Utabiri wa Muhammad katika Bibilia (sehemu 4 ya 4): Utabiri Zaidi Katika Agano Jipya
Maelezo: Ushahidi wa Bibilia kuwa Muhammad si Mtume wa uongo. Sehemu ya 4: Uchambuzi wa ziada kuhusu utabiri uliotajwa katika Yohana 14:16 wa Paraklete, au 'Msaidizi' na jinsi Muhammad anaafikiana na utabiri huu zaidi ya wengine.
- Na Imam Mufti
- Iliyochapishwa mnamo 23 Nov 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 2
- Imetazamwa: 46,147 (wastani wa kila siku: 41)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
5. Yesu anaeleza jukumu la Yule Parakletos Mwingine:
Yohana 16:13 "Atawaongoza muijue kweli yote."
Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani kuhusu Muhammad:
"Enyi Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki itokayo kwa Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo kheri yenu.!..." (Kurani 4:170)
Yohana 16:14 "Atanitukuza mimi."
Kurani aliyokuja nayo Muhammad inamtukuza Yesu:
"…Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).." (Kurani 3:45)
Muhammad pia alimtukuza Yesu:
"Yeyote atakaye shuhudia ya kwamba hakuna anayestahili kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, ambaye hana mshiriki, na kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake, na Isa ni mja wa Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na neno lake alilo mpea Maryamu, na roho iliyotoka kwake, na kuwa Pepo ni kweli, na Jahannamu ni kweli, Mwenyezi Mungu atamkaribisha kwa Pepo kulingana na yale aliyo yatenda.." (Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim)
Yohana 16:8 "Naye akija atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, na haki na hukumu ."
Kurani inaeleza:
"Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru. !’" (Kurani 5:72)
Yohana 16:13 "Yeye hatanena kwa uwezo wake mwenyewe, bali atanena yote atakayosikia."
Kurani inasema kuhusu Muhammad:
"Wala hatamki kwa matamanio.Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa." (Kurani 53:3-4)
Yohana 14:26 "atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha yote."
Maneno ya Kurani:
"…Na hali Masihi mwenyewe alisema, ‘Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi.’" (Kurani 5:72)
…yanawakumbusha watu amri kuu na ya kwanza ya Yesu, ambayo wameisahau:
"Ya kwanza ndiyo hii: ‘Sikiliza Israeli! Bwana Mungu wetu, ndiye peke yake Bwana.’" (Marko 12:29)
Yohana 16:13 "atawafundisha kuhusu mambo yote yajayo."
Kurani inasema:
"Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia, [Ewe Muhammad]…" (Kurani 12:102)
Hudhaifa, mwanafunzi wa Mtume Muhammad, anatuambia:
"Mtume, rehma ziwe juu yake, aliwahi kusimama kati yetu na kutoa hotuba, ambapo hakuacha chochote bali alituambya yote yatakayotokea hadi siku ya kiama ." (Saheeh Al-Bukhari)
Yohana 14:16 "akae nanyi siku zote."
…maana yake ni kuwa mafundisho yake ya awali yatabaki milele. Muhammad alikuwa nabii wa mwisho wa Mungu kwa wanadamu. [1] Mafundisho yake yamehifadhiwa kikamilifu. Anaishi ndani ya mioyo na akili za wafuasi wake wanaomwabudu Mungu kwa kumuiga Muhammad kisawasawa. Hakuna mtu, ikiwa ni pamoja na Yesu au Muhammad, anayeishi milele duniani. Na Parakletos si kesi ya kipekee pia. Hili haliwezi kuwa linamzungumzia Roho Mtakatifu, kwani imani ya kisasa ya Roho Mtakatifu haikuwepo kabla ya Baraza la Kalsedoni , mnamo 451 BK, karne nne na nusu baada ya Yesu.
Yohana 14:17 "huyo ndiye roho wa kweli"
…maana atakuwa nabii wa kweli, tazama 1 Yohana 4: 1-3.
Yohana 14:17 "ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni..."
Watu wengi duniani leo hawamjui Muhammad.
Yohana 14:17 "...wala haumtambui"
Wachache zaidi ndio wanaomtambua Muhammad wa kweli, Mtume wa Rehema wa Mungu.
Yohana 14:26 "yule Msaidizi (parakletos)"
Muhammad ndiye atakuwa mtetezi wa wanadamu kwa ujumla na Waumini wenye madhambi siku ya kiama:
Watu watawatafuta wanaoweza kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba yao ili kupunguza dhiki na mateso Siku ya Kiyama. Adamu, Nuhu, Ibrahimu, Musa na Yesu watajitoa na kupeana udhuru zao.
Kisha watakuja kwa Nabii wetu, naye atasema: 'Hakika mimi ndiye mwenye uwezo'. Kisha atawaombea watu katika uwanja mkubwa ambapo watu wamekusanyika, hukumu itolewe. Hiki ndicho 'Cheo kilicho sifika ' ambacho Mungu anamuahidi katika Qur'an:
"…Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika (heshima ya kuwa mwombezi siku ya kiyama)" (Kurani 17:79)[2]
Mtume Muhammad alisema:
"Maombezi yangu yatakuwa kwa wale wa taifa langu waliotenda dhambi kuu." (Al-Tirmidhi)
"Mimi nitakuwa mwombezi wa kwanza katika Peponi.." (Saheeh Muslim)
Baadhi ya wasomi wa Kiislamu wanaonyesha kuwa kile ambacho Yesu alisema kwa Kiaramu kinawakilisha kwa karibu zaidi neno la Kigiriki periklytos ambalo linamaanisha 'anayependwa.' Kwa Kiarabu neno 'Muhammad' linamaanisha 'anayesifiwa, anayeheshimiwa. ' Kwa maana nyingine, periklytos ni “Muhammad” kwa Kigiriki. Tuna sababu mbili kuu za kuunga mkono jambo hili. Kwanza, kutokana na matukio kadhaa yaliyorekodiwa ya kubadilisha maneno yanayofanana katika Bibilia, inawezekana kwamba maneno yote mawili yalikuwa katika maandishi ya awali lakini yaliwachwa na mwandishi kwa sababu ya desturi ya kale ya kuandika maneno yakikaribiana, bila nafasi katikati. Katika hali kama hiyo maandishi ya awali yangekuwa, “na atawapa msaidizi mwingine (parakletos), anayependwa (periklytos).” Pili, tuna ushuhuda wa kuaminika wa angalau wasomi wanne wa Kiislamu kutoka kwa vipindi tofauti ambao waliwahesabia wasomi wa Wakristo kuwa 'wa kusifiwa' ndio maana inayowezekana ya neno la Kigiriki au la Kisyriak .[3]
Wafuatao ni kati ya wale walioshuhudia kwamba Paraklete inamrejelea Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:
Shahidi wa Kwanza
Anselm Turmeda (1352/55-1425 BK), kuhani na msomi wa Kikristo, alikuwa shahidi wa utabiri huu. Baada ya kukubali Uislamu aliandika kitabu, "Tuhfat al-arib fi al-radd ‘ala Ahl al-Salib."
Shahidi wa Pili
Abdul-Ahad Dawud, ambaye ni Mchungaji wa zamani David Abdu Benjamin Keldani, BD, padri Mkatoliki wa madhehebu ya Umoja wa Wakaldayo. [4] Baada ya kukubali Uislamu, aliandika kitabu, 'Muhammad katika Biblia. ' Anaandika yafuatayo katika kitabu chake:
“Hakuna shaka hata kidogo kwamba neno “Periqlyte,” inamlenga Nabii Muhammad, yaani Ahmad."
Shahidi wa Tatu
Muhtasari wa maisha ya Muhammad Asad tayari imetolewa hapo juu. Akitoa maoni yake kuhusu mstari huo:
"…Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad" (Kurani 61:6)
…ambapo Yesu anatabiri kuja kwa Muhammad, Asad anaelezea kuwa neno Parakletos:
"…bila shaka ni Periklytos ('anayesifiwa kwa wingi'), iliyo badilishwa, na ni tafsiri halisi ya Kigiriki ya neno au jina la Kiaramu la Mawhamana. (Ikumbukwe kwamba Kiaramu ilikuwa lugha iliyotumiwa Palestina wakati wa Yesu, na kwa karne kadhaa baada yake, na hivyo bila shaka ilikuwa lugha ambayo maandiko ya kiasili -ambayo yamepotea kwa sasa - ya Injili yalitungwa.) Kwa mtazamo wa ukaribu wa kimatamshi kati ya Periklytos na Parakletos, ni rahisi kuelewa jinsi mfasiri - au, labda zaidi, mwandishi wa baadaye - aliyachanganya maneno haya mawili. Ni muhimu kwamba maneno ya Kiaramu Mawhamana na Periklytos ya Kigiriki yana maana sawa na ni majina mawili ya Mtume wa Mwisho, Muhammad na Ahmad, ambayo yote yametokana na kitenzi cha Kiebrania hamida ('alisifu') na nomino ya Kiebrania hamd ('sifu').”
Vielezi-chini:
[1] Kurani 33:40.
[2] Angalia pia Saheeh Al-Bukhari
[3]‘Sirat Rasul Allah,’ ya Ibn Ishaq (85-151 CE)uk, 103. ‘Bayn al-Islam wal-Masihiyya: Kitab ‘Abi Ubaida al-Khazraji ,’ uk. 220-221 ya Abu Ubaida al-Khazraji (1146-1187 CE) p. 220-221. ‘Hidaya tul-Hayara,’ ya Ibn ul-Qayyim, uk. 119. ‘al-Riyadh al-Aniqa,’ ya al-Suyuti, uk. 129.
[4] Soma wasifu wake hapa: (http://www.muhammad.net/biblelp/bio_keldani.html.)
Ongeza maoni