Mungu yuko wapi?
Maelezo: Mwenyezi Mungu yuko juu ya mbingu, juu ya viumbe vyake.
- Na Aisha Stacey (© 2009 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 07 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 07 Aug 2023
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,851 (wastani wa kila siku: 3)
- Imekadiriwa na: 93
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Mara kwa mara wanadamu wanasukumwa kujiuliza baadhi ya maswali mazito ya maisha. Katika giza tulivu la usiku, wakati nyota za mbali zinameta katika anga kubwa, kuu, au katika baridi, ngumu, mwanga wa mchana wakati maisha yanapita kama treni inayoenda kwa kasi, watu wa rangi zote, kabila na imani wanashangaa juu ya maana ya kuwepo kwao. Kwa nini tupo hapa? Je, haya yoteyanamaanisha nini? Je, haya yote yapo?
Katika siku za kupendeza zilizo jaa mwanga wa jua na anga ya bluu inayong'aa, watu huelekeza nyuso zao kuelekea kwenye jua na kutafakari uzuri wake. Katika majira ya baridi kali au dhoruba kali zaidi, wanatafakari ushupavu unaopatikana katika nguvu za asili. Mahali fulani katika sehemu ya ndani ya akili, dhana ya Mungu hutokea. Maajabu ya uumbaji ni wito kwa moyo na roho. Mguso wa upole wa theluji, harufu ya nyasi iliyokatwa, matone ya mvua na upepo mkali wa kimbunga ni vikumbusho kwamba ulimwengu huu umejaa maajabu.
Maumivu na huzuni zinapo karibia kutukumba, wanadamu wanachochewa tena kutafakari maana ya maisha. Katikati ya mateso na huzuni, dhana ya Mungu hutokea. Hata wale ambao wangejiona kuwa wako mbali na dini au imani ya kiroho hujikuta wakitazama angani na kuomba msaada. Moyo unapotubana na hofu inapotusonga, bila msaada tunageuka kuelekea aina fulani ya uwezo wa juu zaidi. Basi dhana ya Mungu inakuwa halisi na yenye maana.
Katikati ya kusihi na kujadiliana, ukubwa kamili wa ulimwengu unawekwa wazi. Ukweli wa maisha umejaa hofu na mshangao. Ni ya kubadilika badilika. Kuna nyakati za furaha kubwa, na nyakati za huzuni nyingi. Maisha yanaweza kuwa marefu na ya kupendeza au yanaweza kuwa ya kutojali. Mungu anapoinuka na ukuu wake unapo kua wazi, maswali zaidi huanza kujitokeza. Swali moja ambalo bila kuepukika huja akilini ni - Mungu yuko wapi?
Ulimwenguni kote na mpaka enzi hizo watu wamejitahidi sana kuafikiana na swali la Mungu yuko wapi. Mwelekeo wa mwanadamu ni kumtafuta Mungu. Wababiloni na Wamisri wa kale walijenga minara mirefu katika kumtafuta Mungu. Waajemi walimtafuta katika moto. Bado mengine, kama vile wenyeji wa Amerika Kaskazini na watu wa Kiselti walimtafuta Mungu katika ishara tukufu za asili zilizo wazunguka. Wabudha humpata Mungu ndani yao wenyewe, na katika dini ya Kihindu, Mungu anaaminika kuwa katika kila mahali na katika kila kitu.
Kumtafuta Mungu kunaweza kutatanisha. Wakati wa kuuliza swali Mungu yuko wapi, majibu yanayotoka yanaweza kuwa ya kutatanisha pia. Mungu yuko kila mahali. Mungu yuko moyoni mwako. Mungu ni mahali ambapo wema na uzuri upo. Hata hivyo, ni nini hutokea wakati moyo wako ni mtupu na mazingira yako ni ya huzuni, machafu, na mabaya? Je, Mungu ataacha kuwapo? Hapana! Hapana bila shaka! Katikati ya mchanganyiko huu, dhana ya Kiislamu ya Mungu ni taa ya mwanga kwa wale wanaojikwaa gizani.
Kile ambacho Waislamu wanaamini juu ya Mungu kipo wazi na ni rahisi. Hawaamini kwamba Mungu yuko kila mahali; wanaamini kwamba Mungu yuko juu ya mbingu. Hitaji la mwanadamu kuelekeza nyuso zetu angani wakati wa shida na ugomvi ni jibu la asili kwa swali, Mungu yuko wapi? Mungu anatuambia katika Kurani kwamba Yeye ndiye Aliye juu (Kurani 2:255) na kwamba Yeye yuko juu ya Viumbe Vyake vyote.
“Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo yatenda.” (Kurani 57:4)
Mtume Muhammad alijulikana kwa kuelekezea angani wakati akimtaja Mungu. Alipokuwa akiomba dua kwa Mungu aliinua mikono yake kuelekea mbinguni. Wakati wa khutba yake ya kuaga, Mtume Muhammad aliwauliza watu, “Je, sijafikisha ujumbe huo?” nao wakasema, “Ndio!” Akauliza tena, “Je, sijafikisha ujumbe huo?” nao wakasema, “Ndio!” Akauliza mara ya tatu, “Je, sijafikisha ujumbe huo?” nao wakasema, “Ndio!” Kila mara alisema, “Ee Mwenyezi Mungu, shuhudia!" - wakati huo huo akielekeza juu mbinguni na kisha kwa watu.[1]
Mwenyezi Mungu yuko juu ya mbingu, juu ya viumbe vyake. Hata hivyo hii haimaanishi kwamba Yeye yuko na aina yoyote ya vipimo vya kimwili. Mungu yuko karibu, karibu sana, na wale wanaomwamini na anajibu kila wito wao. Mungu anajua siri zetu zote, ndoto, na matakwa yetu, hakuna kitu kinachofichwa kwake. Mungu yuko pamoja na viumbe vyake kwa ujuzi wake na uwezo wake. Mungu ndiye Muumbaji na Mlinzi. Hakuna kitu kinachopatikana isipokuwa kwa mapenzi yake.
Waislamu wanapostaajabishwa na maajabu ya ulimwengu wanakuwa salama katika kujua kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu yuko juu ya mbingu, na wanafarijiwa na ukweli kwamba yuko pamoja nao katika mambo yao yote. Muislamu anapopatwa na hasara au huzuni, haulizi hekima ya Mwenyezi Mungu, au kuuliza, ‘Mungu alikuwa wapi nilipokua na masikitiko, au nikihuzunika au nikiteseka?’ Wanadamu wameumbwa kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu, (Kurani 51:56) na Mungu alisema mara nyingi kwamba majaribu na dhiki zingekuwa sehemu ya uzoefu wetu wa maisha.
“Na Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita...ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo.” (Kurani 11:7)
Katika usiku wao wa giza zaidi, au saa yao ya giza zaidi kwa asili wanadamu hutazama angani. Mioyo yao inapodunda sana na woga unatishia kuwatawala, watu humgeukia Mungu. Wanainua mikono yao na kuomba rehema, msamaha, au wema, na Mungu anajibu; Kwani Yeye ni Mwingi wa kurehemu, Mwingi wa kusamehe na Mpole. Mwenyezi Mungu ni tofauti na amejitenga na viumbe vyake, na hakuna kitu kama Yeye. Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona. (Kurani 42:11) Hivyo tunapouliza swali yuko wapi Mwenyezi Mungu, bila shaka jibu ni kwamba, Yuko juu ya mbingu na juu ya viumbe vyake vyote. Pia tunasema kwamba Yeye si mhitaji wa kiumbe chake chochote na viumbe vyote vinamhitaji Yeye.
Rejeleo la maelezo:
[1] Maandishi ya Khutba ya Kuaga yanaweza kupatikana katika Sahih Bukhari na Sahih Muslim, na katika vitabu vya At Tirmidhi na Imamu Ahmad.
Ongeza maoni