Wanawake katika Uislamu (sehemu ya 1 kati ya 2)
Maelezo: Hadhi ya mwanamke na usawa wa kijinsia katika Uislamu.
- Na Mostafa Malaekah
- Iliyochapishwa mnamo 22 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 15 Aug 2023
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 6,546
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Utangulizi
Suala la usawa wa kijinsia ni muhimu, faafu, na linaloendana na wakati tulio nao. Mijadala na maandishi kuhusu mada hii inaongezeka na ipo katika mitazamo tofauti. Mtazamo wa Uislamu kuhusu suala hili umefahamika kwa uchache na kufasiriwa vibaya sana na wasio Waislamu na baadhi ya Waislamu vilevile. Makala hii imekusudiwa kutoa muhtasari na ufafanuzi sahihi wa msimamo wa Uislamu kuhusu suala hili.
Wanawake katika Tamaduni za Zamani
Ili uelewe vyema hadhi waliopewa wanawake kupitia Uislamu, mtu hana budi kuilinganisha na mifumo ya sheria nyingine zilizopo sasa na zilizokuwepo zamani.
(1) Mfumo wa Uhindi: Imeelezwa katika Ensaiklopidia Britannica, ya 1911: “Huko India, kugandamizwa kulikuwa kanuni kuu. Mchana na usiku wanawake sharti wawe chini ya walinzi wao katika hali ya utegemezi amesema Manu. Sheria ya urithi iliegemea kuumeni zaidi, yaani wanaorithi wanafuatiliwa kutokana na nasaba ya kiume wakiwabagua wanawake.” Katika maandiko ya Wahindu, wasifu wa mke mzuri ni kama ufuatao: “ni mwanamke ambaye mawazo yake, mazungumzo yake na mwili wake unaweza kudhibitiwa, ndiye hupata umashuhuri hapa duniani, na, kesho ahera, atapata makazi pamoja na mumewe.” (Mace, Ndoa ya Mashariki na Magharibi).
(2) Mfumo wa Kigiriki: Huko Athene, wanawake hawakuwa tofauti sana na wale kutoka India wala Roma: “Wanawake wa Kiathenia daima walikuwa duni, wakiwa chini ya himaya ya baadhi ya wanaume - baba zao, kaka zao, au baadhi ya jamaa zao wa kiume.” (Allen, E. A., Historia ya Tamaduni). Ridhaa yake katika ndoa haikuhitajika na “alilazimika atii matakwa ya wazazi wake, na kupokea kutoka kwao mumewe na bwana wake, hata kama ni mgeni kwake.” (Rejeleo Lililopita)
(3) Mfumo wa Kirumi: Mwanamke wa Kirumi alisifiwa na mwanahistoria mmoja kuwa hivi: “mchanga, mdogo kiumri, anayelelewa, mtu asiyeweza kufanya kibinafsi au kwa niaba ya mwingine kitu chochote kwa kupenda kwake, mtu ambaye daima atakuwa chini ya usimamizi na ulezi wa mume wake.” (Rejeleo Lililopita). Katika Ensaiklopidia Britannica, ya 1911, tunapata muhtasari wa hadhi ya kisheria ya wanawake katika utamaduni wa Warumi: “Katika Sheria ya Kirumi mwanamke alikuwa mtegemezi mno hata wakati wa matukio ya kihistoria. Iwapo ameolewa, yeye na mali yake humilikiwa na mumewe . . . mke alikuwa bidhaa iliyonunuliwa na mumewe, mithili ya mtumwa aliyenunuliwa kutokana na manufaa yake. Mwanamke hawezi kuchaguliwa au kushikilia wadhifa wowote wa kiserikali au wa umma . . . hawezi kuwa shahidi, mdhamini, mkufunzi, au mtunzaji; hawezi kupanga mtoto au kupangwa, au kuandika wasia au kufanya mkataba.”
(4) Mfumo wa Kiskandinevia: Miongoni mwa koo za Waskandinevia wanawake walikuwa: “chini ya uangalizi wa kudumu, ikiwa wameolewa au hawajaolewa. Katika enzi za baadaye za Kanuni za V za Wakristo, mwishoni mwa Karne ya 17, ilipitishwa kuwa iwapo mwanamke ataolewa bila idhini ya msimamizi wake, basi huyo msimamizi wake anaweza, akitaka, kusimamia na kuisarifu anavyopenda mali ya huyo mwanamke katika maisha yake yote.” (Katika Ensaiklopidia Britannica, ya 1911).
(5) Mfumo wa Uingereza: Huko Uingereza, haki ya wanawake walioolewa ya kumiliki mali haikutambuliwa mpaka mwisho wa Karne ya 19, “Kupitia mfululizo wa sheria kuanzia Sheria ya Mali ya Wanawake Walioolewa ya 1870, iliyorekebishwa mnamo 1882 na 1887, wanawake walioolewa walifanikiwa kupata haki ya kumiliki mali na kuingia katika mikataba kama vile waseja, wajane, na watalaka.” (Ensaiklopidia Britannica, ya 1968). Huko Ufaransa, hadi kufikia 1938, Sheria ya Ufaransa iliweza kurekebishwa ili kuwatambua wanawake kustahiki kufanya muamala wowote wa mkataba. Mwanamke aliyeolewa, hata hivyo, bado alihitajika kupata idhini ya mumewe kabla hajaigawa au kutoa mali yake ya kibinafsi.
(6) Katika Sheria za Musa (Kiyahudi): Mke alikuwa amechumbiwa. Ikiieleza dhana hii, katika Ensaiklopidia Biblica, ya 1902, inafafanua: “Kumchumbia mke kunamaanisha kummiliki baada ya kulipa pesa; aliyechumbiwa ni msichana aliyelipiwa pesa.” Kwa mtazamo wa kisheria, ridhaa ya mwanamke haikuhitajika kuhalalisha ndoa yake. “Ridhaa ya msichana sio muhimu na uhitaji wake haujapendekezwa popote katika Sheria.” (Rejeleo Lililopita). Kuhusu haki ya talaka, tunasoma katika Ensaiklopidia Biblica: “Mwanamke akiwa mali ya mwanamume, kinachofuata ni kumpa mwanamume huyo haki ya kumtaliki kama jambo la kawaida.” Haki ya kutaliki ilishikiliwa na mume tu, Katika Ensaiklopidia Britannica, 1911, inafafanua: “Katika Amri za Musa talaka ilimpendelea mume na kumpa yeye mahususi tu kuitekeleza...”
(7) Kanisa la Kikristo: msimamo wa Kanisa la Kikristo hadi karne za hivi majuzi uliathirika sana na Amri za Musa pamoja na fikra zilizotiririka na kuenea katika mila za wakati huo. Katika kitabu chao, Ndoa ya Mashariki na Magharibi, David na Vera Mace waliandika: “Mtu yeyote asidhaniye, halikadhalika, kwamba urithi wetu wa Kikristo hauwezi kuwa na mabezo ya hukumu. Itakuwa shida sana kupata popote mkusanyiko wa marejeleo yanayomtweza mwanamke kuliko yaliyotolewa na Kanisa la akina Baba waasisi. Lecky, mwanahistoria maarufu, anazungumzia juu ya ‘vichocheo hivi shadidi vinavyounda sehemu ya maandishi yaliyo bayana na ya kutisha ya akina Baba . . . mwanamke aliwakilishwa kama mlango wa jehanamu, kama chanzo cha maovu yote ya mwanadamu. Anatakiwa aone aibu kuwa yeye ni mwanamke. Anatakiwa aishi siku zote akitubia kutokana na laana aliyoiletea dunia. Anatakiwa afedheheke na vazi lake, linalomkumbusha kuanguka kwake. Anatakiwa afedheheke hasa na urembo wake, kwani ni silaha yenye nguvu ya shetani.’ Mojawapo wa mashambulizi makali dhidi ya mwanamke yanatoka kwa Tertullian: ‘Je, unajua kuwa kila mmoja wenu ni Hawa? Hukumu ya Mungu kwa jinsia hii yenu inaishi katika zama hizi; lawama lazima ibaki leo pia. Wewe ndiye mlango wa shetani; wewe ndiye mvunjaamri wa ule mti uliopigwa marufuku; wewe ndiye mhamaji wa kwanza wa sheria za Mungu; wewe ndiye nafsi ya kike aliyeshawishi nafsi ya kiume ambayo shetani hakuweza kuishambulia kirahisi.’ Sio tu Kanisa lilithibitisha hadhi duni ya mwanamke, pia lilimnyima haki zake za kisheria alizokuwa nazo hapo awali.”
Misingi ya Usawa wa Kiroho na Kiutu katika Uislamu
Katikati ya giza lililogubika dunia nzima katika Karne ya saba, wahyi kutoka kwa Mungu ulipiga mwangwi katika jangwa pana la Uarabuni kuleta ujumbe mpya, tukufu na kwa ajili ya walimwengu wote, unaoelezwa hapa chini.
(1) Kulingana na Kurani Tukufu, wanaume na wanawake wana maumbile sawa ya kiroho:
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, ambaye aliwaumba kutokana na nafsi moja na akamuumba kutokana na nafsi hiyo hiyo mwenza wake (mke wake) na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi...” (Kurani 4:1, tazama pia 7:189, 42:11, 16:72, 32:9, na 15:29)
(2) Mungu amewekeza katika jinsia zote mbili kwa heshima ya asili na amewapa madaraka wanaume na wanawake wote kuwa makhalifa au wadhamini wa Mungu ardhini (tazama Kurani 17:70 na 2:30).
(3) Kurani haimlaumu mwanamke kuwa chanzo cha “kuporomoka kwa binadamu,” wala haichukulii ujauzito na kuzaa kuwa adhabu ya kuasi kwa “kula kutoka mti ulioharamishwa.” Kinyume na hayo, Kurani inadhihirisha kuwa wote Adam na Hawa walifanya dhambi kwa pamoja ndani ya Bustani la Peponi, bila kumtenga Hawa ndiye wa kulaumiwa pekee. Wote walitubia, na wakasamehewa kosa lao (tazama Kurani 2:36-37 na 7:19-27). Kwa hakika, katika aya moja (Kurani 20:121) Adam alilaumiwa mahususi. Kurani pia inathamini ujauzito na kuzaa kuwa miongoni mwa sababu tosha za akina mama kupendwa na kuheshimiwa na watoto wao (Kurani 31:14 na 46:15).
(4) Wanaume na wanawake wana wajibu na majukumu sawa ya kidini na kimaadili. Kila mwanadamu atalipwa malipo kulingana na amali au matendo yake:
“Na Mola wao akayakubali maombi yao (akajibu): Hakika sipotezi ujira wa kazi ya mfanyakazi (yeyote) miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi...” (Kurani 3:195, tazama pia 74:38, 16:97, 4:124, 33:35, na 57:12)
(5) Kurani iko wazi kabisa kuhusu suala la madai ya ubora au udhalili wa mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke. Linalozingatiwa katika msingi pekee wa ubora wa mtu yeyote juu ya mwingine ni uchaji Mungu na tabia njema, wala sio jinsia, rangi au utaifa (tazama Kurani 49:13).
Kipengee cha Uchumi wa Wanawake katika Uislamu
(1) Haki ya Kumiliki Mali ya Kibinafsi: Uislamu umepitisha hukumu ya haki ya mwanamke aliyonyimwa kabla na baada ya Uislamu (hadi mwishomwisho wa karne hii), haki ya umiliki wa kibinafsi. Sheria ya Kiislamu inatambua haki kamili za mali kabla na baada ya ndoa. Wao wanaweza kununua, kuuza, au kukodisha mojawapo wa au zote za mali zao wanavyopenda. Kwa sababu hii, wanawake wa Kiislamu wanaweza kuendelea kuitwa (na bila shaka yoyote wamekuwa kwa kawaida wakiitwa) kwa majina yao ya utotoni baada ya kuolewa, kama ishara ya uhuru wao wa haki ya kumiliki kisheria.
(2) Usalama wa Kifedha na Sheria za Mirathi: Usalama wa kifedha umehakikishiwa wanawake. Wana haki kupokea zawadi za ndoa au mahari bila kikomo na kuendelea kumiliki mali zao na mapato yao wakati wa sasa na wa baadaye kwa ajili ya usalama wao, hata baada ya ndoa. Hakuna mwanamke yeyote aliyeolewa anahitajika kutumia kiasi chochote kutoka kwa mali zake au mapato yake kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Mwanamke pia ana haki ya kupewa masurufu yake kamili wakati wa ndoa na wakati wa 'kipindi cha kusubiri' (eda) ikiwa ameachwa au amefiliwa. Wanazuoni wengine wanalazimisha, kuongezwa, msaada wa mwaka mmoja kupewa mtalaka na mjane (au aliyeachwa mpaka warejeleane, iwapo kurudiana kuoana kutatokea kabla ya mwaka kwisha). Mwanamke anayebeba au kujifungua mtoto ndani ya ndoa ana haki ya kupewa masurufu ya mtoto na baba mzazi. Kwa ujumla, mwanamke wa Kiislamu anahakikishiwa kupewa msaada wa kifedha katika hatua zake zote za maisha, kama binti, mke, mama, au dada. Ingawa wanawake, na sio wanaume, wamepewa kipaumbele katika matumizi ya kifedha katika ndoa na familia, Kurani vilevile imempa mwanamume mafungu mara mbili kuliko mwanamke katika sheria ya mirathi ili kusawazisha hayo. Wanaume hawarithi zaidi kila wakati; mara nyingine mwanamke hurithi zaidi ya mwanamume. Endapo wanaume watarithi zaidi bado watawajibika kifedha kuwaangalia jamaa zao wa kike: wake, mabinti, mama, na dada zao. Wanawake hurithi kidogo lakini wataendelea kuhifadhi mgao wao wa uwekezaji na usalama wa kifedha, bila ya kuwajibika kisheria kutumia sehemu yao yoyote ile, hata kwa kujikimu wenyewe (kwa ajili ya chakula, mavazi, malazi, matibabu, n.k.). Ikumbukwe kuwa kabla ya Uislamu, wanawake wenyewe walikuwa wakirithiwa pia (tazama Kurani 4:19). Katika baadhi ya nchi za kimagharibi, hata baada ya kuja kwa Uislamu, urathi wote wa marehemu ulipewa mtoto mkubwa (wa kwanza) wa kiume. Hata hivyo, Kurani iliweka wazi kuwa wote wanaume na wanawake wana haki kupata mgao maalumu wa urathi wa wazazi wao waliokufa au jamaa zao wa karibu. Mungu anasema:
“Wanaume wanayo sehemu katika walichokiacha wazazi na jamaa wa karibu, na wanawake wanayo sehemu katika walichokiacha wazazi na jamaa wa karibu, kiwe kidogo au kingi, mgao uliofaridhiwa.” (Kurani 4:7)
(3) Ajira: Kuhusu haki ya mwanamke kutafuta kazi, ni sharti ibainike kwanza kuwa Uislamu unazingatia nafasi yake katika jamii kama mama na mke kuwa adhimu na muhimu zaidi. Hakuna wajakazi wala mlezi wa watotot wa muda wanaoweza kuchukua nafasi ya mama kama mwalimu wa mwana aliyenyooka, asiye na hisia za kujitwaza au kujitweza, na aliyeleleka kwa misingi imara. Hilo ni jukumu bora na muhimu, ambalo kwa kiasi kikubwa linaunda mustakabali wa mataifa, haliwezi kamwe kuzingatiwa kama uvivu. Walakini, hakuna amri katika Uislamu ambayo inakataza wanawake kutafuta ajira wakati wowote kunapotokea haja ya kufanya hivyo, hasa katika nafasi ambazo zinachukuana barabara na maumbile yake, na ambayo jamii inamuhitajia zaidi. Mifano ya kazi hizo za kitaaluma ni uuguzi, ualimu (kufunza hasa watoto), utabibu, na kazi za kijamii na za kutoa misaada.
Maoni
Ongeza maoni