Kwa nini Mungu aliumba wanadamu? (sehemu ya 1 kati ya 4): Ibada ya Mungu
Maelezo: Kusudi la uumbaji wa wanadamu ni ibada. Sehemu ya 1: Haja ya binadamu ya ibada.
- Na Dr. Bilal Philips
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 8,410 (wastani wa kila siku: 8)
- Imekadiriwa na: 128
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Kutokana na mtazamo wa wanadamu, swali la “Kwa nini Mungu aliumba mwanadamu?” linamaanisha “Kwa sababu gani mwanadamu aliumbwa?” Katika ufunuo wa mwisho (Qur'ani) swali hili linajibiwa bila ya utata wowote. Kwanza wanadamu wanaambiwa na Mungu kwamba kila mwanadamu anazaliwa na ufahamu wa kiasili wa Mungu. Katika qurani Mungu anasema:
"Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?" (Qurani 7:172)
Nabii, rehma na baraka za Mungu ziwe juu yake, alieleza kwamba Mungu alipomuumba Adamu, alichukua kutoka kwake agano katika mahali paitwapo Na'maan siku ya 9 ya mwezi wa 12. Kisha akawaondoa kutoka kwa Adamu wazao wake wote ambao wangezaliwa mpaka mwisho wa dunia, kizazi baada ya kizazi, na kuwatandaza mbele yake ili kuchukua agano kutoka kwao pia. Akawaambia uso kwa uso, akiwashuhudisha kwamba yeye ndiye Mola wao Mlezi. Kwa hivyo, kila mwanadamu anawajibika kuwa na imani katika Mungu, ambayo imechapishwa kwa kila nafsi. Ni kutokana na imani hii ya kuzaliwa nao ndio Mungu alifafanua kusudi la uumbaji wa wanadamu katika Qur'ani:
"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." (Qurani 51:56)
Hivyo basi, lengo muhimu ambalo wanadamu waliumbiwa ni ibada ya Mungu. Hata hivyo, Mwenyezi hana haja na ibada ya wanadamu. Hakumuumba binadamu kutokana na haja kwa upande Wake. Kama hakungekuwa na mwanadamu hata mmoja wa kumwabudu Mungu, haingepunguza utukufu Wake kwa njia yoyote, na kama wanadamu wote wangemwabudu, haingeongeza kwa utukufu Wake kwa njia yoyote. Na Mwenyezi Mungu ni mkamilifu. Yeye peke yake yupo bila mahitaji yoyote. Viumbe vyote vilivyoumbwa vina mahitaji. Kwa hivyo, ni mwanadamu anayehitaji kumwabudu Mungu.
Maana ya Ibada
Ili kuelewa ni kwa nini binadamu wanahitaji kumwabudu Mungu, ni lazima mtu aelewe kwanza maana ya neno 'ibada.' Neno la Kiingereza la 'ibada' limetoka kwa neno la Kingereza cha Kale (weorthscipe) linalomaanisha 'heshima.' Kwa hivyo, ibada katika lugha ya Kiingereza hufafanuliwa kama 'utendaji wa vitendo vya ibada kama heshima kwa Mungu.' Kwa maana hii, mwanadamu anaagizwa kuonyesha shukrani kwa Mungu kwa kumtukuza. Katika Qurani, Mungu anasema:
"Mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi..." (Kurani 15:98)
Katika kumtukuza Mungu, mwanadamu anachagua kuwa sawa na viumbe vyote ambavyo kwa kawaida humtukuza Muumba. Mungu anazungumzia jambo hili katika sura nyingi za Qurani. Kwa mfano, katika Qurani, Mungu anasema:
"Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake." (Qurani 17:44)
Hata hivyo, kwa Kiarabu, ambayo ni lugha ya ufunuo wa mwisho, ibada inaitwa 'ibaadah, ambalo linahusiana kwa karibu na nomino 'abd, inayomaanisha 'mtumwa. ' Mtumwa ni yule anayetarajiwa kufanya chochote anachotaka bwana Wake. Kwa hivyo, ibada, kulingana na ufunuo wa mwisho, inamaanisha “ utiifu kwa Mungu.” Hii ilikuwa kiini cha ujumbe wa manabii wote waliotumwa na Mungu kwa wanadamu. Kwa mfano, ufahamu huu wa ibada ulionyeshwa kinagaubaga na Nabii Yesu (Masihi au Yesu Kristo),
“Si kila mtu anayesema, ‘Bwana, Bwana,’ ambaye ataingia katika Ufalme wa mbinguni ila ni wale wanaofanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”
Ikumbukwe kwamba 'mapenzi' katika nukuu hii inamaanisha 'kile Mungu anataka mwanadamu kufanya' na si 'kile ambacho Mungu anaruhusu wanadamu kufanya, 'kwa sababu hakuna kinachotokea katika uumbaji bila ya majaliwa (idhini) ya Mungu. “Mapenzi ya Mungu' yamepatikana katika sheria zilizofunuliwa na Mungu ambazo manabii waliwafundisha wafuasi wao. Kwa hivyo, utii wa sheria ya Mungu ni msingi wa ibada. Kwa maana hiyo utukufu unakuwa pia ibada wakati binadamu wanapochagua kutii maagizo ya Mungu kuhusu utukufu Wake.
Haja ya kuabudu
Kwa nini binadamu wanahitaji kumwabudu na kumtukuza Mungu kwa kutii sheria zilizofunuliwa na Mungu? Kwa sababu utii wa sheria ya Mungu ni ufunguo wa kufanikiwa katika maisha haya na ya pili. Wanadamu wa kwanza, Adamu na Hawa, waliumbwa katika paradiso na baadaye kufukuzwa kutoka huko kwa kuasi sheria tukufu. Njia pekee ya binadamu kurudi peponi ni kwa utiifu wa sheria. Nabii Yesu, aliripotiwa katika Injili kulingana ya Matayo kuwa amesema utii wa sheria za Mungu ndio ufunguo wa paradiso.
“Mwalimu mwema, nifanye jambo jema gani ili nipate uzima wa milele?” Basi akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Hapana aliye mwema ila ni mmoja tu, Mwenyezi Mungu. Lakini mkitaka kuingia katika uzima, shika amri.”
Pia Nabii Yesu aliripotiwa kuwa amesisitiza juu ya utii mkali wa amri, akisema:
“Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika Ufalme wa mbiguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika Ufalme wa mbinguni.”
Sheria za Kimungu zinawakilisha mwongozo kwa wanadamu katika nyanja zote za maisha. Zinawafafanulia sahihi na batili na kuwapa wanadamu mfumo kamili unaoongoza mambo yao yote. Muumba peke yake anajua zaidi yaliyo na manufaa kwa uumbaji Wake na yasiyokuwa na manufaa. Sheria za kimungu zinaamuru na kuzuia vitendo na vitu mbalimbali ili kulinda roho ya binadamu, mwili wa binadamu na jamii ya binadamu kutokana na madhara. Ili binadamu waweze kutimiza uwezo wao kwa kuishi maisha ya uchamungu, wanahitaji kumwabudu Mungu kwa njia ya utiifu wa amri Zake.
Ongeza maoni