua machache yaliyobora zaidi ukiyalinganisha na mengine.
8. Kusilimu kunajibu maswali yote MAZITO ya maisha.
Mojawapo ya manufaa makubwa ya kusilimu ni kwamba hukuondolea ukungu wa kufahamu mambo. Ghafla maisha, na hekaheka zake zote, yanaeleweka kwa urahisi zaidi. Majibu ya maswali mazito yaliyokuwa yakimsumbua mwanadamu kwa maelfu ya miaka yamewekwa wazi sasa. Muda wowote katika maisha yetu, tutakapofika kwenye maporomoko au ukingoni, ama kwenye njia panda, hujiuliza – “Ni haya tu; kweli kuna mengine?” Hapana, haya sio yaliyopo pekee. Uislamu huyajibu maswali na kutuomba tusizingatie sana mali ya hapa duniani bali tuyatazame maisha haya kuwa ni kituo cha mapito katika safari ya maisha ya milele. Uislamu hutoa malengo na madhumuni bayana ya maisha. Kama Muislamu tunaweza kupata majibu katika maneno matakatifu ya Mwenyezi Mungu, kupitia Kurani, na katika kiigizo cha Mtume wa Mwisho Muhammad, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake.
Kuwa Muislamu kunadhihirisha unyenyekevu kamili kwa Muumba na ukweli kwamba tuliumbwa ili kumuabudu Mwenyezi Mungu Pekee. Hiyo ndiyo sababu iliyotuleta hapa, katika sayari hii inayozunguka kwenye ulimwengu usio na mwisho; kumuabudu Mwenyezi Mungu Pekee. Bila shaka, kusilimu kunatuokoa na dhambi isiyosameheka, ambayo ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote.
"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi [Pekee]."(Kurani 51:56)
"...Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye." (Kurani 7:59)
Hata hivyo, ni lazima isemwe kwamba, Mwenyezi Mungu hahitaji ibada ya mwanadamu. Ingekuwa hakuna mwanadamu hata mmoja anamuabudu Mwenyezi Mungu, isingepunguza utukufu Wake kwa namna yoyote ile, na ikiwa wanadamu wote wangemuabudu Yeye, isingezidisha utukufu Wake kwa namna yoyote ile.[1] Sisi, wanadamu ndio tunahitaji faraja na ulinzi kupitia kumuabudu Mwenyezi Mungu.
9. Kusilimu kunasababisha kila kipengele cha maisha kuwa tendo la ibada.
Dini ya Uislamu iliteremshwa kwa manufaa ya wanadamu wote watakaokuwepo hadi Siku ya Hukumu. Ni njia kamili ya maisha, sio inayofanywa wikendi ama katika sherehe za kila mwaka. Uhusiano wa muumini na Mwenyezi Mungu huwa muda wa saa ishirini na nne kwa siku, siku saba kwa wiki. Haimaliziki haianziki. Kupitia kwa huruma Yake isiyo na kikomo, Mwenyezi Mungu ametupatia mtazamo wa jumla wa maisha; ambao unashughulikia vipengele vyote, vya kiroho, kihisia na kimwili. Hajatuacha peke yetu kupotea gizani lakini Mwenyezi Mungu ametupatia Kurani, kitabu cha mwongozo. Kadhalika, mwenendo sahihi wa Mtume Muhammad ambao unaelezea na kufafanua mwongozo wa Kurani.
Uislamu hutosheleza na kuyasawazisha mahitaji yetu ya kimwili na kiroho. Mfumo huu, uliyoundwa na Muumba kwa viumbe wake, hautarajii tu kiwango cha juu cha tabia, uadilifu na maadili bali pia huruhusu kila tendo la mwanadamu kubadilishwa na kuwa ibada. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anawaamrisha waumini wajitolee maisha yao kwa ajili Yake.
“Sema: ‘Hakika sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.’” (Kurani 6:162)
10. Kusilimu husawazisha kila aina ya uhusiano.
Mwenyezi Mungu anajua kile kinachofaa kwa viumbe Wake. Mwenyezi Mungu ana elimu kamili ya akili ya mwanadamu. Kwa hivyo, Uislamu unafafanua kwa uwazi haki na wajibu tulionao kwa Mwenyezi Mungu, wazazi wetu, mume na mke, watoto, jamaa, majirani, n.k. Hatua hii huleta nidhamu badala ya vurugu, maelewano badala ya mtafaruku na amani mahali pa migongano na migogoro. Kujiunga na Uislamu huruhusu mtu kukabiliana na hali zozote kwa ujasiri. Uislamu unaweza kutuongoza katika hali zote za maisha, za kiroho, kisiasa, kifamilia, kijamii na kishirika.
Tunapotimiza wajibu wetu wa kumtukuza na kumtii Mwenyezi Mungu, moja kwa moja tunakuwa na adabu na viwango vya juu vya uadilifu unaohitajika katika Uislamu. Kujiunga na Uislamu kunamaanisha kujisalimisha na matakwa ya Mungu na hatua hii inahusisha kutukuza na kuheshimu haki za wanadamu wote, viumbe vyote vinavyoishi na hata mazingira. Tunapaswa kumjua Mungu na kujisalimisha Kwake ili kufanya maamuzi yatakayotupatia radhi Yake.
Kwa kuhitimisha, kuna faida moja ya kusilimu inayoifanya kila siku kuwa yenye furaha. Haijalishi ni hali gani ambayo kila Muislamu anajipata kwayo, wapo salama wakifahamu kwamba hakuna lolote katika ulimwengu huu litakalotokea bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu. Mitihani, majaribio na ushindi yote hayo ni mambo mazuri na yanapokabiliwa na imani ya Mwenyezi Mungu, yatakuwa ni sababu ya mwisho mwema na kutosheka kwa dhati. Mtume Muhammad alisema, “Hakika mambo ya muumini hushangaza! Yote ni kwa manufaa yake. Ikiwa atapewa wepesi basi hushukuru, na vivyo hivyo hilo ni jambo zuri kwake. Na anapokumbwa na dhiki, huvumilia, na vivyo hivyo ni jambo zuri kwake".[2]
Ongeza maoni