Diane Charles Breslin, Mkatoliki wa Zamani, Marekani (sehemu ya 1 kati ya 3)
Maelezo: Mkatoliki thabiti anapoteza imani baada ya kusoma Biblia, lakini imani yake isiyoisha kwa Mungu inamwongoza achunguze dini nyingine.
- Na Diane Charles Breslin
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,411
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Ninapoulizwa nilivyosilimu, kila mara ninajibu kuwa siku zote nilihisi kuwa mimi ni muumini wa MUNGU MMOJA pekee, ila nilitambua maana ya dhana hiyo niliposikia kuhusu dini inayoitwa Uislamu, na kitabu kinachoitwa Qur'ani.
Lakini hebu kwanza nianze na muhtasari mfupi wa usuli wangu wa Kimarekani asili ya jadi ya Kiayalandi Kikatoliki.
Nilikuwa Mkatoliki Halisi
Baba yangu aliondoka seminari baada ya miaka mitatu ili kujifundisha kuwa mmishonari. Alikuwa mkubwa wa watoto kumi na watatu, wote waliozaliwa na kukulia katika eneo la Boston. Dada zake wawili wakawa watawa, kama vile halati wake alivyokuwa. Ndugu mdogo wa baba yangu alikuwa pia katika seminari na kuiacha baada ya miaka 9, kabla ya kuchukua nadhiri zake za daima. Nyanya yangu angeamka asubuhi ili kuvaa na kupanda mlima hadi kwa kanisa la mtaa ili ahudhurie misa ya asubuhi huku familia nzima ikiwa imelala bado. Namkumbuka kama mwanamke mwenye msimamo mkali, mwenye fadhili, mwenye kutenda haki, na mwenye nguvu - na ni sifa zisizokuwa za kawaida kwa siku hizo. Nina uhakika hakusikia kuhusu Uislamu, na naomba Mungu amhukumu juu ya imani alizoshikilia moyoni mwake. Wengi ambao hawakuwahi kusikia habari za Uislamu wanamwomba Mungu Mmoja kwa silika za kiasili, ingawa wamerithi maandiko ya madhehebu mbalimbali kutoka kwa mababu zao.
Nilijiunga na shule ya kitalu ya Kikatoliki nikiwa na umri wa miaka minne na nilitumia miaka 12 iliyofuata ya maisha yangu nikizungukwa na dozi nzito za mafundisho ya Utatu. Misalaba ilikuwa kila mahali, siku nzima - ilivaliwa na watawa wenyewe, ilikuwa juu ya kuta za darasani, kwenye kanisa ambalo tulihudhuria takriban kila siku, na takriban kila chumba cha nyumba yetu. Bila kutaja sanamu na picha takatifu - kila mahali ulipoangalia kulikuwa na Yesu mdogo na mama yake Maria - mara wakiwa na furaha, wakati mwingine huzuni, lakini daima walikuwa weupe na wenye maumbile ya kizungu. Malaika mbalimbali na picha za watakatifu pia zingeonekana, kulingana na siku takatifu inayokaribia.
Nina kumbukumbu wazi kuhusu jinsi nilivyokuwa nikichukua maua ya bonde kutoka bustani yetu ili kuyafanya shada ambalo niliweka katika chombo kilichokuwa chini ya sanamu kubwa kabisa ya Mama Maria katika njia ya ukumbi wa juu karibu na chumba changu cha kulala. Hapo ningepiga magoti na kuomba, nikifurahia harufu ya kupendeza ya maua na kutafakari kuhusu jinsi nywele za Maria zilivyokuwa nzuri. Ninaweza kusema kwa uhakika kwamba sijawahi KUMWOMBA au kuhisi kuwa alikuwa na mamlaka na nguvu zozote za kunisaidia. Ilikuwa vivyo hivyo pia nilipochukua shanga za rozari usiku kwenye kitanda changu. Nilirudia dua kama Baba yetu na Maria Mtakatifu na Utukufu uwe kwa Baba na kwa Mwana na Roho Mtakatifu, huku wakati wote nikiangalia juu na kusema kwa moyo wangu wa kweli-- Najua ni Wewe tu, Mungu mmoja Mlezi—Ninayasema mambo haya mengine kwa sababu haya ndiyo yote niliyofunzwa.
Nilipofika umri wa miaka kumi na miwili, mama yangu alinipa Biblia siku ya kuzaliwa kwangu. Kama Wakatoliki hatukuhimizwa kusoma chochote isipokuwa Katekisimu yetu ya Baltimore, iliyoidhinishwa na Vatikani. Uchambuzi wowote wa kulinganisha ulikataliwa na kutupwa mbali. Hata hivyo nilisoma kwa bidii, nikitafuta kujua kile nilichotarajia kitakuwa hadithi kutoka na kuhusu muumba wangu. Nilichanganyikiwa zaidi. Ilikuwa wazi Kitabu hiki kilikuwa ni kazi ya wanadamu, kilikuwa na utata na ilikuwa vigumu kukifahamu. Hata hivyo, mara nyingine tena, hiyo tu ndiyo iliyopatikana.
Mahudhurio yangu ya awali ya kanisa langu limeshuka ujanani mwangu, kama ilivyokuwa kawaida kwa kizazi changu, na wakati nilipofikia miaka yangu ya ishirini, sikuwa na dini rasmi. Nilisoma mengi kuhusu Ubuddha, Uhindu na hata nikajaribu kanisa la Kibaptisti la jirani kwa miezi michache. Zote hazikutosha kuniridhisha, za kwanza zilikuwa geni mno na ya pili ilikuwa ya kimkoa tu. Hata hivyo, licha ya kupita kwa miaka mingi ya kutokuwa na dini na ibada rasmi, hakuna siku ilipita ambapo “sikuzungumza na Mungu” hasa wakati wa kulala ambapo ningemshukuru Mungu kwa baraka zangu zote na kutafuta msaada kwa matatizo yoyote niliyokuwa nikiyapata. Daima ilikuwa ni MMOJA NA WA PEKEE ambaye nilikuwa nazumgumza naye, hakika Alikuwa anasikiliza na nilikuwa na uhakika kuhusu upendo wake. Hakuna mtu aliyewahi kunifundisha chochote kuhusu hili; ilikuwa ni silika ya kiasili tu.
Diane Charles Breslin, Mkatoliki wa Zamani, Marekani (sehemu ya 2 kati ya 3)
Maelezo: Kusoma Uislamu kunamfanya Diane awapende tena Yesu na Maria, lakini upendo wa kweli kwa nuru mpya.
- Na Diane Charles Breslin
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,215
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Wengine
Ilikuwa katika maandalizi yangu kwa shahada ya uzamili ndipo nilisikia mara ya kwanza kuhusu Qur'ani. Hadi wakati huo, kama Wamarekani wengi, niliwajua tu “Waarabu” kama waadui wa siri, waliokuja kuteka nyara ustaarabu wetu. Uislamu haukutajwa kamwe — yaliyotajwa ni Waarabu wachafu tu, na ngamia na mahema yao jangwani. Kama mtoto katika darasa la dini, mara nyingi nilijiuliza watu wengine hao walikuwa kina nani? Yesu alitembea huko Kaana na Galilaya na Nazareti, lakini alikuwa na macho ya rangi ya samawati, watu wengine hao walikuwa nani? Nilikuwa na hisia kwamba kulikuwa na kiunganishi kilichopotea mahali fulani. Mwaka wa 1967 wakati wa vita vya Kiarabu na Israeli, tulipata mtazamo wetu wa kwanza wa watu hao wengine, na walitazamwa wazi na wengi kama maadui. Lakini kwangu mimi, niliwapenda, bila ya sababu dhahiri. Siwezi kueleza kwa nini hadi leo, isipokuwa sasa natambua kuwa walikuwa ndugu zangu Waislamu.
Nilikuwa na miaka 35 niliposoma ukurasa wangu wa kwanza wa Quran. Niliifungua kwa nia ya kuipitia tu kikawaida ili nijue dini ya wenyeji wa eneo ambalo nilikuwa nikilitafiti kwa ajili ya Shahada yangu ya uzamili. Mwenyezi Mungu amesababisha Kitabu kifunguke kwa Surat al-mu'minun aya 52-54:
“Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila kundi likifurahia kwa waliyo nayo. Basi waache katika ghafla yao kwa muda.” (Quran 23:52-54)
Kutoka mara yangu ya kwanza kuisoma, nilijua kwamba huu ulikuwa ukweli usiokuwa na shaka- wazi na imara, ukifunua kiini cha ubinadamu wote na kuthibitisha yote niliyojifunza kama mwanafunzi wa Historia. Kukataa ukweli, ushindani wao usio na mwisho wa kuwa bora na kukataa kwao kwa lengo la kuwepo kwao, yote yalikuwa yamewekwa kwa maneno machache. Mataifa, utaifa, tamaduni, lugha — wote wakihisi ubora wao, huku vitambulisho vyote hivi vinaficha ukweli pekee ambao tunapaswa kufurahia katika kuishiriki- yaani kumtumikia Mungu mmoja, MLEZI MMOJA Aliyeumba kila kitu na Anayemiliki kila kitu.
Bado Nawapenda Yesu na Maria
Nikiwa mdogo nilikuwa napenda kusema maneno haya “Mtakatifu Maria, Mama wa Mungu, tuombee sisi wenye dhambi, kwa sasa na wakati wa kifo chetu, Ameni,” yanayopatikana katika sala ya “Maria Mtakatifu”. Sasa naona ni kiasi gani Maria amekosewa kwa kusifiwa kama mama wa mungu. Ni sifa ya kutosha kumsifu kama mwanamke aliyechaguliwa juu ya wanawake wote ili abebe nabii mkuu Yesu na kumzaa kibikira. Mama yangu mara nyingi alitetea maombi yake ya mara kwa mara ya kuomba msaada kutoka kwa Maria kwa kueleza kwamba yeye pia alikuwa mama na kwamba alielewa huzuni ya mama. Ingekuwa ni muhimu zaidi kwa mama yangu na wengine wote kutafakari jinsi Maria alivyotukanwa na Wayahudi wa wakati wake na kutuhumiwa kufanya dhambi chafu zaidi, ile ya uzinifu. Maria alistahimili yote haya, akijua kwamba angetetewa na Mwenyezi Mungu, na kwamba angepewa nguvu ya kukabili masaibu yote hayo.
Utambuzi huu wa imani ya Maria na tumaini lake katika huruma ya Mungu itamwezesha mtu kutambua nafasi yake kubwa zaidi miongoni mwa wanawake, na wakati huo huo kuondoa kashfa ya kumwita mama wa Mungu, ambayo ni tuhuma kubwa zaidi kuliko ile ya Wayahudi wa wakati wake. Kama Muislamu unaweza kumpenda Maria na Yesu, lakini kumpenda Mungu zaidi kutakupa Paradiso, kwani Yeye ndiye yule ambaye sheria zake lazima uzitii. Atakuhukumu siku ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kukusaidia. Yeye ndiye aliyekuumba, wewe na Yesu na mama yake Maria, kama alivyo muumba Muhammad. Wote walikufa au watakufa - Mungu kamwe hafi.
Yesu (`Isa kwa kiarabu) kamwe hakudai kuwa yeye ndiye Mungu. Badala yake, yeye alisisitiza mara nyingi kuwa yeye ni mtume aliyetumwa. Ninapoangalia nyuma na kutafakari kuhusu tashwishi niliokuwa nao wakati wa ujana wangu, naamini kwamba mizizi yake ilikuwa katika madai ya kanisa kwamba Yesu alikuwa zaidi ya yale ambayo alijiita yeye mwenyewe. Wakuu wa kanisa walitengeneza mafundisho ya kuunda dhana ya Utatu. Ni utoaji huu uliochanganyikiwa wa Torati na Injili za awali (maandiko waliyopewa Musa na Yesu) ambao ni msingi wa suala la Utatu.
Kwa kweli, inatosha kusema tu kwamba Yesu alikuwa nabii, ndiyo, mjumbe aliyekuja na neno la Yule aliyemtuma. Tukimwona Yesu, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake, kwa nuru hii sahihi, basi ni rahisi kumkubali Muhammad, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake, kama ndugu yake mdogo ambaye alikuja na ujumbe huo huo — kuwaita wote kwa ibada ya Mwenyezi Mungu MMOJA, ambaye aliumba kila kitu na ambaye sisi wote tutarudi kwake. Hakuna maana yoyote katika kujadili sifa zao za kimwili. Mwarabu, Myahudi, Mzungu, macho ya samawati au kahawia, nywele ndefu au fupi - zote hazina maana kabisa kwa umuhimu wao kama wabebaji wa ujumbe huo. Kila ninapomfikiria Yesu sasa, baada ya kujua kuhusu Uislamu, ninahisi uhusiano ambao mtu anahisi katika familia yenye furaha - familia ya waumini. Yesu alikuwa “Muislamu”, ambaye anamtumikia Mungu wake aliye juu.
Amri ya kwanza kati ya “Amri Kumi” inasema:
1. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, Usiwe na miungu mingine ila mimi.
2. Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
Mtu yeyote ambaye anajua maana sahihi ya “la ilaha ill-Allah” (hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu) atatambua mara moja mfanano katika ushuhuda huu. Kisha tunaweza kwa hakika kuanza kuleta pamoja hadithi halisi ya manabii wote na kukomesha upotovu.
“Na wao ati husema kuwa Arrahmani Mwingi wa Rehema ana mwana! Hakika mmeleta jambo la kuchusha mno! Zinakaribia mbingu kutatuka kwa hilo, na ardhi kupasuka, na milima kuanguka vipande vipande.” (Quran 19:88-90)
Diane Charles Breslin, Mkatoliki wa Zamani, Marekani (sehemu ya 3 kati ya 3)
Maelezo: Diane anaeleza kukubali kwake kwa Uislamu, maisha yake mapya, na maombi kwa ajili ya Amerika.
- Na Diane Charles Breslin
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 4,478
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Safari Yangu ya Kuelekea Uislamu
Ilichukua miaka mitatu kamili ya kutafiti na kusoma Qurani kabla sijakuwa tayari kutangaza kwamba nilitaka kuwa Muislamu. Bila shaka niliogopa mabadiliko katika nguo na tabia, kama vile kuwa na uhusiano na wanaume na kulewa ambayo nilikuwa nimeyazoea. Muziki na densi zilikuwa sehemu kubwa ya maisha yangu, na bikini na sketi fupi zilikuwa vyanzo vyangu vya umaarufu. Wakati wote huu sikuwa na nafasi ya kukutana na Waislamu wowote, kwani hawakuwa kwa sehemu yoyote katika eneo langu isipokuwa wahamiaji wachache ambao hawakuweza kuongea Kiingereza vizuri walioishi masafa ya umbali wa saa moja kwa gari kwenye msikiti pekee katika jimbo letu wakati huo. Kila nilipotaka kwenda Sala ya Ijumaa ili kujaribu kuangalia dini hii niliyoizingatia, ningeangaliwa kwa macho ya kudadisi kwani nilishukiwa nilikuwa mpelelezi kama ilivyokuwa, na bado iko, katika mikusanyiko mingi ya Kiislamu. Hakukuwa na Mmarekani mmoja Muislamu aliyepatikana wa kunisaidia na, kama nilivyosema, ilikuwa nadra sana kwa wakazi wote wahamiaji kuwakaribisha watu.
Katikati ya awamu hii ya maisha yangu, baba yangu alikufa kutokana na saratani. Nilikuwa naye wakati wa kifo chake na nilishuhudia kwa uhakika malaika wa kifo akiondoa roho yake. Alishikwa na hofu huku machozi yakitiririka juu ya mashavu yake. Maisha ya anasa, maboti ya raha, vilabu, magari ghali... kwa yeye na mamangu, yote yakiwa matokeo ya mapato ya riba, na sasa yamekwisha.
Nilihisi hamu ya ghafla ya kuingia kwenye Uislamu kwa haraka, huku nikiwa na wakati bado, na kubadili njia zangu na kutoendelea kutafuta kwa upofu kile nilicholelewa nikiamini kuwa ni maisha mazuri. Muda mfupi baada ya hapo nilikuja Misri, na kushiriki safari ndefu ya polepole kupitia muujiza wa lugha ya Kiarabu na kugundua ukweli ulio wazi - Mungu ni Mmoja, ni wa Milele na Daima; Ambaye kamwe hakuzaliwa wala hakuzaa na hakuna kitu kama Yeye.
Pia ni usawa kati ya wanadamu ulionivuta sana kwa dini hiyo. Nabii Muhammad, Rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema kuwa watu ni kama meno ya kichanuo, wote ni sawa na bora zaidi ni anayemcha Mungu. Katika Qur'ani tunaambiwa kuwa walio bora zaidi ni wachamngu. Ucha Mungu unahusisha upendo na kumcha Mungu peke yake. Hata hivyo kabla hujaweza kuwa mcha Mungu, lazima ujifunze Mungu ni nani. Na kumjua ni kumpenda. Nilianza kujifunza Kiarabu ili kusoma neno la Mwenyezi Mungu kwa lugha ya Kiarabu kama ilivyofunuliwa.
Kujifunza Qurani kumebadilisha kila nyanja ya maisha yangu. Sitaki tena kuwa na anasa zozote za kidunia; si magari si nguo si safari, vyote haviwezi kunivuta kwa mtandao ule wa tamaa zisizo na maana, uliokuwa umeniteka nyara mbeleni. Ninaishi maisha mazuri ya muumini; lakini kama wanavyosema... hayajaingizwa tena moyoni... yamo mikononi tu. Siogopi kuwapoteza marafiki zangu wa zamani au jamaa zangu - Mungu akiamua kuwaleta karibu, basi iwe hivyo, lakini najua kwamba Mungu ananipa hasa kile ninachohitaji, si zaidi, si chache. Sijisikii tena kuwa na wasiwasi wala huzuni, wala sina wasiwasi na yaliyonipita, kwa sababu niko salama katika utunzaji wa Mungu - MLEZI MMOJA Niliyemjua siku zote lakini sikujua jina lake.
Maombi kwa Marekani
Ninamwomba Mwenyezi Mungu amruhusu kila Mwamerika nafasi ya kupokea ujumbe wa Umoja wa Mungu kwa njia rahisi, moja kwa moja... Wamarekani, kwa sehemu kubwa, hawajui habari kuhusu theolojia sahihi ya Kiislamu. Lengo kila mara lipo kwa siasa, ambayo inalenga matendo ya wanadamu. Ni wakati muafaka kwa sisi kulenga na kushughulika na matendo ya manabii ambao wote walikuja kutuongoza kutoka kwa giza na kutupeleka kwa mwangaza. Hakuna shaka kwamba giza lipo katika msukosuko unaoathiri Amerika sasa. Nuru ya kweli itatuhusisha sisi sote, na ikiwa mtu atachagua kufuata au kukataa njia ya Kiislamu, hakuna shaka kwamba kuizuia au kuzuia wengine kuifuata kwa hakika kutasababisha taabu zaidi. Ninajali sana masilahi ya nchi yangu, na nina hakika kwamba kujifunza zaidi kuhusu Uislamu kutaongeza uwezekano wa matumaini yangu kutimia.
Ongeza maoni