Hadithi ya Adamu (sehemu ya 5 kati ya 5): Mwanadamu wa Kwanza na Sayansi ya Kisasa
Maelezo: Baadhi ya matokeo ya kisasa kuhusu hali ya kawaida ya wanadamu kwa kulinganisha na baadhi ya ukweli wa Kurani.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 7,620 (wastani wa kila siku: 7)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Katika Uislamu, hakuna mgogoro kati ya imani ya Mungu na ujuzi wa kisasa wa kisayansi. Ama kwa kweli, kwa karne nyingi katika Enzi za Kati, Waislamu waliongoza ulimwengu katika uchunguzi wa kisayansi na ugunduzi . Kurani yenyewe, iliyoteremshwa karibu karne 14 zilizopita, imejaa ukweli na taswira ambazo zinaungwa mkono na matokeo ya kisasa ya kisayansi. Tatu kati ya hizo zitatajwa hapa. Mojawapo, ni maendeleo ya lugha na seli hai za vinasaba kutoka Hawa, mama wa wanadamu wote (jenetiki) ni maeneo mapya kwenye tafiti za kisayansi.
Kurani inawaamuru Waislamu “tafakari maajabu ya uumbaji” (Kurani 3:191)
Moja ya kipengele cha tafakuri hiyo ni taarifa hii:
“Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo...” (Kurani 38:71)
Kwa hakika, elementi (vitu vingi vya asili) zilizomo duniani kadhalika zinapatikana katika mwili wa mwanadamu. Sehemu muhimu zaidi inayowezesha uhai ardhini ni mchanga wa juu wenye rotuba; tabaka hilo jembamba la udongo mweusi, wenye utajiri mwingi wa kaboni ndimo mimea hutandaza mizizi yake. Ni katika tabaka hili jembamba la mchanga lililo muhimu ambamo viumbe vidogo au vidubini hubadilisha malighafi, nayo ni madini ambazo huunda udongo wa msingi wa mchanga huu wa juu, na kuyafanya yapatikane kwa ajili ya kuendeleza maisha ya aina nyingi za viumbe vilivyokaribu na juu yake.
Madini ni elementi (vitu vya asili) zisokaboni zenye kutoka katika ardhi ambazo mwili hauwezi kutengeneza. Madini yana majukumu muhimu katika kazi mbalimbali za mwilini na yanahitajika kumudu maisha na kudumisha afya bora, na hivyo ni virutubisho muhimu sana.[1]
Madini haya hayawezi kutengenezwa na mwanadamu; hayawezi kuzalishwa kwenye maabara wala hayawezi kutengenezwa kwenye kiwanda
Seli huwa na asilimia 65-90 ya maji kwa uzito, kwa hiyo maji, au H₂O,huwa sehemu kubwa ya mwili wa mwanadamu. Isitoshe, sehemu kubwa ya wingi wa mwili wa binadamu ni oksijeni. Kaboni, kitengo msingi cha molekuli za kikaboni, ndio hufuata. Asilimia 99 ya uzito wa mwili wa mwanadamu unajumuisha elementi sita tu: oksijeni, kaboni, hidrojeni, nitrojeni, kalsiamu, na fosforasi.[2]
Mwili wa mwanadamu una kiasi kidogo cha kila madini ya duniani; ikiwa ni pamoja na salfa, potasiamu, zinki, shaba, chuma, alumini, kromiamu, platinamu, boroni, silikoni, seleniamu, molibidenamu (chuma cha fedha kisichofulika kirahisi), florini, klorini, iodini, manganizi, kobalti, lithiamu, strontiamu, alumini, risasi, vanadiamu, arseniki, bromini na nyinginezo.[3] Bila madini haya, vitamini zinaweza kuwa na athari kidogo au kutokuwa nayo kabisa. Madini ni kichocheo, huchochea maelfu ya athari za vimeng'enya muhimu katika mwili. Elementi za ufuatiliaji zina jukumu muhimu la kumwezesha mwanadamu kuwa na afya. Inafahamika kwamba ukosefu wa madini ya iodini husababisha ugonjwa wa tezi na upungufu wa kobalti utatuacha bila vitamini B12, na bila shaka kutoweza kuzalisha seli nyekundu za damu.
Aya nyingine ya kutafakari ni:
“Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote.” (Kurani 2:31)
Adam alifundishwa majina ya kila kitu; alipewa uwezo wa kufikiri na uhuru wa kuchagua. Alijifunza jinsi ya kupanga vitu kwa mafungu na kuelewa manufaa yake. Hivyo basi, Mungu alimfundisha Adam ujuzi wa lugha. Alimfundisha Adam jinsi ya kufikiria - ili kutumia maarifa kutatua matatizo, kupanga mipango na kutoa maamuzi na kufikia malengo. Sisi, wana wa Adam, tumerithi stadi hizi ili tuweze kuishi ulimwenguni na kumwabudu Mungu kwa njia bora zaidi.
Wataalamu wa lugha wanakadiria kwamba zaidi ya lugha 3000 mbalimbali zipo duniani leo, zote zikiwa tofauti, hivi kwamba wazungumzaji wa lugha moja hawawezi kuelewa lugha nyingine, japo lugha hizi zote zinafanana sana kimsingi hivi kwamba inawezekana kuzungumza kuhusu “lugha ya binadamu” katika hali ya umoja.[4]
Lugha ni aina maalumu ya mawasiliano inayohusisha kujifunza kanuni ngumu za kuunda na kuchanganya alama (maneno au ishara) ili kutunga idadi nyingi ya sentensi zenye maana. Lugha ipo kwa sababu ya kanuni mbili rahisi, - ambazo ni maneno na sarufi.
Neno ni kioanishi wa jozi nasibu kati ya sauti au ishara na maana. Kwa mfano, kwa Kiswahili neno paka halionekani au halisikiki au halihisiki kama paka, bali linataja mnyama fulani kwa sababu sote tulihifadhi na kukariri uhusiano huu wa jozi tukiwa watoto. Sarufi inatumia seti za kanuni za kuchanganya maneno katika virai (vifungu vya maneno) na sentensi. Inaweza kuonekana kuwa ya kushangaza, lakini wazungumzaji wa lugha zote 3000 tofauti walijifunza kanuni zilezile nne za lugha.[5]
Kanuni ya kwanza ya lugha ni fonolojia - jinsi tunavyotoa sauti zenye maana. Fonimu ni sauti za kimsingi. Tunachanganya fonimu kuunda maneno kwa kujifunza kanuni ya pili: mofolojia. Mofolojia ni mfumo tunaotumia kuunganisha fonimu kwenye mafungu ya sauti na maneno yenye kuleta maana. Mofimu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana katika kuunganisha sauti kuwa maneno katika lugha. Baada ya kujifunza kuunganisha mofimu kuunda maneno, tunajifunza kuunganisha maneno kuwa sentensi zenye maana. Kanuni ya tatu ya lugha inaendesha sintaksia au sarufi. Seti hii ya sheria hubainisha jinsi tunavyounganisha maneno ili kuunda virai na sentensi zenye maana. Kanuni ya nne ya lugha unahusu semantiki - maana maalumu za maneno au misemo na jinsi zinavyojitokeza katika sentensi au miktadha mbalimbali
Watoto wote, bila kujali mahali walipo ulimwenguni, hupitia hatua hizo nne za lugha kwa sababu ya silika au mambo ya asili ya lugha. Mambo haya hurahisisha jinsi tunavyounda sauti za kuongea na kupata ujuzi wa lugha. Mwanachuoni mashuhuri wa isimu Noam Chomsky anasema kuwa lugha zote zinapokezana aina moja ya sarufi ya duniani, na kwamba watoto wanarithi mafunzo ya kiakili ili kujifunza sarufi hii ya ulimwengu wote.[6]
Aya ya tatu ya kutafakari ni juu ya kizazi au nasaba:
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi.” (Kurani 4:1)
Utambuzi kwamba nasaba zote (Afrika, Asia, Ulaya na Amerika) zinaweza kufuatiliwa hadi kwenye asili moja inayojulikana sana kuwa nadharia ya "mitochondrial Eve" (seli hai za vinasaba kutoka Hawa). Kulingana na wanasayansi bingwa[7] na utafiti wa hali ya juu, kila mtu kwenye sayari leo anaweza kufuatilia sehemu maalumu ya urithi wake wa kijenitiki hadi kwa mwanamke mmoja kupitia sehemu ya pekee ya muundo wetu wa kijeni, mitochondrial DNA (mtDNA). Hii mtDNA ya "mitochondrial Eve"imepitishwa kwa karne nyingi kutoka kwa mama hadi binti (wanaume ni wabebaji, lakini hawapitishi) na ipo ndani ya watu wote wanaoishi leo.[8] Inajulikana kama nadharia ya Hawa kwa sababu, kama inavyoweza kubainishwa kutoka hapo juu, hupitishwa kupitia kromosomu X. Wanasayansi pia wanachunguza DNA kutoka kwa kromosomu Y (labda iitwe "nadharia ya Adam"), ambayo hupitishwa kutoka kwa baba hadi mwana na haiunganishwi tena na jeni za mama.
Haya ni maajabu matatu tu kati ya mengi ya uumbaji ambayo Mungu anapendekeza tuyatafakari kupitia aya zake katika Kurani. Ulimwengu mzima, ambao uliumbwa na Mungu, unafuata na kutii sheria zake. Kwa hiyo Waislamu wanahimizwa kutafuta elimu, kuchunguza ulimwengu, na kupata “Ishara za Mungu” katika uumbaji Wake.
Rejeleo la maelezo:
[1] (http://www.faqs.org/nutrition/Met-Obe/Minerals.html)
[2] Anne Marie Helmenstine, Ph.D., Your Guide to Chemistry.
[3] Minerals and Human Health The Rationale for Optimal and Balanced Trace Element Levels na Alexander G. Schauss, Ph.D.
[4] Pinker, S., & Bloom, P. (1992) Natural Language and natural selection. katika Gray. P. (2002). Psychology. 4th ed. Worth Publishers: New York
[5] Plotnick, R. (2005) Introduction to Psychology. 7th Ed .Wadsworth:USA
[6] Gray. P. (2002). Psychology. 4th ed. Worth Publishers: New York
[7] Douglas C Wallace Professor of Biological Sciences and Molecular Medicine. At the University of California.
[8] Discovery channel documentary – The Real Eve.
Ongeza maoni