Mtume Yona
Maelezo: Mwenyezi Mungu pekee ndiye chanzo cha msaada kwa walio katika dhiki.
- Na Aisha Stacey (© 2009 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 10 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,637 (wastani wa kila siku: 3)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Mtume Yona[1] alitumwa kwa jamii iliyokuwa ikiishi Iraki. Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu, ibn Kathir anauita mji huo Ninawi. Kama ilivyokuwa kwa Manabii wote wa Mungu, Yona alikuja Ninawi ili kuwaita watu kumwabudu Mungu Mmoja. Alizungumza kuhusu Mungu asiyekuwa na washirika wowote, wana, mabinti au washirika sawa na kuwaomba watu waache kuabudu sanamu na kujihusisha na tabia mbaya. Hata hivyo, watu walikataa kusikiliza, wakajaribu kumpuuza Yona na maneno yake ya maonyo. Walimuona ni kama anawakera.
Mwenendo wa watu wake ulimchukiza Yona na akaamua kuondoka. Alitoa onyo la mwisho kwamba Mungu angewaadhibu kwa sababu ya tabia zao za kiburi lakini watu walimdhihaki na kudai kwamba hawakuwa na woga. Moyo wa Yona ulijaa hasira kwa watu wake wapumbavu. Aliamua kuwaacha katika mateso yao yasiyoepukika. Yona alikusanya virago vyake na kuamua kuenda mbali na watu aliokuja kuwadharau.
“Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika.” (Kurani 21:87)
Ibn Kathir anaeleza kuhusu matukio huko Ninawi mara baada ya Yona kuondoka. Anga ilianza kubadilika rangi, ikageuka kuwa nyekundu kama moto. Watu waliogopa na kuelewa kwamba wangeangamia baada ya muda mchache. Wakazi wote wa Ninawi walikusanyika juu ya mlima na kuomba msamaha wa Mungu. Mungu akakubali toba yao, na kuondoa adhabu iliyokuwa juu ya vichwa vyao. Anga ilirudi kuwa kawaida, na watu wakarudi nyumbani kwao. Waliomba kwamba Yona angerudi kwao na kuwaongoza kwenye njia Iliyonyooka.
Wakati huo huo, Yona alikuwa amepanda meli kwa matumaini kwamba ingempeleka mbali na watu wake wakaidi. Meli na abiria zake wengi walisafiri katika bahari tulivu. Giza lilipowazunguka, bahari ilibadilika ghafla. Upepo ulianza kuvuma kwa ukali na kusababisha dhoruba kali. Meli iliyumbayumba kama kwamba ilikuwa karibu kugawanyika vipande vipande. Watu walijikusanya gizani wakaamua kutupa mizigo yao baharini lakini haikuleta tofauti yoyote. Upepo ulipiga na meli ikaendelea kuyumbayumba. Abiria waliona uzito wao ndio ulikuwa unachangia hali hiyo, hivyo wakaamua kupiga kura ili kutupa mmoja wa abiria baharini.
Mawimbi yalikuwa makubwa kama milima na dhoruba ikatumbukiza meli juu na chini kama kwamba haikuwa na uzito. Ilikuwa ni desturi ya ubaharia kupiga kura kwa kuandika majina yote na kuchagua mtu mmoja wa kutupwa baharini. Uchaguzi ulifanywa na jina lililotokea lilikuwa ni la Yona, ila watu walishangaa. Yona alijulikana kuwa mcha Mungu na mwadilifu na hawakutaka kumtupa baharini. Wakafanya bahati-nasibu tena na tena, lakini mara zote mbili jina lilikuwa la Yona.
Yona, Nabii wa Mungu alijua kwamba hili halikuwa jambo la kibahati. Alielewa kwamba hii ilikuwa majaliwa kama ilivyoamuliwa na Mungu, kwa hivyo aliwaangalia abiria wenzake na kujitupa baharini. Abiria waliogopa walipoona Yona akianguka ndani ya maji na kumezwa na nyangumi.
Fahamu zilipomrudi Yona, alidhani kwamba amekufa na alikuwa amelala katika giza la kaburi lake. Aligusa gusa kando yake na kutambua kwamba hili halikuwa kaburi bali tumbo la nyangumi. Aliogopa. Alihisi moyo wake ukidunda kwa hofu. Yona alikuwa ameketi juu ya viowevu vikali, tindikali za utumbo ambazo zilikuwa zinaharibu ngozi yake na akamlilia Mungu. Katika giza la samaki, katika giza la bahari na katika giza la usiku Yona akainua sauti yake na kumwita Mungu.
“Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu!” (Kurani 21:87)
Yona aliendelea kuomba na kurudia rudia dua yake kwa Mungu. Alitambua makosa yake na kuomba msamaha wa Mungu. Mtume Muhammad, rehema ziwe juu yake, anatuambia kwamba malaika wanavutiwa wanadamu wakimkumbuka Mungu. Hili ndilo lililomtendekea Nabii Yona; malaika walisikia kilio chake gizani na kutambua sauti yake. Walimjua Mtume Yona na tabia zake nzuri akiwa kwenye matatizo. Malaika wakamwomba Mungu wakisema, “Je! hiyo ni sauti ya mtumishi wako mcha Mungu?
Mungu akajibu ndiyo. Mungu alisikia wito wa Yona na kumwokoa kutokana na dhiki yake. Yona alimkumbuka Mungu wakati wa raha, hivyo Mungu alimkumbuka Yona wakati wake wa dhiki. Dua ambayo Yona alitumia inaweza kurudiwa na mtu yeyote wakati wa dhiki. Mwenyezi Mungu alisema katika Qur'ani kwamba alimwokoa Yona, na hivyo atawaokoa Waumini.(Kurani 21:88)
Kwa amri ya Mungu nyangumi alitoka nje na kumtupa Yona ufukoni. Mwili wa Yona ulikuwa umechomwa na viowevu vya utumbo; ngozi yake haikuweza kumlinda kutokana na jua na upepo. Yona alikuwa na maumivu na kuendelea kuomba apewe ulinzi. Aliendelea kurudia dua yake na Mungu alisababisha mmea kutokeza juu yake na kumpa ulinzi kutokana na jua na baridi na kumpa chakula. Yona alivyoanza kupona polepole alitambua kwamba alihitaji kurudi kwa watu wake na kuendelea na kazi ambayo Mungu alikuwa amempatia.
"Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye. Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.” (Kurani 37:139-148).
Yona alipopona, alirudi Ninawi na kushangazwa na mabadiliko ya watu wake. Wakamjulisha Yona kuhusu hofu yao wakati mbingu ziligeuka nyekundu na jinsi walivyokusanyika mlimani ili kumwomba Mungu msamaha. Yona aliishi miongoni mwa watu wake na kuwafundisha kumwabudu Mungu Mmoja na kuishi maisha ya uchaji Mungu na zaidi ya watu 100,000 walioishi Ninawi waliishi katika utulivu... kwa muda.
Hadithi ya Mtume Yona inatufundisha kuwa na uvumilivu, hasa wakati wa masaibu. Inatufundisha kumkumbuka Mungu katika nyakati nzuri na mbaya. Inatufundisha kumkumbuka Mungu katika maisha haya ili atukumbuke tunapokufa. Tukikumbuka Mungu tukiwa vijana atatukumbuka tunapokuwa wazee na tukimkumbuka Mungu tunapokuwa na afya atatukumbuka tunapokuwa na ugonjwa, huzuni, au uchovu. Dhiki inaweza kutatuliwa tu kwa kumgeukia Mungu kwa unyofu.
Ongeza maoni