Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 1 kati ya 5): Waislamu wanampenda Yesu pia!
Maelezo: Yesu na muujiza wake wa kwanza, na muhtasari wa wanachoamini Waislamu kumhusu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 19 Dec 2024
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,060
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Wakristo mara nyingi huzungumza juu ya kukuza uhusiano na Kristo na kumkubali katika maisha yao. Wanadai kwamba Yesu ni zaidi ya mtu na alikufa msalabani ili kuwakomboa wanadamu kutoka kwa dhambi ya asili. Wakristo wanazungumza juu ya Yesu kwa upendo na heshima na ni wazi ana nafasi maalumu katika maisha yao namioyoni mwao. Lakini vipi kuhusu Waislamu; wanafikiria nini juu ya Yesu Kristo na anashikilia nafasi gani katika Uislamu?
Mtu asiyejua Uislamu anaweza kushangaa kujifunza kwamba Waislamu wanampenda Yesu pia. Muislamu hatazungumza jina la Yesu bila kuongeza kwa heshima maneno "amani iwe juu yake". Katika Uislamu, Yesu ni mtu anayependwa na kuthaminiwa, ni Mtume na Mjumbe anayelingania watu wake katika ibada ya Mungu Mmoja wa Kweli.
Waislamu na Wakristo wanashirikiana katika imani kadhaa zinazofanana juu ya Yesu. Wote wanaamini kuwa Yesu alizaliwa na Bikira Maria na wote wanaamini kwamba Yesu ndiye Masihi aliyetumwa kwa watu wa Israeli. Wote pia wanaamini kuwa Yesu atarudi duniani katika siku za mwisho. Walakini kwa jambo moja kuu wanatofautiana sana kama mbingu na ardhi. Waislamu wanaamini kwa yakini kwamba Yesu sio Mungu, yeye sio mwana wa Mungu na yeye sio sehemu ya Utatu wa Mungu.
Katika Kurani, Mungu anazungumzia moja kwa moja na Wakristo akisema:
“Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake. Wala msiseme: ‘Utatu.’ Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu Mmoja tu. ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.” (Kurani 4:171)
Kama vile Uislamu unavyokanusha kimsingi kwamba Yesu alikuwa Mungu, pia inakataa dhana kwamba mwanadamu huzaliwa akiwa ametiwa ila ya aina yoyote ya dhambi ya asili. Kurani inatuambia kuwa haiwezekani kwa mtu mmoja kubeba madhambi ya mwingine na kwamba sisi sote tunawajibika, mbele ya Mungu, kwa matendo yetu wenyewe. "Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine." (Kurani 35:18) Hata hivyo, Mungu, kwa Rehema Yake isiyo na mipaka na Hekima hajawatelekeza wanadamu wajifanyie mambo wanavyotaka. Ametuma mwongozo na sheria ambazo zinaonyesha jinsi ya kuabudu na kuishi kulingana na maamrisho Yake. Waislamu wanahitajika kuwaamini, na kuwapenda Mitume wote; kwani kumkataa mmoja ni kuikataa imani ya Uislamu. Yesu alikuwa mmoja tu miongoni mwa mfuatano mrefu ya Mitume na Wajumbe, akiwaita watu wake kumwabudu Mungu Mmoja. Alikuja hasa kwa Watu wa Israeli, ambao wakati huo walikuwa wamepotea kwa kutofuata njia iliyo wazi ya Mungu. Yesu alisema:
“Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlioharimishiwa, na nimekujieni na ishara kutokana na Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.” (Kurani 3:50-51)
Waislamu wanapenda na kumstahi Yesu. Hata hivyo, tunamuelewa yeye na jukumu lake katika maisha yetu kulingana na Kurani na masimulizi na maneno ya Mtume Muhammad. Sura tatu za Kurani zinaonyesha maisha ya Yesu, mama yake Maryamu na familia zao; kila sura ikitoa maelezo yasiyopatikana katika Biblia.
Mtume Muhammad alizungumzia kuhusu Yesu mara nyingi, na wakati mmoja akimsifu kama kaka yake.
“Mimi ndiye niliye karibu sana na mwana wa Maryamu kuliko watu wote, na mitume wote ni ndugu wa baba, na hakuna mtume alikuja baina yangu na yeye (yaani Isa).” (Saheeh Al-Bukhari)
Hebu tufuatilie kisa cha Yesu kupitia vyanzo vya Kiisilamu ili tuelewe ni vipi na kwa nini nafasi yake katika Uislamu ni muhimu.
Muujiza wa Kwanza
Kurani inatuarifu kwamba Maryamu, binti ya Imran, alikuwa msichana ambaye hajaolewa, safi na mcha Mungu aliyejitolea kumwabudu Mungu. Siku moja alipokuwa amejitenga, Malaika Jibril alifika kwa Maryamu na kumjulisha kwamba atakuwa mama wa Yesu. Jibu lake lilikuwa la woga, mshtuko, na kufadhaika. Mungu alisema:
“...Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lililokwisha hukumiwa.” (Kurani 19:21)
Maryamu alibeba mimba ya Yesu, na wakati ulipofika wa kuzaliwa kwake, alijiondoa kutoka kwa familia yake na kusafiri kuelekea Bethlehemu. Chini ya mtende, Maryamu alimzaa mtoto wake ambaye ni Yesu.[1]
Maryamu alipokuwa anapumzika na kupona kutokana na maumivu na woga uliohusika na kujifungua peke yake, ilimjia fahamu kuwa lazima arudi kwa familia yake. Maryamu aliogopa na kuwa na wasiwasi alipomfunika mtoto huyo na kumkumbatia mikononi mwake. Angewezaje kuelezea kuzaliwa kwake kwa watu wake? Alisikiliza maneno ya Mungu na akarudi Jerusalemu.
“...Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: ‘Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.’ Akaenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba...” (Kurani 19:26-27)
Mungu alijua kwamba Maryamu angejaribu kutoa maelezo, watu wake hawangemwamini. Kwa hivyo, kwa hekima Yake, alimwambia asiongee. Kuanzia muda Maryamu aliwakaribia watu wake, walianza kumtuhumu, lakini alifuata maagizo ya Mungu kwa busara na kukataa kujibu. Mwanamke huyu mwenye haya, asiyezini, alimwashiria mtoto mikononi mwake.
Wanaume kwa wanawake waliomzunguka Maryamu walimtazama bila kuamini na walidai kujua wangeweza vipi kuzungumza na mtoto mchanga aliyebebwa mikononi. Basi, kwa idhini ya Mungu, Yesu, mwana wa Maryamu, bado angali mtoto mchanga, alifanya muujiza wake wa kwanza. Aliongea:
“...Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu na amenifanya Mtume; na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu niko hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.” (Kurani 19:30-34)
Waislamu wanaamini Yesu alikuwa mtumwa wa Mungu na Mjumbe aliyetumwa kwa Waisraeli wa wakati wake. Alifanya miujiza kwa matakwa na ruhusa ya Mungu. Maneno yafuatayo ya Mtume Muhammad yanaelezea wazi umuhimu wa Yesu katika Uislamu:
“Mwenye kushuhudia ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hana mshirika wala msaidizi, na kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake, na kwamba Isa ni mja Wake na Mtume Wake, ambaye ni neno ambalo Mwenyezi Mungu alimpa Maryamu na ni roho iliyoumbwa Naye. na kwamba Pepo ni kweli, na Jehanamu ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atamuingiza katika milango minane ya Mbinguni anayotaka.” (Saheeh Bukhari and Saheeh Muslim)
Rejeleo la maelezo:
[1] Kwa maelezo ya muujiza wa kupata mimba na kuzaliwa kwake, tafadhali rejelea makala ya Maryamu
Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 2 kati ya 5): Ujumbe wa Yesu
Maelezo: Hali halisi ya Yesu na ujumbe wake katika Kurani, na umuhimu wa Bibilia leo kuhusiana na imani za Waislamu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,722
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Tumeshathibitisha ya kwamba Yesu mwana wa Maryamu, au kama anavyoitwa na Waislamu, Isa ibn Maryam, alifanya muujiza wake wa kwanza akiwa amebebwa mikononi mwa Maryamu. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu alisema, na maneno yake ya kwanza yalikuwa “Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu,” (Kurani 19:30). Hakusema “Mimi ni Mungu” au hata “Mimi ni mwana wa Mungu”. Maneno yake ya kwanza yaliweka msingi wa ujumbe wake, na utume wake ulikuwa: kuwaita watu warudi, kwenye ibada halisi ya Mungu Mmoja.
Wakati wa Yesu, dhana ya Mungu Mmoja haikuwa jipya kwa Wana wa Israeli. Taurati ilikuwa imetangaza “Sikia, Ee Israeli, Bwana Mungu wako ndiye Mmoja,” (Kumbukumbu la Torati 6:4). Hata hivyo, mafunuo ya Mungu ilitafsiriwa vibaya na kutumiwa vibaya, na nyoyo zikawa ngumu. Yesu alikuja kuwakana hadharani viongozi wa Wana wa Israili, ambao walijiingiza katika maisha ya kupenda mali na anasa, na kuitetea sheria ya Musa iliyopatikana ndani ya Taurati ambayo hata wao waliibadilisha.
Utume wa Yesu ulikuwa ni kuithibitisha Taurati, kuhalalisha mambo ambayo hapo awali yalikuwa haramu na kutangaza na kuthibitisha tena imani katika Muumba Mmoja. Mtume Muhammad amesema:
“Kila Mtume alitumwa kwa umma wake peke yake, lakini mimi nilitumwa kwa watu wote,” (Saheeh Bukhari).
Kwa hivyo, Yesu alitumwa kwa Waisraeli.
Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani kwamba atamfundisha Yesu Taurati, Injili na Hekima.
“Na atamfunza kuandika na Hekima na Taurati na Injili.” (Kurani 3:48)
Ili kueneza ujumbe wake kwa ufanisi, Yesu aliielewa Taurati, na alipewa ufunuo wake mwenyewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu - nayo ni Injili. Pia, Mungu alijaalia Yesu uwezo wa kuwaongoza na kuwashawishi watu wake kupitia ishara na miujiza.
Mwenyezi Mungu huwapa nguvu Mitume Wake wote kupitia miujiza inayoonekana na yenye maana kwa watu ambao Mtume huyo alitumwa kuwaongoza. Wakati wa Yesu, Waisraeli walikuwa na ujuzi mwingi katika uwanja wa tiba. Kwa hiyo, miujiza aliyoifanya Yesu (kwa idhini ya Mungu) ilikuwa ya namna hii na ilijumuisha kurudisha kuona kwa vipofu, kuponya wenye ukoma na kufufua wafu. Mungu anasema:
“...na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini Yangu; na ulipowafufua wafu kwa idhini Yangu...” (Kurani 5:110)
Mtoto Yesu
Si Kurani wala Biblia inayorejelea ujana wa Isa. Tunaweza kukisia, hata hivyo, kwamba kama mtoto wa kiume katika familia ya Imran, yeye alikuwa mtoto mcha Mungu aliyejitolea kujifunza na mwenye shauku ya kuwashawishi watoto na watu wazima waliomzunguka. Baada ya kumtaja Yesu akizungumza angali mtoto mchanga wa kubebwa, Kurani mara moja inasimulia kisa cha Yesu akifinyanga umbo la ndege kutoka kwenye udongo. Akapuliza ndani yake na kwa idhini ya Mungu ukawa ndege.
“...nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu...” (Kurani 3:49)
Injili ya Utotoni ya Thomas, mojawapo ya seti ya maandishi yaliyoandikwa na Wakristo wa mwanzo lakini haikukubaliwa kuingizwa katika kanuni au mafundisho ya Agano la Kale, pia inarejelea hadithi hii. Inasimulia kwa undani hadithi ya Yesu angali mdogo akitengeneza ndege kutoka kwa udongo na kupuliza uhai ndani yao. Ingawa inavutia, Waislamu wanaamini ujumbe wa Yesu iwapo tu unasimuliwa katika Kurani na simulizi za Mtume Muhammad.
Waislamu wanatakiwa kuamini vitabu vyote vilivyoteremshwa na Mungu kwa wanadamu. Walakini, Biblia, kama ilivyo leo, sio Injili ambayo ilifunuliwa kwa Mtume Yesu. Maneno na hekima ya Mungu aliyopewa Yesu yamepotea, yamefichwa, yamebadilishwa na kupotoshwa. Hatima ya maandishi ya Apokrifa (Yasiyothibitishwa au Yaliyobuniwa) ambayo Injili ya Utotoni ya Thomas ni ushuhuda wa hili. Mnamo 325BK, Mfalme Konstantino alijaribu kuunganisha Kanisa la Kikristo lililovunjika kwa kuitisha mkutano wa Maaskofu kutoka kote ulimwenguni kunapojulikana. Mkutano huu ulijulikana kama Baraza la Naisia, na waliwakifia fundisho la imani ya Utatu, ambalo hapo awali halikuwepo, na kuchangia kupotea kati ya injili 270 na 4000. Baraza hilo liliamuru kuchomwa moto injili zote ambazo hazikustahiki kuingizwa katika Biblia mpya, na Injili ya Utotoni ya Thomas ilikuwa ni mojawapo yazo.[1] Hata hivyo, nakala za Injili nyingi zilisalimika, na, ingawa hazimo katika Biblia, zinathaminiwa kwa umuhimu wao wa kihistoria.
Kurani Inatukomboa
Waislamu wanaamini kwamba Yesu kwa hakika alipokea ufunuo kutoka kwa Mungu, lakini hakuandika neno hata moja, wala hakuwaagiza wanafunzi wake kuliandika.[2] Hakuna haja ya Muislamu kujaribu kuthibitisha au kukanusha vitabu vya Wakristo. Kurani hutuondolea haja ya kujua kama Biblia tuliyo nayo leo ina neno la Mungu, au maneno ya Yesu. Mungu anasema:
“Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili.” (Kurani 3:3)
Na pia:
“Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu...” (Kurani 5:48)
Chochote chenye manufaa kwa Waislamu kukijua kutoka katika Taurati au Injili kimeelezwa kwa uwazi ndani ya Kurani. Jema lolote ambalo linaweza kupatikana katika vitabu vilivyotangulia linapatikana sasa ndani ya Kurani.[3] Ikiwa maneno ya Agano Jipya ya leo yanakubaliana na maneno ya Kurani, basi maneno haya huenda yanaunda sehemu ya ujumbe wa Yesu ambao haukupotoshwa au kupotea kwa kupita muda. Ujumbe wa Yesu ulikuwa ni ujumbe uleule ambao Mitume wote wa Mungu walifundisha watu wao. Mola wenu Mlezi, Mungu wenu, ni Mmoja, basi muabuduni Yeye peke yake. Na Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani kuhusu kisa cha Yesu:
“Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hekima.” (Kurani 3:62)
Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 3 kati ya 5): Wanafunzi wake
Maelezo: Muujiza mwingine wa Yesu unaelezwa. Umuhimu halisi wa muujiza wa meza, kuenea kwa vyakula.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,607
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Sura ya 5 ya Kurani inaitwa Al Maidah (au Meza Iliyoandaliwa Chakula). Ni moja ya sura tatu katika Kurani zinazozungumzia kwa mapana maisha ya Yesu na mama yake Maryamu. Sura nyingine ni sura ya 3 Al Imran (familia ya Imran) na sura ya 19, Maryam (Maryamu). Waislamu wanampenda Yesu, na wanamheshimu Mama yake, lakini hawawaabudu. Kurani, ambayo Waislamu wanaamini kuwa ni maneno ya moja kwa moja ya Mwenyezi Mungu, inawaheshimu sana Yesu na Mama yake Maryamu, na kwa hakika familia yao yote - familia ya Imran.
Tunajua kwamba Yesu aliishi miongoni mwa watu wake Waisraeli kwa miaka mingi, akiwaita warudi kwenye ibada ya Mungu Mmoja wa Kweli, pamoja na kufanya miujiza kwa idhini ya Mungu. Wengi wa wale waliokuwa karibu naye walikataa wito wake na kushindwa kutii ujumbe wake. Hata hivyo, Yesu alikusanya karibu naye kundi la masahaba walioitwa Al Hawariyeen (wanafunzi wa Isa) kwa Kiarabu.
Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“Na nilipowafunulia Al-Hawariyeen (Wanafunzi) kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: ‘Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.’” (Kurani 5:111)
Wanafunzi walijiita Waislamu; hii ingewezekanaje wakati dini ya Uislamu isingefunuliwa kwa miaka 600 mingine? Mungu lazima anarejelea maana ya jumla ya “Muislamu”. Muislamu ni mtu yeyote anayejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu Mmoja na utiifu Wake, na yeyote ambaye utiifu wake na uaminifu wake ni kwa Mwenyezi Mungu na Waumini kuliko kitu kingine chochote. Maneno Muislamu na Uislamu yanatokana na mzizi mmoja wa Kiarabu - sa la ma - na hiyo ni kwa sababu amani na usalama (Salam) asili yake ni kunyenyekea kwa Mungu. Kwa hivyo inaweza kueleweka kwamba Mitume wote wa Mungu na wafuasi wao walikuwa Waislamu.
Meza Iliyoandaliwa Chakula
Wanafunzi wa Yesu wakamwambia:
“Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?” (Kurani 5:112)
Je, walikuwa wakimwomba Yesu afanye muujiza? Je, wanafunzi wa Yesu waliojiita Waislamu walihisi kutokuwa na hakika kuhusu uwezo wa Mungu wa kufanya miujiza apendavyo? Haiwezekani, kwani hiki kitakuwa ni kitendo cha kutoamini. Wanafunzi wa Yesu hawakuwa wakiuliza kama ingewezekana, bali iwapo Yesu angemwomba Mungu wakati huo mahususi awape chakula. Hata hivyo, huenda Yesu alifikiri tofauti, kwa kuwa alijibu:
“...Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.” (Kurani 5:112)
Walipoona jinsi Yesu alivyoitikia, wanafunzi wake walijaribu kueleza maneno yao. Hapo awali walisema: "Tunataka kukila chakula hicho kutoka kwenye (hiyo meza)."
Huenda walikuwa na njaa sana na walitaka Mungu atimize mahitaji yao. Kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie riziki kunakubalika, kwani Mwenyezi Mungu ndiye mpaji, Ambaye riziki zote hutoka kwake. Wanafunzi wakaendelea kusema, “na nyoyo zetu zitue (ziridhike).”
Walimaanisha kwamba imani yao ingeimarika zaidi iwapo wangeona muujiza kwa macho yao wenyewe, na hilo linathibitishwa na kauli yao ya mwisho. "Na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia (ni mashahidi wa kuteremshwa hiyo meza iliyojaa vyakula)."
Ijapokuwa ilitajwa mwisho, kuwa shahidi wa kweli ilivyo na kuona miujiza ambayo ni uthibitisho muhimu zaidi wa ombi lao. Wanafunzi walikuwa wakimuomba Mtume Yesu afanye muujiza huo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ili wawe mashahidi mbele ya wanadamu wote. Wanafunzi hao walitaka kueneza ujumbe wa Yesu kwa kutangaza miujiza waliyoshuhudia kwa macho yao wenyewe.
“Wakasema: ‘Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.’ Akasema Isa mwana wa Maryamu: ‘Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku.’” (Kurani 5:113-114)
Yesu aliomba muujiza huo. Alisali kwa Mungu, akiomba kwamba meza iliyokuwa na vyakula iteremshwe. Yesu pia aliomba kwamba hii iwe kwa ajili yao wote na kwamba iwe sikukuu. Neno la Kiarabu linalotumiwa na Kurani ni Idi, likimaanisha sherehe inayotokea au kurudi tena. Yesu alitaka wanafunzi wake na wale waliokuja baada yao wakumbuke baraka za Mungu na kushukuru.
Tuna mengi ya kujifunza kutokana na dua zilizoombwa na Mitume na waumini wengine wema. Dua ya Yesu haikuwa tu kwa ajili ya meza iliyotandazwa vyakula, bali kwa Mungu kuwapa riziki. Ameifanya dua hiyo kuwa jumuifu kwa sababu chakula ni sehemu ndogo tu ya riziki inayotolewa na Mbora wa Wanaoruzuku. Riziki kutoka kwa Mungu inajumuisha mahitaji yote muhimu kwa maisha yakiwemo, lakini sio tu, chakula, makao, na ujuzi. Mungu akajibu:
“...Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekana baadaye, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.” (Kurani 5:115)
Ujuzi ni Sawa na Uwajibikaji
Sababu kwa nini jibu la Mungu lilikuwa limetoa uamuzi wa mwisho ni kwamba ikiwa mtu atakufuru baada ya kuonyeshwa ishara au muujiza kutoka kwa Mungu, ni mbaya zaidi kuliko kukufuru bila kuona muujiza. Unaweza kujiuliza ni kwa nini. Ni kwa sababu pindi mtu anapoona muujiza, anakuwa na ujuzi na ufahamu wa kuwa Mungu ni muweza wa yote. Kadiri mtu anavyokuwa na ujuzi mwingi, ndivyo anavyokuwa na uwajibikaji zaidi mbele ya Mungu. Unapoziona ishara, wajibu wa kuamini na kueneza ujumbe wa Mungu unakuwa mkubwa zaidi. Mungu aliwaamuru wanafunzi wa Yesu watakapoikea meza hiyo iliyotandazwa vyakula waweze kutambua wajibu mkubwa ambao walikuwa wamejitwika wenyewe.
Siku ya meza ikawa siku ya karamu na sherehe kwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu, lakini, kadiri muda ulivyopita, maana halisi na kiini cha muujiza huo ilipotea. Hatimaye Yesu alikuja kuabudiwa kama mungu. Siku ya Ufufuo, wakati wanadamu wote watasimama mbele ya Mungu, wanafunzi wale watabeba daraka kubwa la kujua ujumbe wa kweli wa Yesu. Mungu atazungumza na Yesu moja kwa moja akisema:
“...Ewe Isa mwana wa Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu?’ (Na Isa) atasema: ‘Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyofichikana. Sikuwaambia lolote ila uliyoniamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi...’” (Kurani 5:116-117)
Sisi ambao tumebarikiwa na ujumbe huu wa kweli wa Yesu, ujumbe uleule ulioenezwa na Mitume wote akiwemo mtume wa mwisho, Muhammad, pia tutabeba jukumu kubwa Siku ya Kiyama.
Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 4 kati ya 5): Je, ni Kweli Yesu Alikufa?
Maelezo: Makala hii inaelezea imani ya Waislamu kuhusu Isa na kusulubiwa. Pia inakanusha dhana ya uhitaji wa ‘dhabihu’ ili kulipia dhambi ya asili kwa niaba ya wanadamu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,076
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Wazo la Yesu kufa msalabani ni msingi wa imani ya Kikristo. Inawakilisha kusadiki kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya madhambi ya wanadamu. Kusulubiwa kwa Yesu ni fundisho muhimu katika Ukristo; hata hivyo Waislamu wanaikataa kabisa. Kabla ya kueleza kile ambacho Waislamu wanaamini kuhusu kusulubiwa kwa Yesu, ni muhimu kuelewa hoja ya Kiislamu ya dhana ya dhambi ya asili.
Adam na Hawa walipokula tunda la mti waliokatazwa peponi, hawakushawishiwa na nyoka. Shetani ndiye aliyewahadaa na kuwarai, wakatumia hiari yao na kufanya uamuzi wa makosa. Hawa hakubeba mzigo wa kosa hili peke yake. Kwa pamoja, Adam na Hawa walitambua kuwa kutotii kwao, wakajuta na kumwomba Mungu awasamehe. Mungu, kwa huruma yake zisizo na kifani na hekima yake isiyo na kikomo, aliwasamehe. Uislamu hauna dhana ya dhambi ya asili; kila mtu atawajibika kwa matendo yake.
“Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine...” (Kurani 35:18)
Hakuna haja ya Mwenyezi Mungu, mwana wa Mungu, au hata Mtume wa Mwenyezi Mungu kujitoa muhanga kwa ajili ya madhambi ya wanadamu ili awasamahe. Uislamu unakataa katakata mtazamo huu. Msingi wa Uislamu umejikita katika kujua kwa yakini kwamba hakuna apasaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee. Msamaha unatoka kwa Mungu Mmoja wa Kweli; kwa hiyo, mtu anapoomba msamaha, ni lazima amgeukie Mungu kwa unyenyekevu na majuto ya kweli na kuomba msamaha, akiahidi kutorudia dhambi hilo. Hapo ndipo tu madhambi yatasamehewa.
Katika mwanga wa ufahamu wa Uislamu wa dhambi ya asili na msamaha, tunaweza kuona kwamba Uislamu unafundisha kwamba Yesu hakuja kufidia madhambi ya wanadamu; badala yake, lengo lake lilikuwa ni kuthibitisha ujumbe wa Mitume kabla yake.
“...Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu...” (Kurani 3:62)
Waislamu hawaamini kusulubiwa kwa Yesu, wala hawaamini kwamba alikufa.
Kusulubiwa
Ujumbe wa Yesu ulikataliwa na wengi wa Waisraeli na vilevile wenye mamlaka Waroma. Wale walioamini waliunda kikundi kidogo cha wafuasi karibu naye, kilichojulikana kama wanafunzi. Waisraeli walipanga njama dhidi ya Yesu na kupanga mpango wa kuuliwa. Alipaswa kuuawa hadharani, kwa namna ya kutisha sana, inayojulikana sana katika Milki ya Roma: kusulubiwa.
Kusulubiwa kulizingatiwa kuwa njia ya aibu ya kufa, na "raia" wa Milki ya Kirumi walipewa udhuru wa kutopata adhabu hii. Iliundwa sio tu kuongeza muda wa uchungu wa kifo, lakini kukeketa mwili. Waisraeli walipanga kifo hiki cha kufedhehesha kwa ajili ya Masihi wao - Yesu, mjumbe wa Mungu. Mungu kwa huruma yake isiyo na kikomo alizuia tukio hili la kuchukiza kwa kuweka mfanano wa Yesu kwa mtu mwingine na kumpaisha Yesu akiwa hai, mwili na roho, hadi mbinguni. Kurani iko kimya kuhusu maelezo kamili ya mtu huyu alikuwa nani, lakini tunajua na tunaamini kwa uhakika kwamba hakuwa Mtume Yesu.
Waislamu wanaamini kwamba Kurani na hadithi sahihi za Mtume Muhammad zina elimu zote zinazohitajika na mwanadamu ili kuabudu na kuishi kulingana na amri za Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, ikiwa maelezo mafupi hayajafafanuliwa, ni kwa sababu Mungu kwa hekima Yake isiyo na kikomo amehukumu maelezo hayo kuwa hayana faida kwetu. Kurani inaeleza, kwa maneno ya Mungu mwenyewe, njama dhidi ya Yesu na mpango Wake wa kuwashinda Waisraeli na kumwinua Yesu mbinguni.
“Na makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.” (Kurani 3:54)
“Na kwa kusema kwao: "Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu." Lakini hawakumuuwa wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi wowote nayo, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini.” (Kurani 4:157-158)
Isa Hakufa
Waisraeli na watawala wa Kirumi hawakuweza kumdhuru Yesu. Mungu anasema waziwazi kwamba alimchukua Yesu hadi kwake na kumwondolea taarifa za uongo zilizotolewa kwa jina la Yesu.
“...Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru...” (Kurani 3:55)
Katika aya iliyotangulia, Mungu aliposema “atampaisha” Yesu, anatumia neno mutawaffeeka. Bila ufahamu wa wazi wa utajiri wa lugha ya Kiarabu, na ujuzi wa viwango vya maana katika maneno mengi, kuna uwezekano wa kutoelewa alichomaananisha Mungu. Katika lugha ya Kiarabu leo, neno mutawaffeeka mara nyingine hutumiwa kuashiria kifo, au hata kulala. Katika aya hii ya Kurani, hata hivyo, maana ya asili imetumika na ufahamu wa neno hili unaashiria kwamba Mungu alimnyanyua Yesu kwake, kikamilifu. Kwa hivyo, alikuwa hai wakati wa kupaa kwake, mwili na roho, bila jeraha au kasoro yoyote.
Waislamu wanaamini kwamba Yesu hajafa, na kwamba atarudi katika ulimwengu huu katika siku za mwisho kabla ya Siku ya Hukumu. Mtume Muhammad aliwaambia masahaba zake:
“Mtakuwaje atakapoteremka Isa miongoni mwenu na atawahukumu watu kwa Sheria ya Kurani na sio kwa sheria ya Injili.” (Saheeh Al-Bukhari)
Mungu anatukumbusha katika Kurani kuwa Siku ya Kiyama ni siku ambayo hatuwezi kuikwepa na anatutahadharisha kuwa kushuka kwa Yesu ni dalili ya ukaribu wake.
“Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.” (Kurani 43:61)
Kwa hiyo, imani ya Kiislamu kuhusu kusulubiwa na kifo cha Yesu iko wazi. Kulikuwa na njama ya kumsulubisha Yesu lakini haikufanikiwa; Yesu hakufa, bali alipaa mbinguni. Katika siku za mwisho kuelekea Siku ya Hukumu, Yesu atarudi katika ulimwengu huu na kuendeleza ujumbe wake.
Yesu, mwana wa Maryamu (sehemu ya 5 kati ya 5): Watu wa Kitabu
Maelezo: Muhtasari wa baadhi ya istilahi zilizotumiwa na Kurani kwa ajili ya Isa na wafuasi wake kabla ya ujio wa Muhammad: "Bani Israeel”, “Eissa” na "Watu wa Kitabu".
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,273
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Baada ya kusoma na kuelewa kile Waislamu wanachoamini kuhusu Yesu, mwana wa Maryamu, kunaweza kuwa na maswali ambayo yanakuja akilini, au masuala ambayo yanahitaji ufafanuzi. Huenda umesoma neno “Watu wa Kitabu” na maana yake haikuwa wazi kabisa. Vivyo hivyo, unapochunguza vitabu vilivyopo kuhusu Yesu unaweza kukutana na jina Eissa na kujiuliza ikiwa Yesu na Eissa ni mtu mmoja. Ikiwa unafikiria kuchunguza zaidi kidogo au pengine kusoma Kurani, mambo yafuatayo yanaweza kukuvutia.
Isa ni nani?
Eissani Yesu. Labda kwa sababu ya tofauti ya matamshi, watu wengi wanaweza kuwa hawajui kwamba wanapomsikia Mwislamu akizungumza kuhusu Eissa, anazungumza juu ya Mtume Eissa. Tahajia ya Eissa inaweza kuwa ya aina nyingi – Isa, Esa, Essa, na Eissa. Lugha ya Kiarabu imeandikwa kwa herufi za Kiarabu, kwa hivyo mfumo wowote wa unukuzi hujaribu kutoa sauti ya kifonetiki. Haijalishi ni tahajia gani, zote zinaashiria Yesu, Mjumbe wa Mungu.
Yesu na watu wake walizungumza Kiaramu, lugha ya familia ya Wasemiti. Lugha za Kisemiti zinazozungumzwa na zaidi ya watu milioni 300 kote Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Pembe ya Afrika, ni pamoja na Kiarabu na Kiebrania. Matumizi ya neno Eissa ni tafsiri ya karibu zaidi ya neno la Kiaramu la Yesu – Eeshu. Kwa Kiebrania hii inatafsiriwa kwa Yeshua.
Kutafsiri jina Jesus (Yesu) katika lugha zisizo za Kisemiti kulizua utata. Hakukuwa na "J" katika lugha yoyote hadi karne ya kumi na nne[1], hivyo basi, jina Jesus lilipotafsiriwa katika Kigiriki, likawa Iesous, na katika Kilatini, Iesus[2]. Baadaye, herufi “I” na “J” zilitumiwa kwa kubadilishana, na hatimaye jina hilo likabadilishwa kuwa Kiingereza na kuwa Jesus. "S" ya mwisho kwenye mwisho ni kiashiria cha lugha ya Kigiriki ambapo majina yote ya kiume huishia kwa "S".
Kiaramu |
Kiarabu |
Kiebrania |
Kigiriki |
Kilatini |
Kiingereza |
Eeshu |
Eisa |
Yeshua |
Iesous |
Iesus |
Jesus |
Ni nani wenye vitabu vitukufu?
Mwenyezi Mungu anapowataja Watu wa Kitabu, anazungumzia zaidi kuhusu Mayahudi na Wakristo. Katika Kurani, watu wa Kiyahudi wanaitwa Bani Israeel, hasa Wana wa Israeli, au kwa kawaida Waisraeli. Makundi haya mahususi yanafuata, au yalifuata wahyi wa Mwenyezi Mungu kama ulivyoteremshwa katika Taurati na Injili. Unaweza pia kusikia Mayahudi na Wakristo wakiitwa "Watu wa Maandiko".
Waislamu wanaamini kwamba vitabu vilivyofunuliwa na Mwenyezi Mungu kabla ya Kurani vilipotea zamani, au vimebadilishwa na kupotoshwa, lakini pia wanatambua kwamba wafuasi wa kweli wa Musa na Yesu walikuwa Waislamu waliomwabudu Mungu Mmoja kwa utiifu wa kweli. Alikuja Yesu mwana wa Maryamu ili kusadikisha ujumbe wa Musa na kuwaongoza Wana wa Israili kwenye njia iliyonyooka. Waislamu wanaamini Mayahudi (Wana wa Israeli) walikataa utume na ujumbe wa Yesu, na Wakristo walimnyanyua kimakosa hadi hadhi ya mungu.
“Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya watu waliokwisha potea tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.” (Kurani 5:77)
Tumeshajadili katika sehemu zilizopita jinsi Kurani inavyohusika kwa mapana na Mtume Yesu na mama yake Maryamu. Hata hivyo, Kurani pia inajumuisha aya nyingi ambapo Mungu anazungumza moja kwa moja na Watu wa Kitabu, hasa wale wanaojiita Wakristo.
Wakristo na Mayahudi wanaambiwa wasiwachambue Waislamu bila sababu yoyote isipokuwa kuamini Mungu Mmoja, lakini Mungu pia anaelekeza kwa makini kwenye ukweli kwamba Wakristo (wale wanaofuata mafundisho ya Kristo) na Waislamu wana mambo mengi yanayofanana, pamoja na mapenzi yao na heshima kwa Yesu na Manabii wote.
“...Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanaosema: ‘Sisi ni Manasara.’ Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi. Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume, utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyoitambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia.” (Kurani 5:82-83)
Sawa na Yesu mwana wa Maryamu, Mtume Muhammad alikuja kuthibitisha ujumbe wa Mitume wote waliomtangulia; aliwaita watu kumwabudu Mungu Mmoja. Utume wake, hata hivyo, ulikuwa tofauti na Mitume waliotangulia, (Nuhu, Ibrahimu, Musa, Yesu na wengineo) kwa namna moja. Mtume Muhammad alikuja kwa ajili ya wanadamu wote na Mitume kabla yake walikuja mahususi kwa ajili ya wakati wao na watu wao. Kuja kwa Mtume Muhammad na kuteremshwa Kurani kulikamilisha dini iliyoteremshwa kwa Watu wa Kitabu.
Na Mwenyezi Mungu alizungumza na Mtume Muhammad katika Kurani na kumsihi kuwaita Watu wa Kitabu kwa kusema:
“Sema: ‘Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu...’” (Kurani 3:64)
Mtume Muhammad aliwaambia masahaba zake, na hivyo kwa wanadamu wote:
“Mimi ni mtu wa karibu zaidi na mwana wa Maryamu, na Mitume wote ni ndugu na hakuna mtume mwingine baina yangu na yeye.”
Isitoshe:
“Mtu akimwamini Isa na kisha kuniamini atapata thawabu maradufu.” (Saheeh Al-Bukhari)
Uislamu ni dini ya amani, heshima na uvumilivu, na inatekeleza uadilifu na huruma kwa dini nyingine, hasa kwa Watu wa Kitabu.
Ongeza maoni