Penomee (Dkt. Kari Ann Owen), Myahudi wa Zamani, Marekani
Maelezo: Kutokana na uzoefu mbalimbali wa maisha, Dkt. Owens anahisi ukosefu wa hisia ya kuwa mmoja wa jamii ya Marekani na Magharibi na anaangalia kwingine ili apate Mwongozo.
- Na Dr. Kari Ann Owen
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 2,303 (wastani wa kila siku: 2)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
“Hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu juu yake, ni Mtume wake."
Naamini, haya ndiyo maneno ya kiapo cha Shahada.
Muumba anajulikana kwa majina mengi. Hekima yake daima inatambulika, na uwepo wake unaonekana wazi katika upendo, uvumilivu na huruma zilizopo katika jamii yetu.
Uwezo wake mkubwa wa kutuongoza kutoka ubinafsi unaofanana na vita uliojikita mizizi katika jamii ya Marekani na kutupeleka kwa imani katika utukufu na heshima ya familia ya wanadamu, na wajibu na uanachama wetu katika familia hiyo. Hii inaelezea kukomaa kwa utu wa kiroho, na labda kukomaa unaohitajika zaidi wa nafsi ya kisaikolojia, pia.
Njia yangu ya Shahadah ilianza wakati mkurugenzi maarufu wa filamu, Tony Richardson, alikufa kutokana na UKIMWI. Bw. Richardson alikuwa tayari mtaalamu mwenye kipaji aliyetambulika kimataifa wakati nilipokuwa karibu kukutana naye nyuma ya jukwaa katika tamthilia ya Luther nikiwa na umri wa miaka 14.
Uandishi wa tamthilia kwangu ulikuwa daima njia ya kupata upatanisho wa kiroho na wa kihisia, ndani yangu na kati yangu na ulimwengu niliouona kama katili kutokana na hali ngumu za utotoni mwangu. Badala ya kupigana na ulimwengu, niliruhusu migogoro yangu ipigane nayo katika tamthilia zangu. La kushangaza ni kuwa baadhi yetu tumekua pamoja!
Kwa hivyo, nilipoanza kukusanya mafanikio ya jukwaani (utengenezaji na usomaji wa kuigizwa), kuanzia umri wa miaka 17, daima nilijihifadhia matumaini ya kwamba siku moja nitatimiza ndoto yangu ya utotoni ya kusoma na kufanya kazi na Bwana Richardson. Alipofuata ugoni-jinsia wake na kwenda Amerika (kutoka Uingereza) ili kukaa na jamii ya mashoga, UKIMWI ulimwua, na pamoja naye kuliondoka sehemu nyingine ya hisia yangu ya kuwa mmoja wa jamii ya Marekani.
Nilianza kutazama nje ya jamii ya Marekani na Magharibi kwa utamaduni wa Kiislamu ili kupata mwongozo wa kimaadili.
Kwa nini Uislamu na sio kwingine?
Mababu wa mama yangu walikuwa Wayahudi wa Hispania walioishi kati ya Waislamu hadi Baraza la Kuhukumu Wazushi la Uhispania lilipowafukuza Wayahudi mwaka wa 1492. Katika kumbukumbu yangu ya kihistoria, ambayo ninaihisi katika kina cha roho yangu, wito wa mwadhini ni kina kama utulivu wa bahari na myumboyumbo wa meli, nyayo za farasi katika jangwa, na madai ya upendo katika uso wa ukandamizaji.
Nilihisi kuzaliwa kwa hadithi ndani yangu, na tamthilia hiyo ikaanza kujitokeza niliposoma kuhusu khalifa mmoja wa dola ya Ottoman aliyewaonyesha huruma wakimbizi wa Kiyahudi wakati wa kufukuzwa kwa mababu zangu. Mungu aliongoza mafunzo yangu, na nikafundishwa kuhusu Uislamu na watu tofauti kama vile Imam Siddiqi wa Chama cha Uislamu cha South Bay; Dada Hussein wa Rahima; na dada yangu mpendwa wa kambo Maria Abdin, ambaye ni mwenyeji asili wa Marekani, Muislamu na mwandishi wa gazeti la SBIA, IQRA. Mahojiano yangu ya kwanza ya utafiti yalikuwa katika duka la nyama ya halal [nyama inayokubalika kuliwa katika sheria za Kiislamu] katika Wilaya ya Mishenari ya San Francisco, ambapo ufahamu wangu wa Uislamu hai uliathiriwa sana na mwanamke wa kwanza wa Kiislamu niliyewahi kukutana naye: mteja aliyekuwa amevaa hijab, alikuwa na wema na pia uwezo wa kusoma, kuandika na kuongea lugha nne.
Uerevu wake, pamoja na unyenyekevu wake wa ajabu (kwangu), ulikuwa na athari kubwa katika mwanzo wa maarifa yangu ya jinsi Uislamu unaweza kuathiri tabia za binadamu.
Sikujua kwamba kungezaliwa siyo tamthilia tu, bali Muislamu mpya.
Utafiti wangu ulinijulisha mengi zaidi kuhusu Uislamu kuliko mambo kadhaa, kwani Uislamu ni dini iliyo hai. Nilijifunza jinsi Waislamu wanavyojiendesha kwa heshima na wema unaowainua juu ya soko la utumwa la Marekani la ngono na uhasama. Nilijifunza kwamba wanaume na wanawake wa Kiislamu wanaweza kuwa pamoja bila ya kupigana na kushindana, kwa maneno na kimwili. Na nilijifunza kwamba mavazi ya sitara, yanayoonekana kama hali ya kiroho, yanaweza kuinua tabia ya kibinadamu na kuwapa wanaume na wanawake hisia ya thamani yao ya kiroho.
Kwa nini hii ilionekana kuwa ya kushangaza, na jambo jipya?
Kama wanawake wengi wa Marekani, nilikua katika soko la utumwa, ambalo sio tu la magonjwa ya ngono ya familia yangu, lakini hukumu hasi ya mara kwa mara ya mwonekano wangu kutoka kwa wenzangu, kuanzia umri mdogo chini ya miaka saba. Nilifundishwa tangu nikiwa mdogo sana na jamii ya Marekani kwamba thamani yangu ya kibinadamu ilikuwa tu katika mwonekano na mvuto wangu (au, kwa upande wangu, ukosefu wake) kwa wengine. Katika mazingira haya, wavulana na wasichana, wanaume na wanawake, mara nyingi walichukiana sana kwa ndani, kutokana na tamaa ya kukubalika na marika, ambayo ilionekana kutegemea kwa kiasi kikubwa sio kwa uzuri wa mtu au huruma au hata akili yake, lakini kwa mwonekano na mtazamo wake.
Huku sitarajii au kutafuta ukamilifu wa kibinadamu kutoka kwa Waislamu, tofauti za kijamii ni kubwa, na ni jambo geni sana kwa mtu kama mimi.
Siwezi kudai kuwa nina majibu yoyote kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati, isipokuwa yale ambayo manabii, wapendwa katika Uislamu, tayari wameelezea. Ulemavu wangu unanizuia nisifunge, na kusali kwa mkao sawa na sala ya [Waislamu] wengine.
Lakini ninaipenda na kuheshimu Uislamu niliyoujua kupitia tabia na maneno ya wanaume na wanawake niliokuja kuwajua katika AMILA (Waislamu wa Marekani wenye nia ya Kujifunza na Uanaharakati) na kwingineko, ambapo ninapata uhuru kutokana na migogoro ya kikatili ya kihisia na hisia ya kiroho iliyo karibu.
Nini kingine ninachohisi na kuamini kuhusu Uislamu?
Ninaunga mkono na napenda heshima ya Uislamu kwa elimu sawa ya jinsia wote; kwa haki za wanawake na wanaume katika jamii; kwa mavazi ya sitara; na juu ya yote hayo kwa ajili ya ndoa na kukatazwa kwa ulevi, ambazo kimisingi ni nguzo mbili kubwa zaidi za maisha yangu, kwa maana nina miaka 21 1/2 ambapo sijalewa na ninaishi kwa ndoa ya furaha. Ni ajabu sana kuhisi kwamba Waislamu bilioni moja na nusu wanashiriki imani yangu katika maendeleo ya tabia ambayo ndoa inatuwezesha, na pia katika uamuzi wangu wa kuepukana na madawa ya kulevya na pombe.
Je, basi ni nini zawadi kubwa zaidi ya Uislamu kwa ujumla?
Katika jamii ambayo inatupatia shinikizo la mara kwa mara ili kujiweka kwenye madhabahu za silika isiyo na heshima bila kuangalia matokeo, Uislamu unatutaka tujichukulie kama wanadamu walioumbwa na Mungu wenye uwezo wa kuwajibika katika uhusiano wetu na wengine. Kupitia kwa sala, sadaka na kujitolea kudumisha elimu na kuepukana na ulevi, tukifuata njia ya Uislamu, tutakuwa na nafasi nzuri ya kulea watoto ambao watakuwa huru kutokana na vurugu na dhuluma ambazo zinawanyang'anya wazazi na watoto wa shule usalama na ujirani, na mara nyingi maisha yao.
Ongeza maoni