Safari ya Kuelekea Akhera (sehemu ya 3 kati ya 8): Muumini wakati wa Siku ya Hukumu
Maelezo: Jinsi waumini watakuwa Siku ya Hesabu, na baadhi ya sifa za waumini zitakazowarahisishia kupita kwenye milango ya Peponi.
- Na Imam Mufti (co-author Abdurrahman Mahdi)
- Iliyochapishwa mnamo 12 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,248 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Siku ya Hukumu
"Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, na mamaye na babaye, na mkewe na wanawe. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha." (Kurani 80:34-37)
Saa ya Ufufuo itakuwa tukio la kutisha na kubwa. Hata hivyo, pamoja na dhiki zake, Muumini atakuwa na furaha, kama Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alivyosimuliwa kutoka kwa Mola wake Mlezi:
Mwenyezi Mungu anasema, "Kwa Ezi Yangu na Jalali Yangu (Utukufu Wangu), Sitampa mja Wangu dhamana mbili na vitisho viwili. Akijihisi salama kutoka Kwangu akiwa duniani[1], nitamtia hofu Siku nitakapowakusanya waja Wangu; na akiniogopa akiwa duniani, nitamweka salama Siku nitakapowakusanya waja Wangu."[2]
"Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika. Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu. Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa." (Kurani 10:62-64)
Wakati wanadamu wote waliowahi kuumbwa watakusanywa kusimama uchi na bila kutahiriwa kwenye tambarare pana chini ya joto kali linalochoma la Jua, kundi la wanaume na wanawake wachaji Mungu litawekwa chini ya kivuli cha Kiti cha Enzi cha Mungu. Mtume Muhammad alibashiri nafsi hizo zilizobahatika kuwa ni za akina nani, Siku ambayo hakutakuwa na kivuli kingine:[3]
·mtawala mwadilifu ambaye hakutumia vibaya mamlaka yake, bali alipitisha haki iliyofunuliwa na Mungu miongoni mwa watu
·kijana ambaye alikua akimuabudu Mola wake Mlezi na akadhibiti matamanio yake ili aendelee kuwa safi
·wale ambao nyoyo zao zilishikamana na Misikiti, wakitamani kurejea humo kila walipotoka
·wale waliopendana kwa ajili ya Mungu
·wale waliojaribiwa na wanawake warembo wenye kuvutia, lakini hofu yao ya Mungu iliwazuia wasitende dhambi
·yule aliyetoa sadaka kwa moyo halisi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kuzificha sadaka zao
·yule ambaye alilia kwa hofu ya Mungu akiwa peke yake
Matendo mahususi ya ibada pia yatawaweka watu salama siku hiyo, yaani:
·jitihada za ulimwengu huu za kuwaondolea taabu wanaotaabika, kuwasaidia maskini, na kupuuza makosa ya wengine, zitawaondolea watu dhiki katika Siku ya Hukumu[4]
·huruma iliyoonyeshwa kwa wadaiwa (kwa kuwasamehe na kufuta madeni yao)[5]
·waadilifu ambao wanawatendea haki familia zao na kufanya uadilifu katika mambo waliyopewa kama amana wasimamie[6]
·kudhibiti hasira[7]
·mwenye hutoa wito kwa sala[8]
·kuzeeka mtu akiwa katika hali au ndani ya Uislamu[9]
·kutia udhu wa kiibada (kutawadha) mara kwa mara na ipasavyo[10]
·wale wanaopigana pamoja na Isa bin Maryam dhidi ya Dajjali na jeshi lake[11]
·kifo cha kishahidi
Mwenyezi Mungu atamleta muumini karibu naye, atamhifadhi, atamfunika (atamsitiri), na atamuuliza kuhusu madhambi yake. Baada ya kuyakubali madhambi yake, ataamini kuwa ameangamia, lakini Mwenyezi Mungu atasema:
"Nilikufichia duniani, na nakusamehe Siku hii ya leo."
Atakemewa kwa mapungufu yake,[12] lakini atakabidhiwa kitabu chake cha matendo mema kwa mkono wake wa kulia.[13]
"Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wa kulia! Basi huyo atahesabiwa hesabu nyepesi!" (Kurani 84:7-8)
Kwa furaha akitazama rekodi yake, atatangaza furaha yake:
"Basi ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: ‘Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hesabu yangu.’ Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza – katika Bustani ya juu, matunda yake yakaribu. [Waambiwe]: ‘Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyotanguliza katika siku zilizopita.’" (Kurani 69:19-24)
Kisha rekodi ya matendo mema itapimwa, kihalisi, ili kubainisha kama inapita rekodi ya matendo mabaya ya mtu, na ili thawabu au adhabu itolewe ipasavyo.
"Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hesabu." (Kurani 21:47)
"Basi anayetenda chembe ya wema, atauona!" (Kurani 99:7)
"Jambo zito zaidi litakalowekwa katika Mizani ya mtu Siku ya Kiyama [baada ya ushahidi wa Imani] ni tabia njema, na Mwenyezi Mungu anamchukia mtu mpujufu (mchafu kutokana na mdomo wake au maneno) na mtu fasiki au asiye mwadilifu (mchafu kutokana na vitendo vyake)." (Al-Tirmidhi)
Waumini hao watakata kiu yao kutoka kwenye hifadhi maalumu (Raudhwa) iliyowekwa kwa ajili ya Mtume Muhammad. Yeyote atakayekunywa humo hataona kiu tena. Uzuri wake, ukubwa wake, na ladha tamu nzuri, imeelezwa kwa kina na Mtume.
Waumini wa Uislamu - wakosefu miongoni mwao na wachaji Mungu - pamoja na wanafiki wataachwa katika bonde kubwa baada ya makafiri kufukuzwa na kukimbizwa Motoni. Daraja refu linalopita juu Motoni na kugubikwa na giza litawatenganisha na Pepo.[14]Waamini watapata nguvu na faraja katika kuvuka kwao kwa haraka juu ya moto unaonguruma wa Jehanamu na kupitia ‘nuru’ ambayo Mungu ataiweka mbele yao, ikiwaongoza kwenye makao yao ya milele:
"Siku utakapowaona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru yao iko mbele yao, na kuliani kwao: ‘Furaha yenu leo - Bustani zipitazo mito kati [chini] yake, mtakaa humo milele.’ Huko ndiko kufuzu kukubwa." (Kurani 57:12)
Hatimaye, baada ya kuvuka daraja, waumini watatakaswa kabla ya kuingia Peponi. Vifundo vyote kati ya waumini vitasuluhishwa ili kwamba hakuna mwanamume anayeweka kinyongo dhidi ya mwingine.[15]
Rejeleo la maelezo:
[1] Kwa maana kwamba haogopi adhabu ya Mungu na hivyo kufanya dhambi.
[2]Silsila Al-Saheehah.
[3]Saheeh Al-Bukhari.
[4]Saheeh Al-Bukhari.
[5]Mishkat.
[6]Saheeh Muslim.
[7]Musnad.
[8]Saheeh Muslim.
[9]Jami al-Sagheer.
[10]Saheeh Al-Bukhari.
[11]Ibn Majah.
[12]Mishkat.
[13]Saheeh Al-Bukhari. Ishara ya kuwa wao ni katika watu wa Peponi, kinyume na wale watakaopewa daftari lao la matendo yao kwa mikono yao ya kushoto au nyuma ya migongo yao.
[14] Saheeh Muslim.
[15]Saheeh Al-Bukhari
Ongeza maoni