Nataka kuwa Muislamu lakini... Uongo Bunifu kuhusu Kusilimu (sehemu ya 3 kati ya 3)
Maelezo: Madhambi, kuogopa watu wengine watasema nini, au kutojua Waislamu wowote hakumzuii mtu kusilimu.
- Na Aisha Stacey (© 2011 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,158 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Tulimaliza Sehemu ya 2 kwa kutaja ya kwamba mtu anaposilimu basi madhambi yake yote yaliyopita, hayajalishi ni makubwa au madogo, hufutwa. Rekodi huwa safi, haina dhambi lolote, hung'ara na ni nyeupe; huu ni mwanzo mpya. Hata hivyo, kuna watu wengine ambao wangesita kuukubali Uislamu kwa sababu wanaogopa kuwa hawataweza kuacha kuendelea kufanya dhambi. Tunaanza Sehemu ya 3 kwa kujadili mada hii.
7. Nataka kuwa Muislamu lakini najua kuna madhambi mengine siwezi kuacha kuyafanya.
Iwapo mtu anaamini ukweli ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, anapaswa kuukubali Uislamu bila kuchelewa, hata kama wanaamini ya kuwa wataendelea kutenda dhambi. Mtu akizoea kuishi maisha bila kubanwa na maadili yoyote, Uislamu unaweza kuonekana mwanzoni kama seti ya sheria na kanuni ambazo haziwezekani kutimizwa. Waislamu hawanywi pombe, Waislamu hawali nyama ya nguruwe, wanawake wa Kiislamu ni lazima wavae mitandio, Waislamu ni lazima wasali mara tano kila siku. Wanaume na wanawake hujikuta wakisema maneno kama, "Nisingeweza kuacha kunywa", au "Ningeona ugumu sana kusali kila siku seuze mara tano”.
Ukweli ni kuwa, mara tu mtu anapokubali ya kwamba hapana mungu anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kukuza uhusiano na Yeye, sheria na masharti hayazingatiwi kwa undani. Ni njia ya taratibu ya kutaka kumridhisha Mwenyezi Mungu. Kwa wengine, kukubali miongozo kwa ajili ya maisha ya furaha huchukua siku, hata saa, kwa wengine inaweza kuwa wiki, miezi, au hata miaka. Safari ya kila mtu kuingia katika Uislamu ni tofauti. Ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu husamehe madhambi yote. Muumini anaweza, kwa rehema ya Mungu, kuingizwa Peponi bila kuzingatia madhambi aliyotenda. Kwa upande mwingine, asiyeamini, anayeabudu kitu kingine au mtu mwingine asiyekuwa Mungu Mmoja wa Kweli, ataingizwa Moto wa milele. Kwa hivyo, ukipewa chaguo kati ya kutokubali kabisa Uislamu au kuwa Muislamu anayetenda dhambi, chaguo la pili kwa hakika ni borazaidi.
8. Nataka kuwa Muislamu lakini ninaogopa kuwajulisha wengine.
Kama tulivyosisitiza mara kwa mara kuwa hakuna kitu ulimwenguni ambacho kinamzuia mtu kuukubali Uislamu. Iwapo mtu anaogopa watu wengine watasema nini, kama vile wazazi wake, ndugu zake au marafiki zake, na anahisi kuwa hayuko tayari kuwajulisha, itabidi asilimu na kujaribu kuutekeleza Uislamu kwa siri kadri ya uwezo wake. Muda unavyosonga, na uhusiano wake na Mwenyezi Mungu umeimarika, imani ya mtu itakuwa na nguvu na atajua jinsi ya kushughulikia hali hiyo vizuri. Kwa kweli Muislamu mpya atajihisi huru na kuona haja ya kufahamisha ulimwengu wote juu ya uzuri wa Uislamu.
Wakati huo huo ni vizuri kuwatayarisha polepole na kwa ustadi marafiki zako na familia kuhusu mabadiliko ambayo yatajitokeza. Labda mtu anaweza kuanza kuzungumza waziwazi juu ya Mungu na dini kwa ujumla, kueleza kuvutiwa kwake na imani zingine au Uislamu hasa. Mtu anapoanza kuufuata Uislamu, ambao kwa kweli ni njia ya maisha, wale waliokaribu naye aghlabu hugundua tofauti fulani. Wataona heshima mpya inayopatikana kwao, familia na jamii kwa ujumla; wataona pia mabadiliko ya tabia kutoka wasiwasi na kutokuwa na furaha hadi kutulia na kutosheka.
Uislamu ni njia ya maisha na ni vigumu kuificha kwa muda mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa watu watakapojua umesilimu kutatokea athari fulani. Kuna wale watafurahi na kukubali, ilhali wengine watakasirika na kusikitika. Mara nyingi wale wanaokasirika, hukubali mabadiliko baada ya muda kupita. Na wanapoona mabadiliko mengi mazuri kwako, wanaweza kuanza kuthamini uongofu wako. Mtu anahitaji kuwa imara, akiamini na kujua Mungu yuko pamoja naye. Maneno yako na tajriba yako huenda ikawaongoza wengine kufuata mfano wako. Mtegemee Mungu, jifunze yote unayoweza kujua kuhusu imani yako mpya na uwezeshe nuru ya Uislamu iangaze kupitia macho yako.
9. Nataka kuwa Muislamu lakini sijui Waislamu wowote.
Watu wengine hujifunza kuhusu Uislamu kupitia kusoma, wengine kwa kutazama tabia ya Waislamu wanaowaona katika miji yao, wengine kupitia vipindi katika runinga na wengine, kupitia sauti ya wito kwenda kusali (adhana). Mara nyingine watu hutafuta na kupata uzuri wa Uislamu bila kukutana na Muislamu yeyote. Sio lazima kujua Waislamu kabla ya kusilimu.
Kusilimu ni rahisi kama kusema maneno haya, Nakiri ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu na pia nakiri ya kwamba Muhammad ni mjumbe Wake. Kusilimu sio lazima kufanywe msikitini (au kituo cha Kiislamu) na wala mashahidi hawahitajiki. Mambo haya yote, hata hivyo, ni dhihirisho la udugu wa Waislamu na dalili ya mwanzo wa imani mpya ya mtu akisaidiwa na kushirikiana na wenzake katika imani. Ikiwa hakuna kituo cha Kiislamu karibu au Waislamu kukusaidia, mtu anaweza kufuata utaratibu ulioelezwa katika "Jinsi ya Kusilimu na kuwa Muislamu”.
Baada ya kusilimu ni muhimu kwa huyo Muislamu mpya kuwasiliana na Waislamu wengine. Wafuasi wenzako wa imani mpya wanapatikana katika misikiti unapoishi na vituo vya Kiislamu, au kujitambulisha kwa Muislamu anayeishi mtaani kwenu, anayetumia usafiri wa basi moja kama wewe, au anayefanya kazi katika kampuni hiyo hiyo na wewe. Ingawa Muislamu mpya atajihisi yuko peke yake, bado ana uhusiano na Waislamu wengine bilioni 1.5.
Kabla ya au baada ya kusilimu, tovuti hii ipo kusaidia Waislamu wapya au wale wanaofikiria kuwa Waislamu. Utapata humu mamia ya makala kuhusu Uislamu ambazo ni rahisi kueleweka. Baada ya kusilimu, tovuti hii itakusaidia kuanza kama Muislamu mpya kwa kukupa nyenzo muhimu na usaidizi wa mtandaoni kupitia Live-Chat (Gumzo ya Moja kwa Moja).
Ongeza maoni