Hadithi ya Adam (sehemu ya 2 kati ya 5): Uumbwaji wa Hawa na Jukumu la Shetani
Maelezo: Uumbwaji wa mwanamke wa kwanza, makao tulivu ya Peponi na mwanzo wa uadui baina ya Shetani na wanadamu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 4
- Imetazamwa: 8,789 (wastani wa kila siku: 8)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Adam alifumbua macho yake na kutazama uso mzuri wa mwanamke ukimtazama. Adam alishangaa na kumuuliza yule mwanamke lengo la kuumbwa kwake ni lipi. Alidhihirisha kwamba alipaswa kumpunguzia upweke na kumpa utulivu. Malaika walimuhoji Adam. Walijua kuwa Adam alikuwa na ujuzi wa mambo wasiyofahamu na elimu ambayo wanadamu wangehitaji ili kuitumia duniani. Wakasema ‘huyu ni nani?’ Adam akajibu ‘huyu ni Hawa’.
Hawa ni Hawwa kwa Kiarabu; linatokana na asili ya neno hay, linalomaanisha kuishi. Hawa pia ni lahaja ya Kiingereza ya neno la zamani la Kiebrania Havva, ambalo pia linatokana na hai. Adam aliwajulisha Malaika kwamba Hawa aliitwa hivyo kwa sababu aliumbwa kutoka na sehemu yake na yeye, Adam, alikuwa kiumbe hai.
Tamaduni za Kiyahudi na za Kikristo zinasisitiza kuwa Hawa aliumbwa kutoka kwa ubavu wa Adam, ingawa katika tafsiri halisi ya tamaduni ya Kiyahudi, wakati mwingine mbavu hujulikana kama upande.
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi..’” (Kurani 4:1)
Tamaduni za Mtume Muhammad zinasimulia kuwa Hawa aliumbwa wakati Adam alipokuwa amelala kutoka kwenye mbavu yake fupi ya upande wa kushoto na kwamba, baada ya muda fulani, alivikwa nyama. Yeye (Mtume Muhammad) alitumia kisa cha uumbwaji wa Hawa kutoka kwenye mbavu ya Adam kama msingi wa kuwasihi watu wawe wapole na wema kwa wanawake. Enyi Waislamu! Ninawashauri muwe wapole kwa wanawake, kwani wameumbwa kutokana na mbavu, na sehemu iliyopinda zaidi ya mbavu ni sehemu ya upande wa juu. Ukijaribu kuinyoosha, itavunjika, na ukiacha, itabaki ikiwa imepinda; kwa hivyo nawasihi muwatunze wanawake."(Saheeh Al-Bukhari)
Makazi ya Peponi
Adam na Hawa waliishi kwenye mazingira tulivu huko Peponi. Kadhalika, hii inakubaliwa na tamaduni za Kiislamu, Kikristo na Kiyahudi. Uislamu unatuambia kwamba Pepo yote ilikuwa raha mustarehe na Mwenyezi Mungu akamwambia Adam, “na kuleni humo popote mpendapo kwa starehe ....” (Kurani 2:35) Kurani haielezi eneo halisi la mahali Pepo hii ilikuwa; hata hivyo, wafasiri wanakubali kwamba haiko duniani, na kwamba ufahamu wa eneo hilo hauna manufaa yoyote kwa wanadamu. Faida ni katika kuzingatia soma kutokana na matukio yaliyofanyika hapo.
Mwenyezi Mungu aliendelea na maagizo yake kwa Adam na Hawa kwa kuwaonya “...lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu” (Kurani 2:35) Kurani haifafanui ulikuwa ni mti wa aina gani; hatuna maelezo ya kutosha na kadhalika kutafuta elimu kama hiyo hakuna manufaa yoyote. Kinachofahamika ni kwamba Adam na Hawa waliishi maisha tulivu na walielewa kwamba walikatazwa kula matunda ya mti huo. Hata hivyo, Shetani alikuwa akingojea kuwapotosha kupitia udhaifu wa wanadamu.
Shetani ni nani?
Shetani ni kiumbe kutoka kwa ulimwengu wa Majini. Majini ni viumbe vya Mwenyezi Mungu vilivyotengenezwa kwa moto. Wako kivyao na tofauti na Malaika na wanadamu; hata hivyo, kama wanadamu, wana uwezo wa kufikiri na wanaweza kuchagua kati ya mema na mabaya. Majini walikuwepo kabla ya kuumbwa kwa Adam[1] na Shetani ndiye aliyekuwa mwadilifu zaidi miongoni mwao, kiasi kwamba alipandishwa cheo cha hadhi ya juu miongoni mwa Malaika.
“Basi Malaika wote pamoja walimsujudia. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura.’ (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo..’” (Kurani 15:30-35)
Jukumu la Shetani
Shetani alikuwepo katika Pepo ya Adam na Hawa na ahadi yake ilikuwa ni kuwapotosha na kuwahadaa wao na vizazi vyao. Shetani alisema: “…Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao.…” (Kurani 7:16-17) Shetani ni mwenye kiburi, na alijiona mbora zaidi kuliko Adam, na vile vile wanadamu. Yeye ni mjanja na mwenye hila, lakini mwishowe anaelewa udhaifu wa wanadamu; anautambua upendo na tamaa yao.[2]
Kamwe, Shetani hakuwashurutisha Adam na Hawa “nendeni mle matunda ya mti ule” wala hakuwaambia moja kwa moja kwamba wasimtii Mwenyezi Mungu. Aliwanong'oneza ndani ya nyoyo zao na kuleta shaka na matamanio yenye kufadhaisha. Shetani aliwaambia Adam na Hawa, “...Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.” (Kurani 7:20) Akili zao zilijawa na mawazo ya mti huo, na siku moja waliamua kula matunda yake. Adam na Hawa walifanya tamaa kama wanavyofanya wanadamu wengine; wakajishughulisha na mawazo yao wenyewe kupitia kwa minong’ono ya Shetani na wakasahau onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ni katika hatua hii ambapo tamaduni za Kiyahudi na Kikristo zinapotofautiana sana na Uislamu. Hakuna wakati wowote maneno ya Mwenyezi Mungu - Kurani, au tamaduni na hadithi za Mtume Muhammad - zinaonyesha kwamba Shetani alikuja kwa Adam na Hawa katika umbo la nyoka.
Kamwe, Uislamu hauonyeshi kuwa Hawa alikuwa dhaifu zaidi kati ya hao wawili, au kwamba alimshawishi Adam kumuasi Mwenyezi Mungu. Ulaji wa tunda la mti huo lilikuwa kosa lililotendwa na wote wawili, Adam na Hawa. Wanachukuwa dhamana sawa. Haikuwa dhambi ya asili iliyozungumziwa katika tamaduni za Kikristo. Kizazi cha Adam hakiadhibiwi kwa dhambi ya wazazi wao wa kwanza. bali ilikuwa ni kosa, na Mwenyezi Mungu, kwa Hekima na Rehema Zake zisizo na kifani, aliwasamehe wote wawili.
Ongeza maoni