Al-Salaam – (Amani) – Jina la Mungu
Maelezo: Ufafanuzi wa mojawapo ya jina zuri la Mwenyezi Mungu, al-Salaam, ambalo linatufahamisha ukamilifu wa Mungu na kwamba Yeye ndiye chanzo cha amani na kuridhika.
- Na Sheikh Salman al-Oadah (islamtoday.net) [edited by IslamReligion.com]
- Iliyochapishwa mnamo 08 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 2,507 (wastani wa kila siku: 2)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Al-Salaam (amani) ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu. Mungu anasema: "Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani..." (Kurani 59:23)
Mwenyezi Mungu ndiye mleta amani anayeeneza amani katika viumbe vyote. Tangu uhai ulipoumbwa kwa mara ya kwanza, umetawaliwa na vipindi virefu vya amani, usalama, utulivu, na kuridhika. Mwenyezi Mungu ni Amani na kutoka kwake hutoka amani yote. Ni kama alivyosema Mtume rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Ewe Mola! Wewe ni Amani na kutoka Kwako kuna amani, mwenye utukufu na heshima."[1]
Inashangaza kwamba baadhi ya watu wanaomwomba Mungu kwa jina hili tukufu wanaishi maisha yao katika mabishano na uadui dhidi ya ulimwengu. Kila nyanja ya maisha yao imejaa ugomvi, kutoka ndani yao wenyewe, hadi tabia zao za nje, katika mawazo yao, na familia zao. Mtu wa namna hiyo anawezaje kupata amani na Mola?
Al-Salaam kama "Utimamu"
Jina al-Salaam pia lina maanisha "utimamu", ni kama kutokuwa na dosari. Inaleta maana ya kwamba Mungu hana mapungufu na upungufu, kama vile uchovu, usingizi, ugonjwa, au kifo. Uwepo wa Mungu ni ukamilifu kabisa. Mungu anasema: "Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala." (Kurani 2:255)
Mungu yuko huru kutokana na chochote ambacho kingepingana na utoshelevu wake kamili. Hakuna kinacho weza kumchosha wala kumkwepa. Hakuna kitu cha zaidi ya uwezo wake.
Watu wa Kitabu wananasibisha upungufu huo kwake pale wanapodai kuwa alipumzika siku ya saba baada ya kuumba mbingu na ardhi. Ndiyo maana Mungu anasema: "Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu." (Kurani 50:38)
Ikiwa Mungu anataka chochote kitokee, Yeye husema tu "Kuwa!" na huwa. (Kurani 36:82)
Maana hii hii ya jina al-Salaam inatumika katika elimu ya Mungu. Mungu yuko huru kwenye ujinga, shaka, na kutokuwa na maamuzi. Hakuna kinachofichika kwa ujuzi Wake. Ujuzi wake haupatikani kwa kujifunza. Ni kamili, na sahihi kabisa, inayo elewa kila kitu cha zamani, cha sasa na cha wakati ujao bila ubaguzi.
"Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo" (Kurani 58:7)
"Ni sawa anaye ficha kauli yake kati yenu na anaye idhihirisha, na anaye jibanza usiku na anaye tembea jahara mchana." (Kurani 13:10)
Kadhalika maneno Yake hayana uwongo na dhulma. Mungu anasema: "Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu." (Kurani 6:115)
Matamshi yake ni ya kweli na hukumu zake ni za haki. Sheria yake na kila dhihirisho la mapenzi yake ni kamilifu. Sheria ya Mwenyezi Mungu imejaa hekima na elimu, kama ilivyo Kurani aliyoiteremsha kwa Mtume wake. Kurani ina maana nyingi, yenye safu nyingi, inawa ongoza wanadamu kwa kila njia kwa yale yanayo wahakikishia ustawi wao katika ulimwengu huu na ujao. Inasikitisha kwamba watu wengi wanaosoma Kurani wametosheka kwa kupuuza utajiri huu na kufuata kwa upofu mila na maarifa ya kukariri. Wameshindwa kuwa na mawazo ya ubunifu na mapya, na kwa sababu hiyo wanajiingiza katika kurudi nyuma, ujinga, na kuzorota kwa utamaduni tunaoshuhudia leo.
Mungu hawezi kuwa na mpinzani, mshindani, au mshirika katika utawala wake. Yeye peke yake ndiye mwenye ukuu juu ya Uumbaji, katika ulimwengu huu na ujao.
Hukumu Yake na amri Yake sio ya dhulma na uonevu. Mtume Muhammad anatusimulia kuwa Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi waja wangu! Nimejiharamishia nafsi yangu kufanya dhulma na nimeiharamisha kwenu nyinyi kwa nyinyi, basi msidhulumiane."[2]
Kutokana na ukamilifu wa uadilifu wa Mungu, Anajizuia kamwe kutenda dhulma na anaifanya iwe haramu kwetu kudhulumiana. Anasema: "wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja." (Kurani 41:46)
Mungu anatuamuru kuimarisha sifa hii ndani yetu na tu si tendeane isivyo haki. Kwa kutenda uadilifu, tunajishughulisha na ibada kwa Mola wetu, kwani Mwenyezi Mungu si mwadilifu tu, bali anapenda uadilifu na wale wanaotenda uadilifu. Vile vile Yeye ni Mjuzi, na Anapenda maarifa na wenye maarifa. Yeye ni mzuri. Anapenda uzuri na wale wanaokuza uzuri ndani yao wenyewe. Yeye ni mkarimu, na anapenda ukarimu na watu wanaotoa sadaka. Haya yote ni katika sifa za Mola wetu Mlezi.
Maana hii ya utimamu, kutokua na dosari, inaenea hadi kwenye matendo Yake: kwa kile Anachotoa na kwa kile Anachozuia. Mungu anapotunyima kitu, haitokani na ubahili au uhaba. Ametakasika Mwenyezi Mungu kuliko hayo! Ni kwamba kutokana na hekima Yake isiyo na kikomo anazuia anachowanyima waja wake. Baadhi ya watu ni bora wakiwa matajiri wakati wengine ni bora wakiwa maskini. "Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo." (Kurani 13:26) Kadhalika, baadhi ya watu hunufaika zaidi kwa kuwa na afya njema huku wengine wakinufaika zaidi kutokana na kupata magonjwa. Mungu anajua kile kila mmoja wetu anahitaji na kile ambacho kinafaa zaidi kwetu.
Sifa zote za Mungu zinashiriki katika ukamilifu huu, kutokua na upungufu. Sifa za Mungu hazifanani na vitu vilivyo umbwa. Yeye hawezi kulinganishwa. Ni kutokana na hekima ya Mungu kwamba sisi, kama viumbe vilivyoumbwa, tuko chini ya mipaka na mapungufu yaliyo katika asili yetu na kwa taabu za kuishi duniani. Mungu kwa upande mwingine ni al-Salaam, ambaye ameepukana na mapungufu yote.
Jina la Mwenyezi Mungu al-Salaam ni kubwa kweli kweli katika maana yake kwa kuwa linaeleza ukamilifu ambao majina yote ya Mwenyezi Mungu yanayo - kwamba kila moja ya sifa za Mungu haina upungufu..
Tunaposalimiana kwa amani kwa kusema: "Al-Salaam `alaykum", tunaliita jina hili la Mwenyezi Mungu, na kwa kufanya hivyo, tunawasilisha maana hii ya ukamilifu wa Mungu pamoja na wazo la amani.
Na hakika Mwenyezi Mungu ameifanya Salamu kuwa ni maamkio ya Waumini. "Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: ‘Salama!’" (Kurani 33:44)
Ametuamuru kutumia salamu hii: "Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu." (Kurani 24:61)Kwa hiyo, Muumini anaomba amani juu yake na juu ya wengine kwa salamu hii.
Mungu ni Mtoa Amani
Hakika Mwenyezi Mungu anawasalimia viumbe wake katika ulimwengu huu kwa salamu ya amani.
"Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!." (Kurani 37:79) "Iwe salama kwa Ibrahim!." (Kurani 37:109) "Iwe salama kwa Musa na Haruni!." (Kurani 37:120) "Iwe salama kwa Ilyas." (Kurani 37:130)"Na Salamu juu ya Mitume." (Kurani 37:181)"Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa." (Kurani 27:59)"Na amani itakuwa juu ya aliye fuata uwongofu.." (Kurani 20:47)
Maamkio ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake ni amri yake kwamba watalindwa katika dunia hii na ijayo. Ingawa wako chini ya majaribu na dhiki wanazopitia duniani, Mungu huweka juu ya mioyo yao kutosheka na uhakika wa imani ambao hubadilisha matatizo yao kuwa neema na kuwapa thawabu. Nyoyo zao zimo zenye kuridhika, zilizo na amani na chochote anachowaandikia Mwenyezi Mungu.
Swahaba mashuhuri Saad ibn Abi Waqqas alibarikiwa kwa kuwa dua zake zilijibiwa kila mara. Alipokuwa kipofu, watu walimuuliza: "Kwa nini humuombj Mungu akurudishe kuona?"
Angejibu: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Kutosheka kwangu na amri ya Mwenyezi Mungu ni muhimu kwangu kuliko vile ninavyotamani."
Ee Mungu! Wewe ni Amani na kutoka Kwako kuna amani. Ubarikiwe wewe mwenye utukufu na heshima.
Ongeza maoni