Biblia Inakana Umungu wa Yesu (sehemu ya 6 kati ya 7): Ushahidi kutoka Injili ya Yohana
Maelezo: Uthibitisho wa wazi kutoka kwa Injili ya Yohana kwamba Yesu hakuwa Mungu.
- Na Shabir Ally
- Iliyochapishwa mnamo 18 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,294 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Injili ya Yohana, Injili ya nne, ilikamilishwa hadi kufika hali yake ya sasa yapata miaka sabini baada ya Yesu kuinuliwa mbinguni. Injili hii katika hali yake ya mwisho inasema jambo moja zaidi kuhusu Yesu ambalo halikujulikana katika Injili tatu zilizotangulia — kwamba Yesu alikuwa Neno la Mungu. Yohana ana maanisha kwamba Yesu alikuwa wakala wa Mungu ambaye kupitia kwake Mungu aliumba vitu vingine vyote. Hii mara nyingi haieleweki kumaanisha kwamba Yesu alikuwa Mungu Mwenyewe. Lakini Yohana alikuwa akisema, kama vile Paulo alivyokuwa amesema, kwamba Yesu alikuwa kiumbe wa kwanza wa Mungu. Katika Kitabu cha Ufunuo katika Biblia, tunaona kwamba Yesu ni: "mwanzo wa uumbaji wa Mungu" (Ufunuo 3:14, pia anaglia Wakorintho 1 8:6 na Wakolosai 1:15).
Yeyote anayesema kwamba Neno la Mungu ni mtu aliyetofauti na Mungu lazima pia akubali kwamba Neno liliumbwa, kwa maana Neno linasema katika Biblia: “BWANA alinileta nikiwa mwanzo wa kazi zake...” (Mithali 8:22).
Injili hii, hata hivyo, inafundisha waziwazi kwamba Yesu sio Mungu. Kama lisingeendelea na mafundisho haya, basi lingepingana na Injili nyingine tatu na pia barua za Paulo ambazo kutoka humo imethibitishwa wazi kwamba Yesu sio Mungu. Tunaona hapa kwamba Yesu hakuwa sawa na Baba, kwa kuwa Yesu alisema: “...Baba ni mkuu kuliko mimi.” (Yohana 14:28).
Watu wanasahau hili na wanasema kwamba Yesu ni sawa na Baba. Je, tunapaswa kumwamini nani — Yesu au watu? Waislamu na Wakristo wanakubali kwamba Mungu yupo. Hii ina maana kwamba Yeye hapati uwepo wake kutoka kwa mtu yeyote. Hata hivyo Yohana anatuambia kwamba kuwepo kwa Yesu kunasababishwa na Baba. Yesu alisema katika Injili hii: “...Ninaishi kwa ajili ya Baba...” (Yohana 6:57).
Yohana anatuambia kwamba Yesu hawezi kufanya lolote kwa uwezo wake mwenyewe anapomnukuu Yesu akisema: “Mimi mwenyewe siwezi kufanya neno lolote...” (Yohana 5:30). Hilo linapatana na yale tunayojifunza kuhusu Yesu kutoka katika Injili nyingine. Katika Marko, kwa mfano, tunajifunza kwamba Yesu alifanya miujiza kwa nguvu ambayo haikuwa ndani yake. Hii ni wazi hasa kutokana na tukio ambalo mwanamke anaponywa kutokana na kutokwa na damu isiyoweza kupona. Yule mwanamke alikuja nyuma yake, akaligusa vazi lake, naye akapona mara moja. Lakini Yesu hakujua ni nani aliyemgusa. Marko anaeleza matendo ya Yesu hivi: “Mara Yesu akatambua kwamba nguvu zilikuwa zimemtoka. Akageuka katikati ya umati na kuuliza, ‘Ni nani aliyegusa nguo zangu?’” (Marko 5:30). Wanafunzi wake hawakuweza kutoa jibu lenye kuridhisha, kwa hiyo Marko anatuambia hivi: “Yesu akaendelea kutazama huku na huku ili aone ni nani aliyefanya hivyo.” (Marko 5:32). Hii inaonyesha kwamba nguvu zilizomponya mwanamke hazikuwa chini ya udhibiti wa Yesu. Alijua kwamba nguvu zimemtoka, lakini hakujua zilienda wapi. Kiumbe mwingine mwenye akili alipaswa kuziongoza nguvu hizo kwa mwanamke ambaye alihitaji kuponywa. Mungu alikuwa yule kiumbe mwenye akili.
Si ajabu, basi, katika Matendo ya Mitume tunasoma kwamba ni Mungu ambaye alifanya miujiza kupitia Yesu (Matendo 2:22).
Mungu alifanya miujiza ya ajabu kupitia wengine pia, lakini hiyo haiwafanyi wengine kuwa Mungu (angalia Matendo 19:11). Kwa nini, basi, Yesu anachukuliwa kuwa ni Mungu? Hata Yesu alipomfufua rafiki yake Lazaro kutoka kwa wafu, ilimbidi kumuomba Mungu afanye hivyo. Martha, dada ya Lazaro, alijua hilo, kwa maana alimwambia Yesu hivi: “Ninajua kwamba hata sasa chochote utakachomuomba Mungu atakupa.” (Yohana 11:22).
Martha alijua kwamba Yesu hakuwa Mungu, na Yohana ambaye alielezea jambo hilo alijua pia. Yesu alikuwa na Mungu, kwa kuwa alipokuwa karibu kupaa mbinguni, alisema: “Ninarudi kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu na Mungu wenu.” (Yohana 20:17).
Yohana alikuwa na uhakika kwamba hakuna mtu aliyemuona Mungu, ingawa alijua kwamba watu wengi walikuwa wamemuona Yesu (angalia Yohana 1:18 na 1 Yohana 4:12). Kwa kweli Yesu mwenyewe aliwaambia umati wa watu, kwamba hawajamuona Baba kamwe, wala hawajasikia sauti ya Baba (Yohana 5:37). Zingatia ikiwa Yesu angekuwa Baba, maneno yake hapa yangekuwa ya uongo. Ni nani Mungu pekee katika Injili ya Yohana? Baba peke yake.
Yesu alishuhudia hili alipotangaza kwamba Mungu wa Wayahudi ni Baba (Yohana 8:54). Yesu pia alithibitisha kwamba Baba peke yake ndiye Mungu wa pekee wa kweli (angalia Yohana 17:1-3). Naye Yesu akawaambia adui zake: “...mnakusudia kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli niliyoisikia kwa Mungu.” (Yohana 8:40). Kulingana na Yohana, kwa hiyo, Yesu hakuwa Mungu, na hakuna chochote alichoandika Yohana kinapaswa kuchukuliwa kama uthibitisho kwamba alikuwa Mungu— isipokuwa mtu anataka kutofautiana na Yohana.
Ongeza maoni