Diane Charles Breslin, Mkatoliki wa Zamani, Marekani (sehemu ya 1 kati ya 3)
Maelezo: Mkatoliki thabiti anapoteza imani baada ya kusoma Biblia, lakini imani yake isiyoisha kwa Mungu inamwongoza achunguze dini nyingine.
- Na Diane Charles Breslin
- Iliyochapishwa mnamo 17 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 6,177 (wastani wa kila siku: 6)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Ninapoulizwa nilivyosilimu, kila mara ninajibu kuwa siku zote nilihisi kuwa mimi ni muumini wa MUNGU MMOJA pekee, ila nilitambua maana ya dhana hiyo niliposikia kuhusu dini inayoitwa Uislamu, na kitabu kinachoitwa Qur'ani.
Lakini hebu kwanza nianze na muhtasari mfupi wa usuli wangu wa Kimarekani asili ya jadi ya Kiayalandi Kikatoliki.
Nilikuwa Mkatoliki Halisi
Baba yangu aliondoka seminari baada ya miaka mitatu ili kujifundisha kuwa mmishonari. Alikuwa mkubwa wa watoto kumi na watatu, wote waliozaliwa na kukulia katika eneo la Boston. Dada zake wawili wakawa watawa, kama vile halati wake alivyokuwa. Ndugu mdogo wa baba yangu alikuwa pia katika seminari na kuiacha baada ya miaka 9, kabla ya kuchukua nadhiri zake za daima. Nyanya yangu angeamka asubuhi ili kuvaa na kupanda mlima hadi kwa kanisa la mtaa ili ahudhurie misa ya asubuhi huku familia nzima ikiwa imelala bado. Namkumbuka kama mwanamke mwenye msimamo mkali, mwenye fadhili, mwenye kutenda haki, na mwenye nguvu - na ni sifa zisizokuwa za kawaida kwa siku hizo. Nina uhakika hakusikia kuhusu Uislamu, na naomba Mungu amhukumu juu ya imani alizoshikilia moyoni mwake. Wengi ambao hawakuwahi kusikia habari za Uislamu wanamwomba Mungu Mmoja kwa silika za kiasili, ingawa wamerithi maandiko ya madhehebu mbalimbali kutoka kwa mababu zao.
Nilijiunga na shule ya kitalu ya Kikatoliki nikiwa na umri wa miaka minne na nilitumia miaka 12 iliyofuata ya maisha yangu nikizungukwa na dozi nzito za mafundisho ya Utatu. Misalaba ilikuwa kila mahali, siku nzima - ilivaliwa na watawa wenyewe, ilikuwa juu ya kuta za darasani, kwenye kanisa ambalo tulihudhuria takriban kila siku, na takriban kila chumba cha nyumba yetu. Bila kutaja sanamu na picha takatifu - kila mahali ulipoangalia kulikuwa na Yesu mdogo na mama yake Maria - mara wakiwa na furaha, wakati mwingine huzuni, lakini daima walikuwa weupe na wenye maumbile ya kizungu. Malaika mbalimbali na picha za watakatifu pia zingeonekana, kulingana na siku takatifu inayokaribia.
Nina kumbukumbu wazi kuhusu jinsi nilivyokuwa nikichukua maua ya bonde kutoka bustani yetu ili kuyafanya shada ambalo niliweka katika chombo kilichokuwa chini ya sanamu kubwa kabisa ya Mama Maria katika njia ya ukumbi wa juu karibu na chumba changu cha kulala. Hapo ningepiga magoti na kuomba, nikifurahia harufu ya kupendeza ya maua na kutafakari kuhusu jinsi nywele za Maria zilivyokuwa nzuri. Ninaweza kusema kwa uhakika kwamba sijawahi KUMWOMBA au kuhisi kuwa alikuwa na mamlaka na nguvu zozote za kunisaidia. Ilikuwa vivyo hivyo pia nilipochukua shanga za rozari usiku kwenye kitanda changu. Nilirudia dua kama Baba yetu na Maria Mtakatifu na Utukufu uwe kwa Baba na kwa Mwana na Roho Mtakatifu, huku wakati wote nikiangalia juu na kusema kwa moyo wangu wa kweli-- Najua ni Wewe tu, Mungu mmoja Mlezi—Ninayasema mambo haya mengine kwa sababu haya ndiyo yote niliyofunzwa.
Nilipofika umri wa miaka kumi na miwili, mama yangu alinipa Biblia siku ya kuzaliwa kwangu. Kama Wakatoliki hatukuhimizwa kusoma chochote isipokuwa Katekisimu yetu ya Baltimore, iliyoidhinishwa na Vatikani. Uchambuzi wowote wa kulinganisha ulikataliwa na kutupwa mbali. Hata hivyo nilisoma kwa bidii, nikitafuta kujua kile nilichotarajia kitakuwa hadithi kutoka na kuhusu muumba wangu. Nilichanganyikiwa zaidi. Ilikuwa wazi Kitabu hiki kilikuwa ni kazi ya wanadamu, kilikuwa na utata na ilikuwa vigumu kukifahamu. Hata hivyo, mara nyingine tena, hiyo tu ndiyo iliyopatikana.
Mahudhurio yangu ya awali ya kanisa langu limeshuka ujanani mwangu, kama ilivyokuwa kawaida kwa kizazi changu, na wakati nilipofikia miaka yangu ya ishirini, sikuwa na dini rasmi. Nilisoma mengi kuhusu Ubuddha, Uhindu na hata nikajaribu kanisa la Kibaptisti la jirani kwa miezi michache. Zote hazikutosha kuniridhisha, za kwanza zilikuwa geni mno na ya pili ilikuwa ya kimkoa tu. Hata hivyo, licha ya kupita kwa miaka mingi ya kutokuwa na dini na ibada rasmi, hakuna siku ilipita ambapo “sikuzungumza na Mungu” hasa wakati wa kulala ambapo ningemshukuru Mungu kwa baraka zangu zote na kutafuta msaada kwa matatizo yoyote niliyokuwa nikiyapata. Daima ilikuwa ni MMOJA NA WA PEKEE ambaye nilikuwa nazumgumza naye, hakika Alikuwa anasikiliza na nilikuwa na uhakika kuhusu upendo wake. Hakuna mtu aliyewahi kunifundisha chochote kuhusu hili; ilikuwa ni silika ya kiasili tu.
Ongeza maoni